Aussems, kocha wa Simba
Blog

Mchezaji muhimu aliyebaki nje ya Taifa Stars ni akili za Patrick Aussems.

Sambaza....

Kuna mengi yanazungumzwa sana baada ya kikosi cha Taifa Stars , timu yetu ya Taifa kutajwa na kocha Emmanuel Amunike.

Mengi sana, lakini machache juu ya hayo mengi ni malalamiko ya kuachwa baadhi ya wachezaji ambao wanaonekana wanaweza kuisaidia timu yetu ya Taifa na kuitwa wachezaji ambao wanaonekana siyo wazuri ukilinganisha na walioachwa.

Hadithi nyingi zinamuongelea sana Ibrahim Ajib, mchezaji ambaye amepika magoli mengi kuzidi wote msimu huu kwenye ligi yetu pendwa.

Mchezaji ambaye amekuwa na umuhimu mkubwa sana kwenye kikosi cha Yanga kwenye upatikanaji wa magoli.

Ajib

Umuhimu ambao wanaulinganisha na umuhimu ambao unahitajika kwenye mechi yetu hii ya mwisho dhidi ya Uganda.

Tunahitaji kushinda tu!. Hiki ndicho ambacho tunatakiwa kukifanya na ndicho ambacho kinaonekana kama mahitaji yetu makubwa na ya msingi.

Unahitaji kushinda, je unafanyeje?. Lazima ushambulie, huwezi kushinda kwa kukaa muda mrefu ukiwa nyuma ya mpira.

Asilimia ya kushinda inakuwa ndogo sana. Na huwezi kuamua kushambulia bila kuwa na wachezaji ambao kwa asilimia kubwa wana sanaa ya kushambulia.

Kushambulia ni sanaa. Sanaa ambayo siyo kila mchezaji amebahatika kuwa nayo kwenye miguu yake.

Ni sanaa ambayo wachache sana wanayo. Na ndiyo ambao tunawahitaji sana kwenye mechi hii. Mechi ambayo tunahiyaji ushindi kuliko hadithi nyingine.

Ushawatazama viungo ambao wameitwa kwenye kikosi chetu cha timu ya Taifa?. Viungo ambao ni wapishi wa ushindi ambao tunauhitaji kwa kipindi hiki ?

Emmanuel Amunike, kocha wa Tanzania

Sitaki kuwahukumu moja kwa moja ila kiukweli wana asilimia kubwa ya sifa za kuzuia kuliko kushambulia. Na hiki kitu kipo kwenye moyo wa Emmanuel Amunike.

Mwalimu ambaye ni muumini mkubwa sana wa kanisa la mtakatifu kujizuia. Huwezi kumwambia kitu chochote akakuelewa kuhusu kutokujizuia.

Rangi yake ameionesha wazi kabisa kwenye mechi ambazo amesimama kama kocha mkuu wa timu ya Taifa.

Nilianza kumtazama kwenye mechi ya Uganda mpaka Nambole mjini Kampala. Aliingia na hiki kitu, kujizuia.

Sikutaka kumlaumu sana kwa sababu tulikuwa ugenini, lakini cha kushangaza hata mechi zote ambazo zilifuata baada ya hii mechi.

Mechi dhidi ya Cape Verde ugenini aliingia na wachezaji wengi wenye asili ya kujizuia sana na tukafungwa.

Mechi dhidi ya Lesotho aliingia na wachezaji pia ambao kwa a asilimia kubwa walikuwa na sifa ya kuzuia na tukafungwa.

Msimamo kundi L (Livescore.com)

Hata tulipokuja kucheza nyumbani dhidi ya CapeVerde, Emmanuel Amunike aliweka kikosi cha aina ile ile, yani chenye asilimia kubwa ya wachezaji ambao wanajilinda.

Mechi ya nyumbani, lakini akawa na hofu akaamua kuwa na wachezaji wengi wenye asili ya kujilinda. Hiki kitu ndicho kilinionesha dhehebu halisi la Emmanuel Amunike.

Huyu muumini mkubwa sana wa kujilinda huwezi kumtoa kwenye hili , anaamini kupitia hiki ndiyo maana akaja na wachezaji wengi wenye asili ya kujizuia kwenye kikosi chake.

Kikosi ambacho kinatakiwa kucheza mechi ambayo tunahitaji kufunga magoli yani kwa kifupi kwenye mechi ambayo tunahitaji kushinda!

Hapa ndipo ninapoanza kuwa tofauti na watu wengi, wengi wanalalamika baadhi ya wachezaji kutoitwa na Emmanuel Amunike.

Siwezi kumlaumu kabisa kwa sababu dini yake ni ya kujizuia. Lakini kitu ambacho nakiwaza tofauti na wengine ni timu yetu kukosa mtu mwenye akili ya Patrick Assumes.

Kocha mkuu wa klabu ya Simba. Kocha ambaye anaamini katika kushambulia iwe kwenye mechi ya ugenini au mechi ya nyumbani.

Aina hii ya mwanadamu ndiye ambaye tumemkosa kwenye kikosi chetu cha timu ya taifa. Mechi hii tunahitaji kushambulia.

Tunahitaji mtu wa kulisha mbegu za kushambulia kwenye kikosi chetu cha timu ya Taifa ili tuweze kufuzu kwenda Afcon.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x