Sambaza....

NAHODHA wa KMC FC, Juma Kaseja alishuhudia Yanga SC wakigongesha nguzo mara tatu wakati wa pambano lao la ligi kuu Tanzania Bara jana Alhamis katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mshindi huyo mara saba wa ligi kuu alishuhudia kiki ya mkwaju wa faulo ya kiungo Feisal Salum ‘ Fei Toto’ ikitinga katika nyavu zake na kuipa klabu yake ya zamani ushindi wa 0-1.

Feisal alifunga goli hilo dakika ya 90 baada ya mshambuliaji Matheo Anthony kuchezewa faulo nje kidogo ya eneo la hatari. “ Tulicheza vizuri kwa muda wote wa mchezo, lakini tulikuja kupoteza mchezo dakika za mwisho kutokana na umakini wetu mdogo.” Anasema mchezaji huyo aliyezichezea Simba SC na Yanga kwa vipindi viwili tofauti tofauti.

“ Nawapongeza Yanga, walicheza kitimu na walifanya mashambulizi mazuri . walistahili kushinda lakini hatukustahili kupoteza kwa stahili ile ya dakika za mwisho kabisa. Inaumiza lakini kuna wakati unapaswa kuangalia umepoteza mechi dhidi ya mpinzani wa aina gani. Tunatazama mbele, tutarekebisha makosa yaliyotuangusha .”

Sambaza....