Ligi Kuu

Pondamali ni ‘gwiji’ lakini asimkosee heshima Kindoki

Sambaza....

GOLIKIPA wa Yanga SC, Klaus Kindoki amemtupia lawama kocha wa magolikipa wa klabu yake, Juma Pondamali ambaye hivi karibuni alimponda kipa huyo raia wa Congo DR kwa kumuita ‘asiye na uwezo’

Pondamali alinukuliwa katika mahojiano na moja ya chombo cha habari nchini akiponda uwezo wa nyanda huyo na kwa jinsi alivyokuwa akimzungumzia ni wazi wawili hao hawatakuwa na mahusiano mazuri msimu ujao.

Pondamali (Kulia) akimfanyia mazoezi Ramadhani Kabwili wakati wa mechi ya Yanga vs KMC msimu wa 2018/19

Pondamali amekuwa kocha wa magolikipa wa Yanga kwa takribani miaka mitano sasa, na licha ya kwamba ni kocha mzuri lakini ubora wake unaweza kupimwa na uwezo wa magolikipa wa Yanga ambao walikuwa chini yake.

Deogratius Munishi ‘Dida’, Ally Mustapha ‘Barthez’, Youthe Rostand, Beno Kakolanya, na sasa Kindoki na Ramadhani Kabwili wote walipokuwa chini ya Pondamali walikuwa na makosa mengi.

Katika sehemu ya maelezo yake, Kindoki amesema kuna wakati msimu uliopita yeye na chipukizi Kabwili walipeleka malalamiko yao kwa kocha mkuu, Mwinyi Zahera na kumueleza kuhusu ubora mdogo wa kocha wao, Pondamali.

Kindoki, Kipa wa Yanga

Sitaki kuzungumzia kuhusu ubora ama ana faa au hafai lakini kikubwa ni kutaka kumkumbusha, Pondamali kuwa licha ya kwamba ni moja kati ya magolikipa bora wa muda wote kuwahi kutokea Tanzania kwa wakati wake anapaswa pia kuheshimu watu wengine.

Yeye ni mwalimu ambaye kimsingi pale wanafunzi wake wanapokosea hupaswa kuwarekebisha na si kuwasema vibaya ‘kwamba hawajui’ kazi yake ni kuisaidia Yanga kuwa imara katika goli, lakini maneno yake ni ukosefu wa hekima na busara.

Kindoki (Kushoto) akiwa na meneja wa tim, Hafidh

Nadhani Yanga wanapaswa pia kulitazama suala hili la kocha wao wa magolikipa kuwasema vibaya wachezaji katika vyombo vya habari. Pia uongozi wa klabu unapaswa kukaa na kocha mkuu, ZAhera na kumuuliza kuhusu uwezekano wa kuendelea au kutoendelea kufanya kazi na Pondamali kulingana na kiwango cha magolikipa wao ndani ya misimu miwili iliyopita ambacho kimekuwa cha wasiwasi mno.

Sawa, KIndoki ni ‘mbovu’ kama alivyosema Pondamali lakini ni jitihada gani alifanya ili kumsaidia kipa huyo kufikia ubora unaotakiwa kikosini mwao? Je, vipi kuhusu viwango vya Rostand? Kabwili? mbona nao vipo chini?

Licha ya ugwiji wake, Pondamali anapaswa kuwapa heshima wanafunzi wake na hata pale anapokuwa akikosea anapaswa kufanya hivyo kwa hekima na busara kwa sababu watu wengi wanamsikiliza na kumuheshimu pia.


Sambaza....
Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.