Blog

Bao la Chirwa liwakumbushe Simba kuhusu usajili huu wa Shamte

Sambaza....

OBREY Chirwa alitumia nguvu na akili mara moja tu kati ya dakika 90’ za mchezo wa fainali ya kombe la FA na kufunga goli ambalo kwa hakika linawakumbusha Simba SC juu ya mtazamo wao wa usajili katika dirisha ili.

Simba inafukuzia saini za ‘wachezaji wao wawili’ wa zamani ambao walichezea Lipuli FC katika mchezo wa fainali ya FA siku ya Jumamosi iliyopita katika uwanja wa Ilulu, Lindi dhidi ya mabingwa Azam FC. Mlinzi wa kati, Haruna Shamte alikubali kukaa nje ya eneo lake baada ya kuzidiwa nguvu, ujanja na mbinu na Chirwa ambaye alifunga goli pekee ‘lisilotarajiwa’ mbele ya mlinzi huyo mkakamavu.

SHAMTE…..

Shamte amewahi kucheza Simba kwa vipindi viwili tofauti, na sasa inasemekana klabu yake hiyo ya zamani imekuwa ikimsaka katika usajili unaondelea nchini ili kuwa mbadala wa baadhi ya wachezaji ambao wanaondoka kwa sababu za kimpira klabuni hapo.

Haruna Shamte akipiga mpira wa faulo kwenye moja ya mechi msimu 2017/18

Kwa Simba kurudi tena kwa Shamte naona ni muendelezo uleule tu wa kufanya usajili ambao hauwezi kuongeza ubora unaotakiwa katika malengo yao ya Caf. Kumsaini mlinzi huyu ni jambo ambalo linaweza kuongeza nguvu katika beki ya pembeni si eneo la kati.

Shamte ana uwezo wa kucheza vizuri Zaidi ya Mburkina Faso, Zana Colibally katika beki ya pembeni na kama Simba inamuhitaji mchezaji huyo aliyekuwa na msimu mzuri katika kikosi cha Lipuli FC basi watalazimika kumtumia kama mlinzi wa pembeni na si beki wa kati kama wanavyokusudia.

Zana (Kushoto)

Taarifa zilizosambaa jana ya kujitonesha kwa mlinzi Shomari Kapombe licha ya mlinzi huyo wa Taifa Stars kukanusha kuumia ni ishara kuwa Simba inatakiwa kufanya usajili Zaidi katika nafasi ya beki wa kulia. Sijui kwanini kocha Patrick Aussems anaendelea kumng’ang’ania, Zana mchezaji ambaye ameonyesha wazi hawezi kuisaidia klabu kwa kiwango cha kimataifa.

Kuyumba kwa ‘afya’ ya Kapombe kunafungua milango kwa Shamte kutua tena Simba lakini kwa kile ambacho Chirwa alikifanya mbele ya mlinzi huyo Jumamosi iliyopita kinapaswa kuwafungua macho Zaidi Simba kuhusu ubora wa mchezaji huyo –kama wanakusudia kumsaini kama mbadala wa wachezaji wengine wanaoondoka katika eneo la beki ya kati.

Siafiki usajili wa Shamte kama mlinzi wa kati Simba, lakini naweza kukubali kama mlinzi huyo atasajiliwa kama ‘kiraka wa muda’ katika beki ya kulia sehemu ya kwanza kabisa ambayo Simba wanapaswa kuijaza kwa umakini mkubwa kufuatia kuyumba kwa Kapombe na kushindwa kufikia kiwango cha juu kwa Zana.

Chirwa akishangilia goli lake dhidi ya Lipuli wakati wa Fainali ya ASFC

Ni wazi Simba haitakuwa imekosea sana kumpa mkataba Shamte kama mbadala wa beki ya kulia, lakini kama wanahitaji kumsaini kama mlinzi wa kati ni wazi bao la Chirwa vs Lipuli wikendi iliyopita linapaswa kuwakumbusha kuwa mchezaji huyo bado hawezi kukabiliana na washambuliaji wa kiwango cha juu hasa wale wa kimataifa, hivyo wanapaswa kutazama kwingine Zaidi.

Bao la Chirwa limedhihirisha kuwa Shamte si mlinzi mzuri wa kati na ni onyo la kwanza la Simba kuelekea usajili wao mpya msimu huu wa kiangazi.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x