Sambaza....

AKIWA amepoteza namba mbele ya Feisal Salum ‘Fei Toto’ kiungo mlinzi wa kati wa Yanga SC, Said Juma Makapu anataraji kuitumia michuano ya Mapinduzi Cup-Zanzibar iliyoanza Januari Mosi na ile ya SportPesa Super Cup inayotaraji kuanza Januari 17 kurejesha nafasi yake katika kikosi cha kwanza.

Yanga imepangwa kundi B katika Mapinduzi Cup na itashuka dimbani kwa mara ya kwanza Alhamis hii kuwavaa KVZ FC kisha watakamilisha michezo yao ya hatua ya makundi kwa kuzivaa Azam FC na Jamhuri FC ya Pemba.

” Msimu umekuwa mzuri kwetu kama timu, tunaongoza ligi kuu na tupo hapa Zanzibar kujaribu kushinda kikombe hiki cha Mapinduzi Cup.” anaanza kusema kiungo huyo wa timu ya Taifa ya Zanzibar nilipofanya naye mahojiano mafupi akiwa huko Visiwani.

” Ni kweli nimepoteza nafasi yangu katika kikosi cha kwanza lakini siku zote mwalimu Zahera ( Mwinyi) amekuwa karibu yangu na ananisaidia sana kama mchezaji. Nitatumia michuano hii kumshawishi mwalimu na kumuonyesha nipo tayari kurejea kikosi cha kwanza.” anasema Makapu ambaye msimu uliopita alitumika mara nyingi katika beki ya Kati.

” Kama unakosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na timu inasonga mbele inamaanisha wapo wachezaji wa kutosha na wenye ubora katika timu, hivyo kama mchezajj unalazimika kujituma na kuongeza juhudi zaidi ili kuendelea kuisaidia timu yako na ndicho ninachokifanya.”

Sambaza....