Sambaza....

Geofrey Mwashiuya, alitingisha nchi kipindi cha usajili wake, kijana mdogo kutoka Mbozi ambaye aliifanya mitaa ya Kariakoo kuhamia kwa muda mjini Mbozi.

Kila jicho kutoka karikakoo lilimwangalia kwa jicho la matamanio, watu wa Mbozi nao wakawa na viburi baada ya kuona kiwango cha tamaa kimezidi kwa kijana huyu.

Kila aliyekuwa anakuja , watu wa Mbozi walitamka bei huku wakiwa wameangalia pembeni.

Hawakuwa na muda wa kukaa na kufanya mazungumzo ya kubembelezana, na kiburi hiki kilikuja mara baada ya kuwagonganisha mabwana wawili.

Mwisho wa siku bwana mkubwa Yanga akafanikiwa kumnasa Geofrey Mwashiuya, watu wakawa na matumaini makubwa sana kwa kijana huyu.

Wengi waliamini atakuwa kufanya vizuri na kikosi cha Yanga kwa sababu ya aina ya uchezaji wa Yanga.

Yanga ina utamaduni wa kushambulia kupitia pembeni, hivo kuwa na wachezaji wenye kasi na wenye uwezo wa kutengeneza magoli na kufunga kupitia pembeni ni mtaji mkubwa wa Yanga.

Ndiyo maana hata Mwalimu George Lwandamina hakusitia kumchukua Emmanuel Martin mara baada ya kumshuhudia kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya JKU ya Zanzibar.

Emmanuel Martin aliwafunga Yanga magoli mawili, George Lwandamina aliona kuna kitu cha ziada kutoka kwa Emmanuel Martin.

Kufunga kwake kupitia pembeni kuliweza kumshawishi George Lwandamina kuwa Emmanuel Martin anauwezo mkubwa wa kuendana na utamaduni wa Yanga.

Utamaduni wa kushambulia kupata magoli kupitia pembeni.

Emmanuel Martin naye alikuja akiwa na matumaini mazito ndani ya kikosi cha Yanga kama ilivyokuwa kwa Geofrey Mwashiuya.

Wote walikuwa wachezaji wenye kasi, kasi ambayo iliwapa nafasi ya moja kwa moja kuingia kwenye kikosi.

Watu wengi walikaa na kusubiri kipi ambacho watakuja kufanya hawa wachezaji wawili lakini cha ajabu mpaka sasa hivi hawa wachezaji wawili na wenyewe wapo wamekaa wakifurahia kuwepo Kariakoo.

Kariakoo ni tofauti sana na Mbozi, kuna wakati ukiwa umetoka Mbozi kuja kariakoo waweza kuona hapo ndipo mwisho wa ndoto zako.

Ndiyo maana Emmanuel Martin karidhika na Geofrey Mwashiuya akiwa hana hasira.

Emmanuel Martin anaona hana mtu wa kupigania naye namba katika kikosi cha Yanga, ndiyo maana kakaa na kuridhika kuvaa jezi ya Yanga.

Hili Geofrey Mwashiuya halioni, yeye kakaa chini huku akiwa anachekelea tu hana hasira ya kumuona Emmanuel Martin alivyoridhika.

Hawapambani kutoka sehemu waliyopo na kwenda sehemu nyingine bora, wao wanaona walipo ndipo wamefika.

Hiki kitu ni moja ya madhara ya vijana wadogo kufika kwa haraka katika timu kubwa wakiwa na umri mdogo.

Mara nyingi huona kama ndiyo wamefika kwenye safari ƴyao ambayo walikuwa wanaiota siku nyingi.

Akikosekana mtu wa kuwatoa kwenye giza hili vijana wa aina hii hupotea kwa haraka sana.

Na ndicho kitu ambacho kinaonekana kwa kina Emmanuel Martin na Geofrey Mwashiuya, wakiendelea kuwa hivi kama walivyo siku zao za kuishi Yanga zinahesabika sana.

Hakuna juhudi yoyote wanayoonesha kupigania vipaji vyao, wakipata nafasi ya kucheza hawachezi kulingana na mitazamo ya wengi waliyokuwa nayo wakati wamesajiliwa.

Ni wakati sahihi kwao kupata hasira na kuacha kuridhika kuendelea kuwepo Yanga.

Wanatakiwa waitumie Yanga kama daraja la wao kufika mbali , wawe na ndoto kubwa ambazo watatakiwa kuzitimiza kwa hali na mali.

Siyo muda mzuri kwao wao kuona kucheza Yanga ndiyo kila kitu kwenye maisha ya mpira .

Sambaza....