Sambaza....

Kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amekubali ombi la kukutana na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo hapo kesho lakini kwa sharti la kutozungumzia suala linalomuhusu mlinda mlango Beno Kakolanya.

Zahera ameuambia mtandao huu kuwa alipata taarifa kuwa kuna wachezaji waliowahi kuichezea Yanga wametaka kuzungumza naye lakini katika kudodosa alifahamu kuwa walitaka kuzungumza naye kuhusu suala la Beno hivyo ametahadhalisha kuwa kama wanataka kufanya mazungumzo basi kusiwepo na suala hilo.

“Kuna mtu alinipigia simu akasema wanataka kukutana na mie tuzungumze, wanasema wanataka kuinipongeza kwa kazi nzuri ninayofanya, nikasema kama ni kuhusu timu hakuna tatizo, ila nimemwambia sipendi kuzungumza lolote kuhusu Beno Kakolanya,”

“Wamesema wanakuja lakini sio kwa mambo ya Beno Kakolanya, wanakuja kwa ajili ya mambo mengine, nikawaambia sawa, kwa sababu mambo ya Beno siwezi kurudia nyuma, kwangu mie nimeshasahau na nimemaliza nayo hata kabla sijakwenda Ufaransa, na wameniambia kuwa Beno ameandika barua ya kuvunja mkataba sasa nashangaa kuona mara watu wananipigia simu kutaka kuzungumza, nimesema hapana,” Zahera ameongeza.

Zahera amesema hatokubali kwa mchezaji mwingine afanye kama alivyofanya Beno Kakolanya na ikitokea basi atachukua maamuzi sawa na hayo ambayo ameyachukua kwa Kakolanya ambaye ni kipa namba mbili wa timu ya Taifa.

Ikumbukwe kwamba toka Taifa Stars iliporejea kutoka nchini Lesotho, Beno Kakolanya aligoma kufanya mazoezi akishinikiza kulipwa madai yake ikiwemo fedha ya usajili na mishahara ya miezi kadhaa.

Sambaza....