Sambaza....

Hatunaye tena, yupo zake akiwa amekaa kwenye nyumba ya kibibi, kibibi kizee cha Turin. Miaka 9 aliitumia kujenga na kuweka alama ambazo zitakumbukwa na kila kizazi cha mpira wa miguu.

Kitabu chake cha historia RealMadrid kilianza kuandikwa kwa dau ambalo lilimtoa Manchester United kuja RealMadrid.

Dau ambalo lilimfanya kuwa mchezaji ghali kwa kipindi kile mwaka 2009.

Inawezekana namba tisa ilikuwa na maana kubwa sana katika maisha yake ya soka, alikuja RealMadrid mwaka 2009, na kupewa jezi namba 9 baada ya kumkuta mkongwe Raul Gonzales Blanco akiwa anavaa jezi namba 7.

Ilikuwa ngumu kwake yeye kupewa jezi namba 7 kwa sababu ya uwepo wa Raul Gonzales Blanco. Maisha yalianza katika timu ya RealMadrid.

Maisha ambayo yalimfanya aishi miaka 9 katika jiji la Madrid, hapa ndipo ukamilifu wa namba 9, namba ambayo ilitawala tangu ajiunge na kuondoka RealMadrid.

Hatuwezi kusema hii ndiyo namba muhimu kwake lakini ni namba yenye maana kubwa kwake katika maisha ya RealMadrid.

Umuhimu wa namba kwa Cristiano Ronaldo unabaki kwenye namba 7.

Namba ambayo aliivaa tangu akiwa Manchester United na baadaye RealMadrid.

Namba ambayo ilinfanya aweke alama nyingi na kubwa katika dunia hii ya michezo.

Na ndiyo namba ambayo aliivaa huku akibeba makombe manne (4) ya Ligi ya mabingwa barani ulaya, La Liga mara mbili (2) , Copa Del Lay (2).

Ndiyo jezi ambayo inaheshimika RealMadrid kwa sababu ikiwahi kuvaliwa na watu wazito.

Mgongo wa Emilio Butragueno uliivaa hii jezi ikawa nyepesi sana, mgongo wa Junaito ukafuata kuibeba jezi hii kabla ya Raul Gonzales Blanco kuweka alama akiwa na jezi hii.

Na mwisho wa siku mchezaji bora kuwahi kutokea duniani , Cristiano Ronaldo alikabidhiwa jezi hii na kuweka alama ambazo zimemfanya kuwa mchezaji wa kuheshimika duniani.

Wastani wa kufunga magoli 40 kila msimu ikiwemo msimu aliofunga magoli 61 ( msimu wa 2014-2015) kwa kifupi Ronaldo alimaliza maisha yake na RealMadrid akiwa na magoli 450 katika michezo 438.

Leo hii hayupo tena na RealMadrid, jezi yake ipo imetundikwa tu hakuna mtu aliyekabidhiwa kuivaa.

Swali kubwa ni nani ambaye anaweza kukabidhiwa jezi namba 7 baada ya Cristiano Ronaldo kuondoka?

Kichwa cha Julen Lopetequi kinawasha kumtafuta ni nani ambaye atafaa, ndiyo maana mpaka sasa hivi hajampa mtu yeyote jezi hiyo.

NANI ANAFAA ?

Kabla hatujaanza kumwangalia mmoja baada ya mwingine, kuna kitu ambacho unatakiwa kufahamu.

Kuvaa jezi namba 7 ya RealMadrid lazima uwe na sifa zifuatazo; kuibeba timu nyakati ngumu, kuwa na uwezo wa kufunga na kutoa pasi za mwisho, kuwa mchezaji ambaye ni nguzo ndani ya uwanja na nje ya uwanja.

Kuna makundi mawili ambayo tumeyainisha.

Kundi la kwanza ni la wachezaji waliopo kwenye kikosi cha RealMadrid na kundi la pili ni la wachezaji walio nje ya kikosi cha RealMadrid.

WACHEZAJI WALIOPO NDANI YA KIKOSI CHA REALMADRID.

MARCOS ASENSIO

Ni mmoja ya vijana ambao wanaonekana kuaminika na kubeba matumaini makubwa kwa watu wengi. Anatajwa kuwa mshindi wa Ballon D’or kwa siku zinazokuja.

Ameonesha dalili za kuibeba timu katika michezo mikubwa, anauwezo wa kufunga na kutoa pasi za mwisho za magoli pia.

ISCO.

Ndiye mchezaji ambaye anaonekana kama roho ya Julen Lopetequi.

Hakupewa nafasi kubwa sana katika kipindi cha Zinedine Zidane lakini chini ya Julen Lopetequi tangu wakiwa timu ya taifa amekuwa akipewa nafasi kubwa sana na katika kombe la dunia alikuwa mhimili wa Hispania.

Sifa kubwa inayombeba ni kuwa anaweza kucheza kwa ufasaha nafasi mbalimbali uwanjani. Mfano kiungo wa kati eneo la ushambuliaji, kucheza nyuma ya mshambuliaji wa mwisho na kucheza pembeni kushoto na kulia.

BALE.

Cristiano Ronaldo ameondoka, mpaka sasa hakuna aliyesajiliwa kwa ajili ya kuziba pengo lake. Mchezaji aliyebaki na anayeonekana ana ukomavu wa kuibeba timu kwenye michezo mikubwa, kufunga na kutoa pasi za mwisho za magoli ni Gareth Bale. Kwa sasa anavaa jezi namba 11 huyu anafaa pia kuvuliwa jezi namba 11 na kuvalishwa jezi namba 7.

WACHEZAJI WALIO NJE YA REALMADRID.

EDEN HAZARD.

Huyu anaonekana ana bei ya chini kuliko kina Mbappe na Neymar kwa sababu ya umri wake lakini kama akifanikiwa kuja RealMadrid ana nafasi kubwa ya kupewa jezi namba 7 kutokana na uwezo wake mkubwa.

MBAPPE.

Mchezaji bora chipukizi katika mashindano ya kombe la dunia. Mashindano ambayo yalimfanya afunge magoli 3 na alikuwa anapewa nafasi ya kushinda kuwa mchezaji bora wa mashindano.

Ndiye mchezaji ghali wa pili baada ya Neymar kwa sasa na anatajwa kuwa mshindi wa Ballon D’or kwa siku za hivi karibuni.

Ana kipaji kikubwa na umri wake ni mdogo , kitu ambacho kinawapa nafasi RealMadrid kumchukua.

NEYMAR

Bado ni biashara ambayo haijaisha, inasemekana imeandikwa kuwa ipo siku Neymar atavaa jezi ya RealMadrid.

Msimu huu kashindwa kwenda RealMadrid, tunachosubiri ni muda uje kutupa majibu sahihi ni lini anaweza akaja katika dimba la Santiago berbaneu na kuna uwezekano mkubwa kuwa jezi namba 7 inamsubiria kwa ajili ya kuibeba mgongoni mwake.

MWISHO.

Real Madrid wametangaza kumrudisha Mariano Diaz, na inasemekana kuna asilimia kadhaa ya mchezaji huyu kupewa jezi namba 7

Sambaza....