Sambaza....

Kuelekea  mchezo wa pili katika kundi D, Simba SC dhidi ya AS Club Vita utakaopigwa kule Kinshasa nchini Congo, kocha wa Wekundu wa Msimbazi, Patrick Auissems ameelezea jinsi anavyowafahamu Vita na jinsi atavyowakabili katika mchezo huo.

“Tunajua wataanza kutushambulia kwa  kasi kama ilivyo kawaida kwa klabu kama Vita katika michezo yake ya nyumbani”

Kocha mkuu wa Klabu ya Simba
Kocha mkuu wa Klabu ya Simba

“Kila mechi huwa tunajitahidi kuumiliki mpira na kujaribu kutengeneza nafasi nyingi za magoli, hata hapa tutafanya hivyo, sisi hatukuja kujilinda tumekuja kucheza”

Taarifa

Tarehe Muda Ligi Msimu Mwisho
19/01/2019 7:00 pm Klabu Bingwa Afrika Kundi D 2018-2019 90'

Kwa upande hali ya kiwanja, Aussems amedai kuwa, hawana hofu na uwanja utakaotumika kwa kigezo kuwa ni wa nyasi bandia, huku akidai kuwa hata wao wamevizoea viwanja vya nyasi bandia.

“ Muda wote tulipokuwa Zanzibar kwa ajili ya Mapinduzi Cup, tulikuwa tukifanya mazoezi katika uwanja wa nyasi bandia, kwahiyo sidhani kama uwanja utakuwa ni tatizo kwetu” alisema Aussems.

AS Vita Club mazoezini

Aussems aliongeza kwa kusema kuwa, kila klabu ina nafasi ya kufanya vizuri katika mchezo huo, kwahiyo matumaini kwa vijana wake kupata ushindi bado ni mkubwa.

Kwa upande wake Daktari wa Wekundu hao, Yassin Gembe amesema kuwa, wao kama idara ya matibabu wamejipanga vizuri kuhakikisha mambo yanakuwa sawa .

“Hii ni kama vita, sisi kama madaktari wa timu, tupo muda wote, lolote likitokea kwa wachezaji au benchi la ufundi, tuko tayari kwa muda wowote na hali yoyote” alisema daktari huyo.

Simba SC inaingia katika mchezo huo ikiwa inaongoza katika msimamo wa kundi D, ikiwa na alama 3 na magoli matatu kibindoni, ikifuatiwa na Al ahly ya Misri yenye alama 3 na magoli mawili. AS Club Vita inaingia katika mchezo huo ikiwa na hasira baada ya kujeruhiwa katika  mchezo wake wa kwanza  dhidi ya Al ahly baada ya kukubali kichapo cha goli 2-0 ugenini.

Sambaza....