Sambaza....WATER Bwalya aligongesha ‘mtambaa wa panya’ mara moja, akapoteza nafasi tatu za wazi- ndani ya kipindi cha kwanza, ikiwemo ili aliyopiga kiki iliyokwenda nje ya lango akiwa ndani ya hatua saba kutoka lango la Simba SC dakika ya mwisho ya kipindi cha kwanza.

Pamoja na nahodha huyo wa Nkana Red Devils FC kushindwa kufunga katika dakika 90’ za mchezo wa kwanza, makosa yake yanapaswa kuwakumbusha beki ya Simba makosa yao kadhaa na kama hawatajirekebisha katika mchezo ujao wa Jumapili hii, wamnaweza kujikuta nje ya michuano licha ya kwambna walifanikiwa kufunga goli linaloweza kuwa muhimu sana kwao katika mchezo wa kwanmza huko Kitwe, Zambia.

Okwi (kushoto) Na Mohamed Hussein (Kulia) wakimkaba Hassan Kessy (Katikati) huku Meddie Kagere kwa mbali akifuatilia.

BEKI YA SIMBA INAMUHITAJI ZAIDI JUUKO

Hassan Kessy aliweza kutengeneza goli moja kwa mpira wake wa krosi kumaliziwa vizuri na Ronald Kampamba dakika ya 28’ na mlinzi huyo wa kulia wa Nkana aliweza kuwa tatizo kubwa kwa Simba na hata majaribio yote matatu yaliyofeli ya Bwalya yalitokana na mipira ya krosi iliyopigwa na mlinzi huyo wa timu ya Taifa ya Tanzania.

Kessy alikuwa kati ya wachezaji bora katika mchezo huo wa Jumamosi iliyopita, alimfanya Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ kushindwa kupandisha timu na wakati mfumo wa kocha Patrick Aussems ukihitaji zaidi nguvu ya walinzi wa pembeni, Mghana, Nicolas Gyan alikuwa na dakika ‘mbaya zaidi’ kwa kipindi chote cha kwanza katika beki ya kulia.

Murushid Juuko

Alisumbuliwa mno na mfunmgaji wa goli la pili la Nkana, alipitwa kwa chenga dhaifu na hakuonekana kujiamini. Kasi ya Nkana katika wings na uwezo wa washambuliaji wake wa kati, Bwalya na Kampamba ni hatari na uwezo wa beki ya Simba ulioonyeshwa juzi ni dhahiri bado wa kazi ngumu ya kufanya na tayari wapo karibu na mlango wa kutokea katika michuano hiyo ya ligi ya mabingwa Afrika.

MIAKA MINNE ILIYOPITA WAKATI Simba ilipomuondoa kikosini kiungo na mchezaji wake muhimu zaidi wakati huo, marehemu Patrick Mafisango katika msafara wa kwenda Algeria kurudiana na ES Setif katika mchezo wa Caf Confederations Cup, sababu moja tu ilitazamwa na wana Simba wote. Utovu wa nidhamu.

Mafisango ilisemekana alikuwa amekwenda katika mazoezi ya timu yake akiwa amelewa siku mbili kabla ya timu kusafiri. Uongozi ulimuweka kando, lakini nilitoa wazo ambalo baadae lilifanyiwa kazi. Sikutazama sababu yoyote nje ya zile za kimpira. Nje, ya uwanja Mafisango alikuwa mkosefu- kama alikwenda akiwa amelewa kweli katika mazoezi.

Lakini baada ya kusikia utetezi wake nilitazama kwa nini Simba inaweza kuanguka Algers kama haitakwenda na Mafisango. Ndiye alikuwa mcheezaji muhamasishaji ndani ya uwanja muda wote wa mchezo- nilimtazama mara zote klabuni Simba kama ‘nahodha asiyevaa beji begani.’ Alikuwa bora katika kupandisha timu na kushambulia kwa pasi za umbali mrefu, si hivyo tu, alikuwa mwenye hamu na michuano ya Caf nah ii ndiyo ilikuwa sababu ya kuondoka Azam FC Juni 2011 na kujiunga Simba.

Mafisango ( mwenyezi Mungu Amrehemu alikuwa na ubora wa juu katika ukabaji kuliko wachezaji wote wa Simba wakati huo na wiki moja kabla ya safari ya Setif kiungo huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Rwanda alikuwa ametawala mechi katika ushindi wa Simba 2-0 Setif jijini, Dar. Nakumbuka Simba walikuwa pungufu ndani ya dakika 7 tu baada ya Juma Nyosso kuondolewa uwanjani kwa kadi nyekundu katika mchezo wa marejeo.

Mafisango akarudi kucheza beki ya kati na Kelvin Yondan na wakati matokeo yakiwa Setif 3-0 Simba, na dakika ya pili kati ya nne za nyongeza, Mafisango alikimbilia pasi kutoka kwa mlinzi wa kati na haraka akageuka nao na kupiga pasi ndefu kwa Emma Okwi ambaye aligeuka akiwa amelipa mgongo lango la Setif kwa kasi aligeuka na kuachia ‘kombora’ lililotinga nyavuni na Simba wakafuzu kwa sheria ya goli la ugenini baada ya mechi mbili kumalizika kwa sare ya kufangana 3-3.

Kazi ile ya Mafisango ilikuwa baada ya shinikizo la kuwataka uongozi kumjumuhisha kiungo huyo katika msafara wa Algers na kuja kumuadhibu baada ya kurejea kama itabaika ni kweli atakuwa amekosea. Na kwa sasa nawashauri tena, si lazima ila ni muhimu sana kwao. Kocha Aussems amrejeshe beki wa kati Mganda, Jjuuko Murshid katika program za mchezo wa marejeo dhidi ya Nkana.

Na wakati huu, Shomari Kapombe akiwa nje ya kikosi kutokana na majeraha ni lazima Erasto Nyoni achezeshwe katika beki ya kulia. Ni lazima kwa sababu hiyo ni nafasi ambayo anaimudu vizuri miaka na miaka amekuwa akicheza kama beki wa kulia au kushoto. Beki ya kati Pachal Wawa na Jjuuko imeonekana kufiti vizuri .

Pascal Wawa kushoto

Wawa na Nyoni waliiweka sana majaribu timu yao katika mchezo wa Kitwe kutokana na wote wawili kupendelea kukabia macho, huku wakitorokwa kirahisi na washambuliaji wa Nkana wakati wa mipira ya wazi inapoelekezwa golini mwao.

Ukiwa na golikipa mwenye kiwango cha ‘wasiwasi’ katika michuano ya kimataifa kama Aishi Manula, na beki inayokabia macho na inayopitika kirahisi pembeni na kati mwa uwanja kama hii ya Gyan, Wawa, Nyoni na Zimbwe Jr usianze kuanza ‘gwaride’ la kusherekea kufuzu kwa makundi hasa mbele ya washambuliaji ambao tayari wamefunga mara mbili katika dakika 90 tu na kupoteza nafasi zaidi ya nne walizotakiwa kuzigeuza magoli.

Beki ya Simba bado ni uchochoro, na wala usiwaze kuhusu 1-0 Dar es Salaam, Nkana watakuja hapo na kufunga tena na si ajabu ni wao wakapita kwa goli la ugenini kwa beki hii ya Simba na golikipa ‘asiyeona kiki za mbali.’

Sambaza....