Beno
Ligi Kuu

Beno angefuata njia ya Kessy, si kuimaliza Yanga.

Sambaza kwa marafiki....

KWA misimu miwili ndani ya Yanga SC, golikipa Beno Kakolanya ameanza kikosi cha kwanza katika michezo isiyozidi 25 kati ya 73 ya ligi kuu Tanzania Bara, amecheza chini ya mechi tano kati ya 22 ambazo Yanga wamechezakatika michuano yaCaf ( Champions league + Confederations), na hajawahi hata mara moja kuichezea timu ya Taifa ya Tanzania.

Takwimu hizi haziondoi ukweli kwamba nyanda huyo wa zamani wa Tanzania Prisons ni kati ya magolikipa watano bora nchini ndani ya miaka hii nane ya karibuni. Beno ni kipa mwenye ubora, lakini kwa namna mambo yalivyo, Yanga wanapaswa kuachana nae mara baada ya kumalizika kwa msimu huu.

Ikumbukwe, Yanga walimsaini Beno katikati ya mwaka 2016 baada ya kuonyesha kiwango cha juu msimu wote wa 2015/16 akiwa mchezaji wa TP.

Msimu wake a kwanza ndani ya ´Timu ya Wananchi´ alikuwa msaidizi wa Deogratius Munishi ´Dida´ na msimu uliopita alikuwa chaguo la pili nyuma ya Youthe Rostand raia wa Cameroon.

Beno alianza kupewa nafasi na kuwa chaguo la kwanza katika mchezo wa nne wa hatua ya makundi katika Caf Confederations Cup Julai mwaka huu dhidi ya USM Alger baada ya Youthe kuendelea kufanya makosa makubwa katika michezo miwili ya Yanga vs Gor Mahia FC mwezi Juni katika michezo ya hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika.

Kiwango chake cha juu katika ´Dar es Salaam-Pacha´ dhidi ya mahasimu wao Simba SC kilimpaisha zaidi na naweza kuthubu kusema ndiye alisababisha suluhu-tasa katika mchezo wa mahasimu hao wa soka la Tanzania.

Ni ukweli ulio wazi kuwa Beno ni nyanda wa kiwango cha juu nchini, anastahili kuchezea klabu kubwa kama Yanga, lakini tangu January, 2017 golikipa huyo amekuwa akisusa-susa na mwanzo ilitajwa ni kwasababu klabu ilikuwa ikimzungusha kummalizia pesa zake za usajili.

Baadae ikasemekana alikuwa akigoma kucheza kwasababu ya kutolipwa mshahara. Nakumbuka wakati mkataba wake wa miaka miwili ulipokuwa ukielekea mwisho mapema mwaka huu, Beno alirejea kikosini na akasema alikuwa nje ya timu si kwa sababu za kimaslai bali ilitokana na majeraha yake ya goti.

Alisaini mkataba mpya Juni mwaka huu wakati akifahamu fika klabu inapitia wakati gani kiuchumi. Kama alihitaji kujiendeleza kimpira alikuwa sahihi kuongeza walau mwaka mmoja kubaki Yanga, lakini kama alikuwa kimaslai alipaswa kufuata njia ya Hassan Kessy- alipaswa kuondoka Yanga.

Kubaki kwake mahala ambako hakuwa na uhakika wa kupata mshahara ni makosa makubwa aliyafanya, na makosa yake hayo hapaswi kuyatumia kuwayumbisha wenzake walioamua kubaki katika sehemu yenye shida.

Beno ameshindwa kuichezea Yanga katika michezo mitatu mfululizo ya ligi kuu kutokana na kugoma kwake kujumuika na timu kwasababu hajalipwa mshahara kwa miezi inayosadikiwa mitano sasa. Yupo sahihi kudai haki yake ya msingi, lakini kwanini anadai akiwa nje ya kikosi? Anahujumu?

Kama si hujuma ni kwanini anajitenge katika wakati huu timu ikipambana katika ligi? Kwanini alipwe peke yake wakati wachezaji wote wanadai? Yeye akilipwa na wenzake wasilipwe unadhani katika hali ya kawaida ya ´kitimu´ wachezaji wataona upo usupastaa ambao unafanya wachache walipwe na wachache wasilipwe.

Ushauri wangt kwa Beno na Yanga ni huu. KamaBeno yupo kimpira arejee kikosini- tena kwa kuwaomba msamaha wachezaji wenzake na benchi la ufundi. Na kama yupo kimaslai awafuate, Obrey Chirwa, Vicent Bossou, Kessy na Yanga wamuache aende zake. Hastahili kulipwa pekee, bali wachezaji wote na wakufunzi wao Wanatakiwa kulipwa.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.