Sambaza....

HIVI karibuni kocha mkuu wa Yanga SC, Mcongoman, Zahera Mwinyi alimzungumzia kwa mara nyingine kiungo wake mshambulizi Ibrahim Ajib na kile alichokisema ni kitu kilekile nilichowahi kusema, na ambacho Juma Ndabile ( aliyekuwa meneja wa Ajib) aliwahi kumwambia-namba kumi huyo.

Zahera alijibu swali la mwandishi alimuuliza kama Ajib anastahili kuitwa katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars) kutokana na kufunga magoli matatu na kupiga pas inane za magoli katika michezo saba ya Yanga katika ligi kuu msimu huu. Kocha huyo, alijibu- si nukuu rasmi- “ Hakuna mchezaji kama Ajib katika nchi hii, lakini timu ya Taifa inahitaji mchezaji anayejituma.”

Wakati kocha Emmanuel Amunike alipotangaza orodha yake ya wachezaji wa Stars kabla ya michezo miwili iliyopita dhidi ya Cape Verde na jina la Ajib kutokuwepo, wapo waliohoji ni kwanini kiungo huyo mshambulizi hajaitwa. Niliwahi kuulizwa hilo pia na wadau Fulani katika mjadala, na niliwaambia, “ Hakuna nafasi ya Ajib katika timu ya Taifa.”

Ndiyo, kama Farid M,ussa, Kelvin Sabato, Yahya Zayd, Shaaban Idd, John Bocco wanasubiri nafasi inamaanisha Ajib anatakiwa kuendelea kufanya vizuri katika klabu yake . kwa mtazamo wa kawaida, Ajib ni kweli amepiga pas inane na kufunga magoli matatu katika ligi, lakini mchezaji huyo bado anacheza kivivu mno jambo ambalo kwa kocha mwenye uchaguzi mpana wa wachezaji hawezi kumchukua.

Mtazame, Kelvin Sabato- napenda juhudi zake na naamini siku ambayo atapewa nafasi ya kuichezea Taifa Stars atafanya mambo makubwa sana. Ajib ni kweli ana kipaji- ana uwezo mzuri wa kumiliki mpira, kupiga pasi za mwisho na kufunga magoli yasiyotarajiwa, lakini timu ya Taifa inahitaji wachezaji wanaojituma kama Bocco, Zayd, Chilunda, Farid na si mchezaji anayeamini kupiga pasi tu na kufunga inatosha kumfanya awepo uwanjani.

Katika mchezo uliopita wa Yanga 3-0 Alliance School, Ajib licha ya kwamba alipiga pasi mbili za magoli na kufunga goli moja aliipa wakati mgumu timu yake kutokana na kutojali kupoteza kwake pasi na uchezaji wa taratibu wakati wa kushambulia na kuzuia. Mchezaji wa namna hii hawezi kukupa majibu mazuri katika mchezo mgumu ambao wapinzani wataingia na mikakati juu yake.

Ni rahisi kumzuia Ajib kama mpinzani hatacheza mbali nae nah ii inatokana na uvivu wa kiasili alionao mchezaji huyo wa zamani wa Simba. Hivi majuzi niliona mahala mtu mmoja aliyejitambulisha kama meneja wa Ajib akisema kwamba mchezaji huyo atasaini mkataba mpya kwa dau lisilopungua Tsh. 200 milioni.

Kwa mtazamo wake wa chini anaamini Ajib ana thamani hiyo lakini kiukweli uchezaji wake hauwezi hata kuzidi thamani ya Tsh.70 milioni. Katika michezo yote mitatu ya ligi aliyoichezea Yanga dhidi ya mahasimu wao Simba, Ajib hakuwahi kuonekana, pia alishindwa kucheza kwa kiwango kizuri katika michezo dhidi ya Azam FC msimu uliopita na ndani ya miezi 12 iliyopita ameichezea timu ya Taifa michezo isiyozidi miwili-thamani hiyo ya Tsh. 200 Milioni anaitoa wapi?

Ajib

Hajashinda taji wala tuzo yoyote binafsi katika miezi yake 15 ya kwanza akiichezea Yanga. Ndabile aliachana na Ajib kutokana na kuona mchezaji huyo hawezi kucheza nje ya Tanzania kutokana na uvivu wake katika mazoezi na hakutaka kuwa meneja wa kusubiri mkataba uishe na kutazama aende Simba au Yanga ama Azam FC. Humu ndipo kiwango cha Ajib kinamruhusu kwa sasa na yote hii inatokana na ukweli kwamba hakuna timu ya nje ambayo inaweza kumchukua mchezaji asiye na msaada.

Kauli ya Zahera kwamba, Ajib hana nafasi ya kuichezea Taifa Stars kutokana na uvivu wake ni ya kweli kabisa, ameunga mkono mawazo yangu yaliyopita nay ale ambayo Ajib aliwahi kuambiwa na Ndabile. Kumbuka mchezaji huyu alifeli katika majaribio yake Haraas Hodood ya Misri mwaka mmoja na nusu uliopita kutokana na uvivu wake na si kipaji alichonacho.

Kama anahitaji kurejea Stars ni jukumu lake mwenyewe kutazama mchezo wake na kujikosoa kutokana na makosa mfululizo yanayojirudia rudia katika uchezaji wake. Ajib ni bonge la mchezaji hakuna anayekataa katika hilo lakini bado hajakamilika kufikia levo ya mchezaji wa kimataifa- tatizo lake pekee ni uvivu, kupoteza hovyo mpira mchezoni . ni jukumu lake kuisaidia timu ya Taifa lakini si lazima awepo kama hawezi kuibeba kwa moyop wa kujitolea na kujituma.

Maneno ya Zahera sikoni mwa Ajib si mapya, nilishamwambia, Ndalile alishamwambia, wadau walishamwambia, kama hayana maana kwake anaweza kuendelea kuweka ‘pamba masikioni’ mwake na kupiga pasi za mwisho na kufunga dhidi ya timu dhaifu tu na kukwama katika michezo mikubwa.

Sambaza....