Shirikisho Afrika

Mtibwa Sugar wawashukuru Watanzania.

Sambaza kwa marafiki....

Klabu ya soka ya Mtibwa Sugar imewashukuru watanzania waliojitokeza kwa wingi kwenye uwanja wa Azam Complex kuiunga mkono wakati wa mchezo wao wa shirikisho Afrika dhidi ya Northern Dynamo ya Ushelisheli.

Thobias Kifaru Ligalambwike ambaye ni Afisa habari wa Mtibwa Sugar amesema wameweza kufikia malengo na kupeperusha vyema bendera ya Taifa lakini Hilo limetokana zaidi na ubora wa kikosi chao na watanzania waliojitokeza kuwaunga mkono.

Amesema kwa sasa wanajiandaa kwa ajili ya mchezo ujao, ambapo wataendelea kuweka kambi Jijini Dar es Salaam hadi Jumapili ambapo ndipo watakapoondoka kwa ndege kuelekea Ushelisheli kukamilisha mchezo wa raundi ya pili.

“Ulikuwa ni mchezo mgumu, lakini hatimaye tumeweza kupata ushindi wa goli nne, ni ushindi mzuri kwetu kwenye michuano ya kimataifa, na tunarudiana Desemba 4, na tumesalia Jijini Dar kwa ajili ya matayarisho ya mchezo wetu, tunahitaji kuondoka hapa Disemba 2 kuelekea Ushelisheli kuwafuata wenzetu kwa ajili ya mchezo wa marudiano,”

“Na ninaamini kutokana na ubora wa kikosi chetu japokuwa wachezaji wengi ni wageni wa michuano ya kimataifa mfano jana tumepata nafasi nyingi lakini tumeshindwa kuzitumia, Mtibwa ni timu ya Watanzania, inajua maana ya bendera ya Taifa inawachezaji wote na benchi lote ni wa Tanzania kwa hiyo wanauchungu na bendera yao inavyopepea,” amesema.

Kwa ushindi ambao Mtibwa wameupata itawalazimu Northern Dynamo kushinda zaidi ya mabao 5-0 Ili kusonga mbele katika mchezo wa marudiano utakaofanyika nchini Ushelisheli.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.