Zana
Ligi Kuu

Aussems anapowakataa Kotei, Niyonzima na kumkubali Zana ni matokeo niliyotaraji

Sambaza....

MOJA kati ya makosa makubwa waliyofanya Simba SC ni kumuongezea mkataba kocha Mbelgiji, Patrick Aussems kwa kigezo kimoja tu- kufikia malengo aliyopewa na klabu wakati akisaini mkataba wa mwaka mmoja katikati ya mwaka uliopita.

Ndiyo, inawezekana Aussems alifikia malengo aliyopewa- kuifikisha timu walau hatua ya makundi katika michuano ya Caf Champions League na kutetea ubingwa wa ligi kuu. Samba iliyokuwa ikishiriki ligi ya mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka mitano, ilifanikiwa kuziondoa Mbabane Swallows ya Swazland, Nkana FC ya Zambia katika hatua ya kwanza na ile ya pili na kutinga hatua ya makundi yaliyohusisha timu 16.

Aussems, kocha wa Simba

Ushindi mara tatu na vipigo vitatu ( ikiwemo vile vya kihistoria vya 5-0, 5-0) katika michezo sita katika kundi lililokuwa na timu za Al Ahly ya Misri, AS Vita Club ya Congo DR na JS Sauora kutoka Algeria, suluhu-tasa na kichapo cha 4-1 kutoka kwa TP Mazembe katika robo fainali; kimpira hayakuwa matokeo mazuri hata kama klabu ilifikia lengo la kwanza kimataifa- kufika hatua ya makundi.

Mbinu mbovu za kujilinda dhidi ya Vita Club pale Kinshasa zilipelekea Simba kuchapwa 5-0, na Aussems hakwenda na funzo lolote Alexandria siku kumi baadae na kiasi cha kuchapwa tena 5-0 na Al Ahly huku magoli yote ya mabingwa hao wa kihistoria wa Caf yakifungwa ndani ya dakika 45’ za kipindi cha kwanza tu.

Naamini licha ya kwamba Simba ilifanikiwa kuzifunga timu zote hapa Dar es Salaam katika hatua ya makundi, bado Aussems kama kocha alionyesha udhaifu wa kimbinu katika kujilinda pale Congo DR na kule Misri. Simba haikuwa imewahi kupoteza mechi yoyote ya Caf kwa tofauti ya magoli matano ndani ya dakika 90’ lakini chini ya Aussems hilo lilitokea tena katika njia ya ‘mfuatano’, unapigwa tano Congo DR kisha zinafuata 5-0 nyingine Misri.

Aussema akitoa maelezo kwa wachezaji

Nilidhani Simba ingetazama kwanza baadhi ya michezo muhimu ya msimu uliopita na kuamua kuhusu Aussems lakini kwa vile klabu hiyo imekuwa na tabia ya ‘kupiga hatua kimazungumzo’ tu, kivitendo wakampa mkataba kocha ambaye kwa kutazama msimu wake wa kwanza na malengo yanayotajwa kila leo ya kupiga hatua kimataifa wamempa mkataba kocha ambaye hata hawezi kuifanya timu yake ipate magoli dhidi ya timu zenye mbinu kali za kujilinda- rejea Yanga 0-0 Simba, Simba 1-0 na Azam FC 0-0 Simba mechi ambazo unaweza kupima vizuri mbinu za kocha kama Aussems, au zile za Vita Club 5-0 Simba, Al Ahly 5-0 na Saoura 2-0 Simba.

KUWAACHA KOTEI, HARUNA NIYONZIMA…..

Tayari kuna mvutano mkubwa kati ya uongozi wa klabu na kocha huyo kuhusu suala la usajili. Aussems hawataki viungo, Mghana, James Kotei na Mnyarwanda, Haruna Niyonzima- kama kocha anajua ni kwanini hawahitaji wachezaji hao ambao walikuwa na msimu mzuri wao binafsi ukiachana nay ale kiasi ya klabu msimu uliopita.

Kotei (Kushoto)

Labda Aussems angetoa sababu za kiufundi kwanini anataka kuwaondoa Haruna na Kotei na uongozi kama una watu hasa wa mpira unaweza kuchanganua na kukubaliana nae au kumkatalia ili kutoondoa ubora kidogo uliokuwepo msimu uliopita. Pamoja na mbinu zake mbovu za kujilinda na kushambulia, Aussems kwa kiasi kikubwa alibebwa mno na James kwa msimu wote.

Mghana huyo alijitolea kwa kadri alivyoweza, alikuwa juu kinidhamu na Zaidi aliweza kuisaidia Simba katika ulinzi na mashambulizi ndiyo maana hakuna aliyehoji baada ya kushinda tuzo ya kiungo bora wa mwaka katika tuzo za klabu yake mwezi uliopita. Unaweza kuwa na sababu gani za kiufundi, kiubora na kinidhamu za kutuambia Kotei haitajiki Simba?

 

Si kimbinu na ufundi tu wa kiufundishaji ambao Aussems hana, bali hata macho yake hayawezi kutambua ubora wa mchezaji ndiyo maana ameendelea kung’ang’ania kubaki na Mburkina Faso, Zana Coulibally aliyemsajili mwishoni mwa mwaka uliopita. Zana ambaye amefeli vibaya na wale wachezaji wake aliowaleta na kuwajaribu katika michuano ya SportPesa mwanzoni mwa mwaka huu ni kielezo kingine tosha kuwa kocha huyo hana ubora wowote na hakufaa kupewa muda Zaidi.

Simba walipaswa kutazama malengo yao mapya na kumpima Aussems kama anaweza kuyabeba kabla ya kumpatia muda zaidi, uliona kiwango alichomalizana nacho msimu Mzambia, Chama? Kiungo huyo alikuwa akishuka siku hadi siku tofauti na wakati alivyokuja hii ni sababu nyingine ya kuthibitisha kuwa mbinu za kocha huyo zitaendelea kushusha viwango vya mchezaji mmoja mmoja na timu kiujumla.

Usajili wake wa Zana na kitendo cha kupendekeza kuachwa kwa Kotei na Niyonzima ni mwanzo tu wa majuto watakayopitia Simba msimu ujao chini ya Mbelgiji huyo, kimbinu na ufundi wataanguka Zaidi msimu ujao na utakuwa ni ‘msimu wa mateso kwao’

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x