Wachezaji wa Simba wakishangilia na mashabiki wao
ASFC

Simba Kurudi Tena Jumanne.

Sambaza....

Baada ya kumaliza mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Afrika Klabu ya Simba ilitua Dar es salaam na kuwapa wachezaji wake mapumziko ya siku mbili ambapo wanapaswa kurejea kambini kesho Jumanne.

Simba wanaingia kambini ili kujiandaa na mchezo unaofuata wa Kombe la FA maarufu kama  Azamsports Federation Cup (ASFC) ambapo watakua na kibarua kigumu dhidi ya Mbogo Maji Ihefu Fc.

 

Mchezo huo unatarajiwa kupigwa siku ya Ijumaa Aprili saba mwaka huu katika Dimba la Uhuru majira ya saa kumi jioni. Mchezo huo wa robo fainali unategemewa kuwa mgumu na wakuvutia kutokana na kiwango kizuri walichonacho Mbogo maji hao katika Ligi.

Mara ya mwisho Simba kufanya vyema katika michuano hiyo ni msimu wa mwaka juzi ambapo walitwaa kombe hilo mbele ya watani zao Yanga katika fainali iliyopigwa mkoani Kigoma.

Tayari klabu ya Simba imeonyesha kuhitaji ushindi katika mchezo huo na kwa kuonyesha wanauchukulia kwa umuhimu mchezo huo wachezaji wote wanapaswa kuripoti kambini kesho jumanne ili kuanza kujifua kuelekea robo fainali hiyo.

Mshindi katika mchezo huo kati ya Simba na Ihefu atakutana na mshindi wa mechi kati ya Azam Fc dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza.

Tayari Singida Big Stars imeshakata tiketi ya nusu fainali baada ya kumshindilia Mbeya City kwa mabao manne kwa moja na sasa wanamsubiri mshindi kati ya Yanga ama Geita Gold.

Sambaza....