Sambaza....

WAKATI ni timu tano tu zimemudu kufunga magoli 15 ama zaidi katika ligi kuu Tanzania Bara msimu huu, timu nane zimefunga magoli chini ya kumi na nyingine saba zimefunga magoli kati ya kumi-14.

Hii inamaanisha kuwa makocha wengi ´wamefeli´ katika mbinu za ufungaji. Katika michezo 11 waliyokwishacheza, mabingwa watetezi Simba SC wamefanikiwa kufunga jumla ya magoli 23 (wastani wa magoli mawili kwa kila mchezo) na ndio timu iliyofunga magoli mengi zaidi kufikia mzunguko wa 14 katika ligi.

Msimamo

PosTimuPWFAGDPts
1Simba SC382977156293
2Yanga SC382756272986
3Azam FC382154213375
4KMC FC381340251555

Yanga SC wanafuatia baada ya kufunga magoli 17 katika michezo kumi waliyokwishacheza. Mabingwa wa 2013/14 na vinara wa ligi hiyo Azam FC wenyewe wamefanikiwa kufunga magoli 15 katika michezo 12.

Mtibwa Sugar FC walio nafasi ya nne wamefunga magoli 17 katika michezo 14, wakati Mbeya City FC walio nafasi ya saba wanakamilisha orodha ya timu tano ambazo angalau zimefunga magoli 15+.

BIASHARA UNITED.


Timu hii kutoka Mkoani Mara inaburuza mkia katika ligi. Ikicheza ligi kuu kwa mara ya kwanza timu hiyo imefanikiwa kushinda mchezo mmoja tu ( Singida United 0-1 Biashara United)- ushindi ambao waliupata siku ya ufunguzi wa msimu Agosti 23.

Katika michezo 13 wamefanikiwa kufunga magoli manne tu. Wamekuwa wakijilinda vizuri kwani hadi sasa wameruhusu magoli tisa tu katika nyavu zao. Wanapaswa kurekebisha haraka matatizo yao ya ufungaji kama kweli wanataka kusalia katika ligi msimu ujao.

Waziri Junior Akitambulishwa wakati akijiunga na Azam

Straika, Wazir Junior ameonyeshwa mlango wa kutokea katika kikosi cha Azam FC baada ya miezi 18 ya kukosa nafasi. Junior anapatikana kwa mkopo tu hivyo Biashara United wanaweza kumchangamkia ili awasaidie kumaliza sare na vipigo vinavyotokana na ubutu wa safu yao ya ushambuliaji.

Biashara licha ya kushinda mchezo mmoja tu, wametoa sare mara saba na kupoteza michezo mitano.

JKT TANZANIA


Inashangaza kiasi kuona wakiwa nafasi ya sita na pointi 19 wakati wamemudu kufunga magoli saba tu katika michezo 13 waliyokwishacheza. Timu hii inapaswa pia kurejea sokoni katika usajili huu na kusaini walau wafungaji wawili.

Nchimbi

Ditram Nchimbi ameshindwa kupata nafasi katika timu ya Azam FC hivyo naye ni mchezaji aliyewekwa sokoni na JKT Tanzania hawapaswi kujiuliza kuhusu namba kumi huyo wa zamani wa Mbeya City FC na Mji Njombe FC.

TANZANIA PRISONS


Kama ilivyo kwa JKT Tanzania, Prisons nao wamekuwa hoi katika nafasi ya 19 ya msimamo kutokana na ubutu wa wafungaji wake. Wamefunga magoli saba tu katika michezo 14, wameshinda mchezo mmoja, sare saba na kupoteza mara sita.

Wanaweza kuondoka mkiani kama wataongeza wafungaji na wanaweza kumrejesha Mohamed Rashid aliyewafungia magoli 12 msimu uliopita walipomaliza ndani ya nne bora. Rashid ameshindwa kucheza mchezo wowote wa ligi tangu alipojiunga Simba na tayari ameambiwa anaweza kuondoka.

LIPULI FC


Kocha, Suleimani Matola baada ya kumpoteza Adam Salamba aliyejiunga Simba msimu huu aliwasaini Paul Nonga na Keneth Masumbuko lakini bado Lipuli FC wameshindwa kupata magoli ya kutosha.

Ikiwa nafasi ya 17 katika msimamo, Lipuli imefanikiwa kufunga magoli saba tu katika game 13 walizokwishacheza. Wameshinda michezo miwili tu, wamepoteza mara tano na sare sita.

Kaheza

Matola anajaribu kumuwania mshambulizi Marcel Kaheza aliyeshindwa kupata nafasi ya kucheza kikosini Simba. Kaheza alifunga magoli 15 akiichezea Majimaji FC msimu uliopita ni mfungaji ambaye anaweza kuwaondoa Lipuli chini ya msimamo.

AFRICAN LYON, MWADUI, NDANDA & ALLIANCE


Mwadui FC na Alliance School wamefunga magoli nane nane katika michezo 13 ( Mwadui) na 14 (Alliance). Lyon na Ndanda FC wenyewe wamefunga magoli tisa tisa katika michezo 13 ( Lyon) na 14 ( Ndanda).

Timu hizi sambamba na Biashara, JKT, Prisons na Lipuli ndio pekee ambazo zimefunga magoli chini ya kumi katika ligi. Kwa namna yoyote wanatakiwa kusaini washambuliaji wakati huu wa usajili mdogo.

Mbao FC ( magoli kumi), Ruvu Shooting ( magoli 12), Kagera Sugar FC ( magoli 11), Coastal Union ( magoli 11), KMC FC ( magoli kumi), na Singida United ( magoli 12) nazo zinapaswa kuongeza makali katika ufungaji kwani wanaweza kuanguka zaidi kutokana na uchache wa magoli wanayofunga.

Sambaza....