Sambaza....

Meneja wa klabu bingwa nchini Hispania FC Barcelona Ernesto Valverde amekitaka kikosi chake kujifunza kupambana bila ya nahodha na mshambuliaji Lionel Messi, ambaye atakosa baadhi ya michezo, kufuatia kupata jeraha la mkono mwishoni mwa juma lililopita, wakati wa mchezo wa La Liga dhidi ya Sevilla CF.

Valverde ametoa tamko la kuwahimiza wachezaji wake kujenga ujasiri wa kucheza bila Lionel Messi, alipokua katika mkutano na waandishi wa habari uliozungumzia mpambano wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya makundi, ambao utawakutanisha dhidi ya Inter Milan, leo usiku kwenye uwanja wa Camp Nou.

Meneja huyo aliyejiunga na FC Barcelona msimu wa 2017/18 amesema, kuna ulazima wa wachezaji wake wakajitambua na kuamini hakuna mchezaji zaidi ya klabu, na kama watakua na mawazo ya kumtegemea Messi, watakua wanakosea.

“Tunapaswa kushirikiana kwa pamoja, mmoja wetu anapoumia ama kuwa na matatizo mengine ya kimaisha, hatuna budi kujiamini na kuendeleza mapambano dhidi ya adui zetu,” alisema Valverde.

“Tuna wachezaji wengi wenye uwezo wa kuziba pengo la Messi, ninaamini katika mchezo wetu dhidi ya Inter Milan mtaliona hilo, kuumia kwa mshambuliaji huyu sio mwisho wa mapambano, tutaendelea na tutahakikisha tunapigania alama tatu muhimu.”

FC Barcelona, ambao walishindwa kuendelea na michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu uliopita baada ya kufungwa na AS Roma katika mchezo wa robo fainali, msimu huu wameanza vyema kwa kuzichapa Tottenham na PSV, hali ambayo inawafanya kuongoza msimamo wa kundi B, wakiwa na alama sita sawa na Inter Milan, lakini tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, inawaweka juu mabingwa hao wa Hispania.

Hata hivyo usiku wa leo FC Barcelona watakua na kazi ya kufanya kufuatia wapinzani wao (Inter Milan) kuwa na muendelezo mzuri katika michezo waliyocheza siku za karibuni, kwani mpaka sasa wamecheza michezo saba bila kupoteza hata mmoja.

Kufuatia hali hiyo, Valverde aliwaambia waandishi wa habari kuwa: “Inter Milan ni moja ya klabu kubwa barani Ulaya na ina wachezaji wazuri, sishangazwi na muendelezo wao mzuri wa kushinda michezo saba mfululizo. Wana tabia ya kutokukata tamaa, lakini naamini vijana wangu leo watapigana ili kuwapa upinzani wa kweli.”

Sambaza....