Sambaza....

NI kikosi gani na mbinu gani atatumia kocha wa Uganda ‘Cranes’ Mfaransa, Sebastien Desabre dhidi ya Tanzania ‘Taifa Stars’ iliyochini ya Mnigeria, Emmanuel Amunike katika mchezo wa kundi la tatu Jumamosi hii kufuzu CAN 2019 katika uwanja wa Namboole, Kampala hakika sifahamu, lakini nataraji kuona mchezo wa kasi kutoka kwa wenyeji.

Cranes wanaongoza kundi kufuatia kushinda 1-0 ugenini dhidi Visiwa vya Cape Verde, Juni 11 mwaka uliopita ugenini, wakati Stars ilibanwa nyumbani na Lesotho siku moja nyuma kwa sare ya kufungana 1-1 katika uwanja wa Azam Complex Chamanzi.

NAMBOLE STADIUM….

Ni uwanja wa kisasa unaouchukua watazamaji 60,000 katka jiji la Kampala. Timu ya kwanza kuondoka na furaha ndani uwanja huo ilikuwa Zambia, lakini licha ya kwamba walipata nafasi ya kufuzu kwa fainali za Afrika za mwaka 2013- Afrika Kusini, Chipolopolo ( walishinda kwa mikwaju ya penalty) walishindwa kuvunja rekodi ya Cranes ya kutopoteza mchezo kwa miaka kumi mfululizo katika uwanja huo.

Uwanja wa Namboole

Wakiwa na kikosi cha wachezaji 15 wanaotoka ng’ambo ya nchi yao, Desabre hawezi kuruhusu timu yake ibaki nyuma. Katika uwanja huu, Cranes hujiachia. Hushambulia kwa wakati maalamu na wanapofanya hivyo wanahakikisha wanapata goli. Mashabiki wa Uganda mara zote hushangilia kwa nguvu kikosi chao kinapocheza nyumbani na jambo hilo litawasumbua mno Stars na si rahisi kwao kupata matokeo, achilia mbali sare.

Sijui, Amunike atapangaje kikosi chake, lakini vyovyote atakavyopanga kuishinda Uganda ni jambo lisilowezekana katika ardhi yao kwa sababu wanajua umuhimu wa kucheza vizuri na kupata ushindi katika uwanja wa nyumbani. Wakiwa tayari wanaongoza kundi kwa alama tatu walizozipata Cape Verde huku Visiwa hivyo vya Maharibi mwa Afrika vikiwa uwanja kuwakabili Lesotho ugenini Jumamosi hii, Cranes lazima watalazima ushindi na Stars inapolazimishwa kurudi nyuma mambo huwa mabaya.

KUMILIKI MPIRA….

Ni nani ambaye anaweza kukaa na mpira walau kwa sekunde kumi tu katikati ya uwanja na kuupeleka sehemu sahihi? Uganda wanaweza kutembea na mpira vile wanavyotaka hata pale wanapopigwa presha umakini wao wanapoupata mpira huwa ni wa kiwango cha juu. Katika mchezo wa Stars 1-1 Lesotho Juni 10, mwaka jana kuna wakati viungo wa Stars walikuwa wakipiga pasi hovyo ambazo nyingi zilinaswa.

Wageni walifunga goli lililotokana na uzembe wa Abdi Banda na Salim Mbonde ambao walicheza kama mabeki pacha wa kati. Wawili hao walitorokwa kirahisi na mfungaji wa goli la kusawazisha la Lesotho kutokana na kutazama kule mpira unapotokea tu na si kufuatilia pia wapinzani wengine jinsi walivyojipanga.

Uganda Cranes wakiwa mazoezini

Stars wanapaswa kujitahidi kumiliki mpira hasa pale wanapotoka kushambuliwa, kupiga pasi kwa nguvu, kucheza na muda, umakini na kufuata maelekezo ya kocha kama wanahitaji kupata chochote katika mchezo huo ambao wenyeji wanaamini utawapaisha zaidi na kuwaacha Stars kwa alama tano baada ya michezo miwili tu kama watashinda.

KUJILINDA….

Si ujinga kuona kocha Fulani akitumia mbinu za kujilinda. Kuwapanga, Saimon Msuva, Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta kama washambuliaji watatu watakaoongoza mashambulizi dhidi Uganda itakuwa ni makosa kwa sababu timu itategemea viungo watatu tu katikati ya uwanja.

Labda inapaswa kuwa mechi ya kuanza kwa kujilinda zaidi na hapo ndipo kocha anapopaswa kumuanzisha Rashid Mandawa kama mshambulizi wa kwanza, Samatta akicheza kama namba kumi atakayezunguka eneo lote la mbele kulia na kushoto.

5-3-2 ungeweza kusaidia kwa sababu katika mfumo huu, Amunike anaweza kuwatumia mabeki watatu wa kati Banda, Aggrey Morris na Kelvin Yondan. Kuwazima Cranes inapaswa kujaza wachezaji wengi katikati ya uwanja lakini wale wenye uwezo wa kucheza vizuri. Himid Mao, Frank Domayo na Msuva wakicheza kati Stars itakuwa ngumu na wanaweza kupata kitu katika mchezo huo.

CRANES WATASHINDA….

Umakini mdogo katika kujilinda, uwezo mdogo wa kumiliki mpira katika presha, na mbinu za kujlinda zitaiangusha Stars na Uganda ni watu wasio na masihara wanapocheza nyumbani. Inawezekana kukawepo na mabadiliko makubwa katika uchezaji wa Stars –mchezaji mmoja mmoja lakini linapokuja suala la kucheza kitimu jambo hilo litawabeba Cranes.

Uganda hucheza vizuri na kitimu kuliko Stars. Pasi mkaa zisizofika huwa hatari unapokutana na timu makini na Uganda tayari wamepiga hatua nyingi mbele ya Stars kimbinu na kiufundi. Wanajua kucheza nyumbani na kulazimisha kupata matokeo. Kama ni shilingi, basi hii ya kwangu nitaiweka kwa Cranes. Wataendelea kujichimbia kileleni.

Sambaza....