Blog

Malengo ya MO Dewji yanaukweli gani bila kutumia namba?

Sambaza kwa marafiki....

Mwana-hisa mkuu wa klabu ya Simba SC, Mohamed Dewji ‘MO’ amekuwa akisema mara kwa mara ndoto yake ni kuifanya klabu hiyo kufikia ‘matawi’ ya juu katika soka la Afrika, huku akitolea mfano klabu mahiri na kubwa kama Al Ahly, TP Mazembe, Raja Casablanca, Mamelodi Sundowns, Esperance Tunis, as Vita Club na nyinginezo ambazo zimekuwa na ‘mazoea’ ya kufika mbali-pengine kutwaa mataji ya Afrika.

Mtazamo wake ni mzuri, lakini bila mwekezaji huyo kujipanga na ‘kutumia namba’ kwa hakika sioni mafanikio yoyote mbeleni. Simba tayari ipo katika mfumo wa soko la hisa kufuatia mabadiliko yao ya uendeshaji wa mfumo wa klabu na jambo hilo limekuwa likitazamwa kama msaada wa kuisaidia klabu hiyo bingwa Tanzania Bara kujiendesha vizuri kiuchumi, lakini malengo hasa ya klabu yamepangwa katika mpangilio gani?.

Mo Dewji wakati wa mechi ya kirafiki kati ya Simba SC na Sevilla FC

Kufika robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika msimu uliopita ni mafanikio makubwa kwa klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi, na hili limewezekana baada ya klabu kutumia kiasi kikubwa cha pesa katika isajili, ulipaji wa mishaara, posho na bonsai mbalimbali.

Wakati, MO anaingia katika klabu hiyo mwanzoni mwa msimu uliopita kama mwekezaji, alisema kuwa Simba inatakiwa kufika hatua ya makundi na jukumu hili alipewa kocha Mbelgiji, Patrick Aussems. Simba ilifika hatua hiyo ya makundi na bahati nzuri Zaidi klabu ilifanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili katika kundi lililokuwa na klabu za Al Ahly (waliomaliza katika nafasi ya kwanza), AS Vita Club ( iliyomaliza katika nafasi ya tatu), na JS Saoura kutoka Algeria ambayo ilimaliza nafasi ya mwisho katika kundi.

Mo Dewji(kushoto) wakati wa mechi dhidi ya TP Mazembe, Robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2019.

Kumaliza katika nafasi ya pili katika kundi hili na kutolewa katika hatua ya robo fainali kwa jumla ya magoli 4-1 na TP Mazembe haikuwa bahati mbaya bali klabu hiyo ya DR Congo na nyingine zote kubwa ambazo MO anaota kuipeleka Simba katika ‘tawi’ walilopo wababe hao wa Afrika kutokana na malengo yao wanayojiwekea.

MO anatakiwa kutumia ‘namba’ ili afanikiwe katika malengo yake, namaanisha anatakiwa kugawa malengo anayokusudia ya klabu katika maeneo matatu na kutuambia; Malengo ya muda mfupi ya klabu ni yapi? Yatatumia muda gani?

Malengo ya muda mfupi ni klabu kuendelea kukua kiuchumi na kimpira, kushinda mataji ya ndani na kujaribu kufika hatua ya makundi au Zaidi katika michuano ya Caf, ndani ya muda huu mfupi klabu na watendaji watakuwa wakijenga uwezo na uzoefu wao kidogokidogo. Kwa mfano, MO alitakiwa kusema baada ya misimu ‘fulani’ Simba itakuwa wapi katika soka la Afrika na si kusema tu kuwa ndoto yake ni kuifanya Simba kuwa kubwa kama ilivyo klabu nyingine zilizofanikiwa Afrika.

Kila malengo ya ukweli yanaendana na namba, kwa mfano MO anaweza kusema ndani ya miaka mitano ijayo malengo ya klabu ni kufikia nusu fainali ( malengo ya miaka mitano) na kujaribu kutwaa ubingwa huo ndani ya miaka kumi ( malengo ya muda mrefu), na kushinda kila kikombe cha ndani ( malengo ya muda mfupi) lakini kitendo cha yeye kuendelea kusema tu ‘Simba inataka kushindana na klabu kubwa Afrika’ bila kusema itatumia muda gani kufika huko ni sawa na ‘udanganyifu’ kwasababu malengo ya kweli yanaendana na namba.

MO ana ndoto kubwa lakini hatujui ni muda gani atatumia kufanikisha ndoto hizo kuwa kweli! Labda ni wakati sasa wa MO kusema malengo ya muda mfupi ya klabu yatatumia muda gani, malengo ya kati na yale ya muda mrefu –yote yanapaswa kuendana na namba, atuambie ndani ya miaka miwili, mitano , au kumi Simba itakuwa wapi na si kusema tu kama yupo katika ‘baraza la wazee’

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.