Stori

Uongozi Azam Fc: Fiston Mayele Ametuambia Ukweli

Sambaza....

Baada ya mchezo wa nusu fainali kumalizika kati ya Singida Big Stars dhidi ya Yanga na Yanga kupata ushindi wa bao moja bila, mshambuliaji wa Yanga Fiston Mayele alitoa maoni yake jinsi anavyoitazama Azam Fc ambao wanakutana nao fainali.

Mayele ambae ataiongoza Yanga kumenyena na Azam Fc katika fainali mkoani Tanga amesema Azam ina wachezaji wazuri sana lakini wanakamia mechi kubwa tuu za Simba na Yanga halafu wanapoteza katika na timu ndogo.

Msemaji wa Azam Fc Zakaria Thabit maarufu kama Zakazakazi ameyachukulia maneno hayo katika hali chanya na kuwapa ujumbe wa wachezaji wake wa Azam Fc kuelekea pia mchezo dhidi ya Yanga Tanga.

Azam Fc dhidi ya Simba katika mchezo wa nusu ya kombe la FA.

“Ahsante sana Fiston Mayele kwa kutuamsha kwenye usingizi mzito. Japo maneno haya yanauma lakini yawezekana ndiyo ukweli na yanatakiwa kuchukuliwa kwa mtazamo chanya badala ya hasi,” alisema Zakari Thabit kupitia ukurasa wake wa instagram na kuongeza:
“Manahodha wetu Bruce Kangwa na Sospeter Banyana ongeeni na wachezaji wenzenu wa Azam Fc na kukitafakari anachokisema huyu jamaa hapa.

Hivi ndivyo yeye anavyowachukulia na yawezekana wachezaji wengine pia klabuni kwake na hata nje ya klabu yake na mitaani kwa ujumla. Mpira unachezwa hadharani na kila mmoja anaona na kutafsiri anavyoweza yeye ndiyo kawatafsiri hivi nyinyi.”

Zaka pia ameongeza Mayele yupo sahihi na anaongea kitu ambacho ana uhakika nacho kwasababu mpira unachezwa hadharani.

Khalid Aucho wa Yanga katikati ya wachezaji wa Azam Fc Tape Edinho na Prince Dube.

“Mayele anayasema haya kwa kujiamini na kwa uhakika, kwa sababu ushahidi anao.
Msimu huu kwenye ligi kuu tumepoteza mechi saba hadi sasa, sita kati ya hizo ni dhidi ya timu aina ya Namungo kama anavyosema hapo.
Yeye anaamini kwamba kama tungecheza kwa kiwango sawa na tulichocheza dhidi yao, tungeepuka vipigo hivi, na yawezekana kuvuna alama tatu.”

“Kwa bahati mbaya hajui ugumu mnaokutana nao kwenye hizo mechi na wala hajisumbui kuwaza kwamba yawezekana na nyie mnakamiwa na hao akina Namungo. Yeye anaangalia jambo moja tu kwamba mlistahili kushinda hizo mechi…basi!

Hii ina maana kwamba anaheshimu uwezo wenu na anaamini kwamba mnachokipata uwanjani hamstahili…anataka mpate zaidi. Ni jukumu lenu kubadili hali hii…heshima huwa inatafutwa, haiji yenyewe.  Mara zote dawa huwa chungu sana. Anayekukumbusha kunywa dawa anataka upone, usimuone kama mbaya wako, kwamba labda ndiye aliyekuroga. Tuanze kumthibitishia Tanga,” alimaliza Zakaria Thabit.

Sambaza....