Wachezaji wa Yanga wakiwa mazoezini
Stori

Muda Unakwenda Kasi kwa Wananchi

Sambaza....

Nimekumbuka jioni moja jua la kawaida Dar es Salaam, Yanga inaingia kwenye tetesi za kuwania saini ya beki wa kulia Mkongomani Djuma Shabani.

Ilikuwa ni jioni yenye faraja kwa wadau wa soka nchini, ubora na wasifu wake vilitosha kuzungumzwa sana mitandaoni, redioni, magazetini, vijiweni na katika runinga.

Ilikuwa ni fahari kwa timu ya Tanzania kuhusishwa na mchezaji mkubwa kama Djuma na mwisho ikawa fahari zaidi baada ya kusajiliwa Yanga.

Djuma Shabani akipiga penati katika mchezo dhidi ya Azam Fc..

Huenda mkawa mmesahau lakini nawakumbusha, wakati Djuma anatua Jangwani ndiye alikuwa Staa zaidi kwa wakati ule licha ya kuwepo sajili nyingine ikiwemo ya Mayele.

Muda ukasonga, Mayele akapindua meza na kuwa staa, ile kufunga mabao na kutetema ikawa habari ya mjini na Mayele akapanda thamani maradufu.

Wakati Mayele akiibamba nchi kwa kutetema, katikati ya dimba la Yanga alikuepo Mzee wa Kazi chafu, Yanick Bangala.

Yanick Bangala mchezaji bora kwa msimu wa 2021/2022.

Dimba la Yanga lilikuwa sehemu salama, Muda ukasonga na Bangala akaibuka mchezaji bora wa Ligi msimu wa 2021/2022. Alistahili.

Muda ukaendelea kuishi katika tabia yake, yule Djuma aliyesajiliwa akiwa staa, akaanza kukaa benchi, ghafla akaanza kusemwa amenenepa na sasa amekosa thamani ndani ya Yanga.

Hivyo hivyo kwa yule MVP wa msimu wa 2021/2022, ghafla akaanza kukalia mbao ndefu, huku na huku akapewa shutuma anauza mechi bila kusahau ile ya kugawa timu na sasa thamani yake inaonekana ndogo ndani ya Yanga.

Djuma Shaban na Yanick Bangala.

Kuna uwezekano mkubwa ikawa ndio mwisho wa Djuma na Bangala ndani ya Yanga, lakini pia kuna maisha nje ya Yanga.

Hakuna wa kulaumiwa, bali muda. Muda unafurahisha na Muda unahuzunisha. Hizo Ndio tabia za Muda.

NB: Huyu anaikataa laki, Yule anaifuata kwa bus.

Left Writter!

Sambaza....