Tahariri

Mwamnyeto ameamini katika mchakato na umemlipa.

Sambaza....

Moja ya kauli bora ya muda wote kwa wapambanaji ni ‘Trust The Process’ Yaani kuamini katika mchakato. (Naam).

Hii ni kwenye kila eneo la upambanaji, wapambanaji wengi wanaotoboa huamini katika mchakato na imani yao huwalipa maradufu na maisha husonga. (Amini)

Rejea mitaa ya Avic Town pale Kigamboni zilipo kambi za Yanga, utakutana na mpambanaji anayeamini katika mchakato. Wanamuita Nondo, Bakari Mwamnyeto. (Ukuta wa Chuma)

Kuna upepo mbaya ulipita kwa Kitasa hiki, alipata majanga kwa kupata msiba mkubwa wa familia yake, mke na mtoto, lakini akakaza kiume na mapambano yakaendelea. (Ujasiri)

Haikuwa rahisi kwake lakini watu baki wakahitaji aendelee kuwa kama zamani kitu ambacho hakiwezekani kiuhalisia bali kinahitaji muda na Imani. (Ustahimili)

Nondo alistahimili na kuyafanya machozi yake yasionekane nje bali yavujie ndani kwa ndani yakitelemka kwenye moyo wa Imani. (Uanaume).

Bakari Mwamnyeto akimthibiti mshambuliaji wa Real Bamako.

Wakati Nondo akijitafuta, watu baki walimbeza na kutaka kuaminisha umma kuwa hafai lakini yeye alikaa kimya na kuendelea kuamini mchakato. (Imani)

Siku zote daraja halipotei bali kuna muda ubora unapungua. Misukosuko ya hapa na pale ilimfanya Nondo kupungua kidogo ubora siku kadhaa nyuma lakini sio kiviile. (Kawaida)

Mwamba hakuogopa kwani aliendelea kuamini katika mchakato, kupanda na kushuka ni kawaida kwenye mchakato na sasa ameanza kujipata upya, kwa kasi kubwa anarejea kwenye daraja lake. (Ubora)

Usinga wa Yanga umerejea kwenye mkono wake wa kushoto, Namba tano imerejea kuwa eneo lake, uwanjani ni Ofisi yake na ‘First Eleven’ ya Yanga ni wafanyakazi wenzake na yeye akiwa Kingozi wao. (Nahodha).

Kikosi bora cha raundi ya nne Kombe la Shirikisho Afrika, ukuta unaundwa na yeye akiwa mchezaji pekee wa Yanga aliyeingia kwenye timu hiyo ya mafundi tupu. (Wajuzi)

Muda umefika sasa wa kutaja jina lake kwa kuzingatia itifaki mkianza na Herufi kubwa kwa nguvu ile ile iliyotumika kulidharilisha. (Heshima).

Sambaza....