Sambaza....

Katika mojawapo ya matoleo ya mwisho mwisho ya Jarida la mpira wa miguu-Number10 mwezi April, 2011 niliandika makala iliyobebwa na kichwa cha habari ´Abdulhalim Humud: Aliipenda Simba, ila changamoto zimemshinda´.

Ndani ya makala yale nilimchambua, Humud katika mambo makubwa matatu. Kipaji, nidhamu, na changamoto. Hakika si rahisi kupata kipaji kipya katika soka la Tanzania kama alichonacho, Humud. Atabaki kuwa yeye tu.

Ukiachana na mambo mengine yote, Humud ni kipaji tunachoweza kusema ´hakitazaliwa tena´ katika soka letu. Kama mwanasoka niliyetumia muda mwingi kucheza katika nafasi anayocheza mchezaji huyo wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania, kuna wakati nashindwa kumtazama Humud katika mambo yake mabaya.

KIPAJI.

Kumiliki kiungo kwa stahili ya mchezo wa kuvutia- pasi ndefu timilifu kutoka upande hadi upande wa uwanja. Soka la nguvu, ufundi na uwezo wa kutengeneza nafasi za magoli, mbio zake katikati ya uwanja zilinifanya mara nyingi kumlinganisha na gwiji wa zamani wa Ujerumani, Michael Ballack. Humud alinivutia kwa hamasa yake akiwa uwanjani.

Siwezi kumuhukumu moja kwa moja kwa makosa yake ya kiubinadamu na kusahau kile alichonacho miguuni mwake. Bado hatafananishwa, hatafikiwa, lakini ni ukweli ulio wazi ni kipaji kilichopotea kutokana na harakati zake-Njia ya maisha aliyochagua. Si rahisi kubadilisha njia ya maisha ya mtu mwingine. Hivyo ndivyo harakati zilivyo.

NIDHAMU

Nilikuwepo Jamhuri Stadium, Morogoro wakati Tanzania Prisons wakiichapa Ashanti United katika mchezo wa ligi kuu Ndogo mwaka 2007. Kama ilivyo kawaida yangu, nilikaa upande wa jukwaa la Simba na mbele kulikuwa na benchi la ufundi na wachezaji wa akiba wa Prisons.

Humud (Kulia) akiwa na klabu ya Simba SC

Kwa robo saa yote ya kwanza katika mchezo huo Prisons walikuwa wametawala kiungo. Mashabiki wakereketwa wa Ashanti walisogea hadi katika senyege zinazofanya uzio wa kuwazuia kuingia uwanjani. Wakawa wanampigia kelele kocha wa timu yao na kumshinikiza amtoe Humud.

Akiwa mchezaji wa timu ya Taifa, Humud aliboa sana. Muda mwingi alikuwa akipoteza mpira na hakuwa na msaada katika kuutafuta. “mtoe bishooo huyo, kocha tunakuomba umtoe Humud…” Mashabiki wa Ashanti walipaza sauti zao kwa namna ya kuimba. Misango Magae ´Diego´ aliteka shoo, akampoteza kabisa Humud.

Akiwa nahodha wa Ashanti katika mchezo huo, Humud alikitupa chini kitambaa cha unahodha wakati akitoka kumpisha Ramadhani Chombo ‘Redondo’. Haitoshi, akaamua kutokaa kwenye benchi la wachezaji wa akiba na hiyo ilikuwa ni mara yake ya mwisho kuichezea Ashanti United.

Hii ilikuwa tabia mbaya ya kwanza kufanywa hadharani na mchezaji huyo mwenye kipaji kikubwa cha kuiga pasi na kichezesha timu. Baadae akiwa Simba SC msimu wa 2010/11 na kwa muda mfupi msimu wa 2013/14, akiwa mchezaji wa Azam msimu wa 2011/12-2013, Coastal Union msimu wa 2014/15, kwa muda mfu[pi akiwa Majimaji FC msimu uliopita na sasa KMC FC kote huko Humud amekuwa ‘mtovu wa nidhamu’

Kwa msimu mmoja aliokuwa Real King FC ya Afrika Kusini mwaka mmoja uliopita, Humud pia hakudumu na sasa amejimaliza kwa kashfa ya kujaribu kuwatongoza wake na marafi wa kike wa wachezaji wenzake katika klabu change ya KMC. Hakuna tena matarajio makubwa- kwamba atafikia kiwango cha juu kwa mara nyingine kama wakati ule akiwa Mtibwa Sugar FC msimu wa 2009/10.

Wengi hawapendezwi na namna anavyowazungumzia wapinzani wake mchezoni lakini kwa aina ya uchezaji wake, hamasa aliyonayo na akiwa katika ubora wake Humud ni ‘dimba la ukweli’ lakini sasa ni sawa na kipaji kilichoshindwa kututimizia matarajio tuliyoweka dhidi yake kutokana na aina ya harakati zake alizoamua kuishi.

CHANGAMOTO

Wakati alipoamua kujiondoa mwenyewe katika kikosi chja Ashanti kwa sabnabu za kuzomewa na mashabiki wa timu yake mwaka 2007, Humud aliona si rahisi kwake kuweza kutamba tena mbele ya Chombo kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha mara baada ya kuchukua nafasi yake dhidi ya Prisons. Akaamua kuachana na soka kwa muda.

Humud akiwa na Azam FC

Mwishoni mwa mwaka 2008 alisajiliwa na Mtibwa na alitumia miezi 18 Turiani kutulia na kuonyesha kiwango bora kilichomfanya kurejeshwa timu ya Taifa mwaka 2009 baada ya kukosekana kwa miaka miwili. Samba ilimsaini Juni 2010, lakini uwepo wa Mkenya, Jerry Santo ulimfanya Humud kususa mara kadhaa kujiunga na timu kwa madai ya kukosa nafasi.

Humud si mshindani wa namba hasa pale anapokuta kmchezaji bora akicheza nafasi yake. Huwa na visingizio vingi na mwisho wa siku Simba iliamua kumpeleka Azam FC ili kumpata Mnyarwanda, marehemu Patrick Mafisango Juni 2011. Huko Azam FC nako alikutana na vita kubwa ya namba katika eneo lake na tabia ileile ya kususa susa iliwafanya ‘LambaLamba’ kuachana naye; pia tabia ya kutongoza wake wa wachezaji wenzake ikichangia kwa kiasi kikubwa.

Kushindwa kwake kukabiliana na changamoto za kuwania nafasi ndiko kumemfanya Humud kushindwa kuwika akiwa klabu kubwa nchini licha ya kwamba wakati fulanifulani aliweza kufanya vizuri. Kushindwa kwake kuwatafsiri wanawake kumemmaliza kwa namna ya kusikitisha mchezaji huyu wa aina yake. Humud alisahau kwamba wanawake ni watu dhaifu- si katika kuwakubali wanaume pia hadi katika kuwaangamiza pale wanapoamua kufamnya hivyo.

HITIMISHO

Kipaji chake, nidhamu yake na changamoto ndiyo zimemuangusha Humud kufikia matarajio yetu lakini si kuwatongoza wake ama marafiki wa kike wa wachezaji wenzake kwa sababu hizo ni tabia kibinadamu. Humud aliamini katika kipaji chake tu, hakuipenda nidhamu wala hakuwa tayari kwa changamoto ya kuwania nafasi.

Sambaza....