Sambaza....

MRISHO Ngassa ameifungia Yanga SC goli lake la kwanza tangu aliporejea klabuni hapo kwa mara nyingine katika vipindi vyake vitatu tofauti.

Hapana shaka, nitakaposema Ngassa yuko mbali na uwezo wake wa nyuma, lakini bila shaka ndiye mchezaji aliyejizolea mashabiki wengi wa Yanga katika ‘muongo‘ wa kwanza wa karne mpya.

Mwishoni mwa mwaka 2006, Yanga ilimsaini Ngassa kwa mara ya kwanza akitokea Kagera Sugar FC. Alikuwa sehemu muhimu ya wachezaji walioisaidia ‘Timu ya Wananchi‘ kushinda mataji mawili mfululizo ya ligi kuu- 2007/08, 2008/09.

Baada ya miaka minne mizuri Ngassa alijiunga Azam FC katikati ya mwaka 2010 kwa usajili wa rekodi wakati huo- Tsh. 96 millioni. Alishinda tuzo binafsi ya ufungaji bora wa ligi kuu msimu wa 2010/11 akifunga magoli 16.

Hakuwa na mafanikio makubwa kiuchezaji ndani ya Azam FC ambayo ilimpeleka Simba SC Agosti 2012 kwa usajili wa mkopo na licha ya Simba kuingia nae makubaliano rasmi ya kuitumikia kwa misimu miwili, Ngassa alitambulishwa Yanga mwezi Juni, 2013.

Usajili huo ulipelekea TFF kumfungia Ngassa na kutakiwa kuilipa Simba kiasi kisichopungua Tsh.40 millioni. Yanga ilimlipia Pesa hiyo huku ikimkata kidogokidogo katika malipo yake.

Ngassa (kulia)

Baada ya kukosa michezo tisa ya Mwanzo wa msimu wa 2013/14, Ngassa alifunga magoli tisa katika michezo saba likiwemo moja dhidi ya Simba katika mchezo alioweka ‘nadhiri‘ ya kuchoma nyumba/magari yake moto kama hatofunga goli katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 3-3- Yanga wakiongoza 3-0 hadi mapumziko.

“Ni mechi ninayoikumbuka kwa mambo mengi. Kuongoza 3-0 dhidi ya Simba ndani ya dakika 45 za kwanza kisha mechi kumalizika 3-3 ilituchanga sisi kama wachezaji, lakini ndio mchezo wa soka ulivyo. Saa nzima ya mchezo tuiitawala sisi. Tulicheza vizuri, kuna watu wanaweza kusema mwalimu alifanya mabadiliko mabaya, lakini waelewe ule ndio mpira wa miguu- dakika tisini uamua matokeo.”  anasema Ngassa.

Ngassa aliondoka Yanga mara baada ya kuisaidia kushinda ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2014/15. Alisaini mkataba wa miaka minne Free State United ya ligi kuu Afrika Kusini, lakini kufikia September 2016, Ngassa aliamua kuvunja mkataba.

Ngassa amekuwa mgumu kusema sababu iliyopelekea kulazimisha kuondoka Afrika Kusini baada ya mwaka mmoja tu. Alijiunga Fanja FC ya Oman lakini kufikia November 2016 akaondoka kiutata na kujiunga Mbeya City FC mwezi Disemba 2016.

Baada ya mwaka mmoja ulioshindwa kumuibua upya, Disemba 2017 akajiunga Ndanda FC na alitumia miezi mitano kati ya sita na timu hiyo ya Mtwara kupandisha kiwango chake na sasa katika umri wa miaka 29 (unaotambulika) amerejea Yanga.

“ Nahitaji kurudi katika kikosi cha timu ya Taifa. Nimekuwa nje ya Taifa Stars kwa miaka miwili lakini nahitaji kurudi. Nitafanya kazi yangu vizuri Yanga na hii ni timu itakayo nisaidia kurejea timu ya Taifa.”  anasema Ngassa akiwa na haraka na kuongeza.

“Mimi si mzee, Nimekuwa na uzoefu mkubwa sasa na sitazami nyuma ili kujilaumu au kumlaumu yeyote. Naendelea kujifunza kila siku na nitajitahidi kuifanya kazi yangu vizuri.”

Ngassa anaamini Yanga ina kikosi kinachoweza kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.

“Kama tunapata pointi tatu katika mchezo wa ligi, bila kujali tumechezaje ni bora kuliko kucheza vizuri na kupoteza mechi. Lakini kama timu na mchezaji mmoja mmoja lazima tusahihishe na kujitahidi kupunguza makosa yetu uwanjani. Kucheza vizuri na kushinda mechi. Tunaweza kushinda ubingwa kama tutajituma kwa msimu wote.”

Sambaza....