Stori

Kocha wa Simba Kuanza na Mtihani wa Manula

Sambaza....

Klabu ya Simba imemtambulisha kocha wake wa makipa Daniel Cadena ambae msimu uliopita aliitumikia Azam Fc kabla ya kuachana nae na kumpa “Thank you” mapema June hii.

Baada ya kutambulishwa rasmi leo na Simba baada ya kuachwa na Azam Fc Mwandishi wa habari nwandamizi Charles Abel Makia “Mzee wa ghafla” ametoa maoni yake akiandika hivi.

Ghafla tu, Daniel Cadena ameibukia katika kikosi cha Simba. Kocha huyo raia wa Hispania mwenye umri wa miaka 47, kabla ya kujiunga na Simba alikuwa kocha wa makipa wa Azam FC ambayo baada ya msimu kumalizika ilimpa “THANK YOU.” Kwa mtazamo wangu, mitihani mikubwa inayomkabili Cadena ndani ya Simba ni 4

Daniel Cadena (mbele) wakati akiitumikia Azam Fc.

● Kushughulika na mikono ya Ally Salim: Kwa mahitaji ya sasa, Ally Salim hatakiwi kutazamwa kama kipa mdogo tena. Kuwa benchi hakumaanishi awe anafanya makosa mepesi ambayo yanaweza kuigharimu timu kama ilivyotokea katika mechi za mwisho za msimu. Mikono yake inapaswa kuwa na uimara wa kukamata mpira (catching). Hii ni moja ya sifa za kipa mzuri na mwenye wajibu wa kumuimarisha ni Cadena.

● Kuongeza na kulinda ubora wa Aishi Manula na kipa mpya atakayesajiliwa: Sijawahi kumuona huyo kipa mpya wa Simba lakini naamini hadi kocha ameshauri asajiliwe basi atakuwa na ubora wake lakini kiwango cha Aishi kinafahamika. Kupanda na kuwa na mwendelezo wa grafu ya makipa hao kunapaswa kuwa deni la Cadena.

● Kuthibitisha wasifu wake: Kiwango cha makipa wa Azam chini ya Cadena hakikuwa kinachofurahisha. Hii iko wazi labda watu waamue kubisha tu. Inawezekana tatizo lilikuwa kwa Cadena mwenyewe au hao makipa. Ndani ya Simba, Cadena anapaswa kutuonyesha kuwa kilichopinda hakikuwa ni kivuli bali mti.

Daniel Cadena kocha mpya wa makipa Simba Sc.

● Kutengeneza uwiano mzuri wa ubora wa makipa wake: Timu kubwa haipaswi kuwa na wachezaji waliopishana sana ubora. Kunahitajika kuwepo namba moja, mbili au tatu kwa vile hawawezi kudaka wote kwa mchezo lakini viwango visiachane sana. Yaani haiwezekani makipa wote wawe na safari ya kwenda Mwanza kwa usafiri wa basi halafu mmoja yupo Tinde, mwingine Ikungi halafu anayewafuata mwishoni yupo Mikese.

Kama mmoja yupo Tinde basi angalau mwingine awe Nzega na mwingine Igunga.
Huo ni mtazamo wangu baada ya utambulisho wa Cadena

Sambaza....