Sambaza....

KOCHA mkuu wa Yanga SC ameulalamikia uongozi wa klabu yake kwa kushindwa kuwasaini wachezaji aliowahitaji katika usajili wa dirisha dogo uliofungwa Disemba 15. Zahera alihitaji golikipa mpya na pendekezo lake lilikuwa kipa wa Bandari FC ya Kenya, alihitaji kiungo mpya, Reuben Bomba raia wa DR Congo na kiungo mshambulizi, Charles Ilanfya.

Hessein Nyika ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo hawezi kukwepa lawama licha ya kwamba wamefanikiwa kumsaini kiungo mkongwe Haruna Moshi ‘Boban’ kutoka African Lyon. Jumatatu hii, Zahera alilalamika hadharani na kuhoji usajili wa golikipa Ibrahim Hamid ambaye Yanga imemsaini. Zahera amesema Hamid si chaguo lake na wala hajui jina lake na hajawahi kumuona akicheza.

NYIKA NI WA ASILIMIA KUMI?

Mara baada ya kukamilisha usajili wake wa kujiunga na KMC FC akitokea Mwadui FC, Ilanfya amesema alikuwa na shahuku kubwa ya kuichezea Yanga msimu huu lakini jambo hilo limeshindikana kutokana na Nyika kutoonyesha utayari.

Kiungo huyo mshambulizi wa zamani wa Mtibwa Sugar FC, amesema wala hakuhitaji kiasi cha Tsh. 25 milioni ambacho inadaiwa Nyika alifikisha kwa uongozi wa klabu. “ Nilihitaji milioni kumi tu si 25 kama inavyosema ili niichezee Yanga.” Amenukuliwa akisema, Ilanfya.

Kwa namna mchezaji huyo alivyosema huku kukiwa na kumbukumbu ya ‘sajili hewa’ kadhaa zilizowahi kufanywa na kamati ya Nyika kama ule wa Mcongo, Feston Kayembe ambaye licha ya kutangazwa na kutambulishwa kuwa alisaini mkataba wa miaka miwili na kuvuta Tsh. 20 milioni miezi 18 iliyopita mlinzi huyo hakuwahi kuichezea Yanga katika mchezo wowote rasmi na hadi sasa hakuna taarifa zake zozote.

Boban amejiunga na Yanga kwa mkataba wa miezi sita.

Inafahamika Yanga wamekuwa wakipitia miezi karibia 20 sasa ya uchumi mgumu klabuni mwao lakini kwa namna mambo ya usajili yanavyoendeshwa kuna uwezekano upo ‘ubadilifu’ unafanyika na baada ya maneno ya Ilanfya ninaanza kupata wasiwasi kama ni kweli Boban amesajiliwa kwa dau la Tsh.25 milioni linalotajwa tena kwa mkataba wa miezi sita tu!

Kushindwa kuwasaini wachezaji muhimu watatu waliohitajika na kocha Zahera na kumpa Boban Tsh. 25 milioni kwa mkataba wa miezi sita ni kosa kwa timu inayolalamika ukata kila siku na ni kuwavunja nguvu wanachama na mashabiki wanaojitolea kuichangia chochote klabu yao.

Kwanini Nyika alisema Ilanfya alihitaji Tsh. 25 wakati ukweli mchezaji huyo alihitaji milioni kumi tu? Ni wachezaji wangapi wamesainiwa Yanga chini ya Nyika na ni wangapi ‘hakupiga’ pesa kama alivyotaka kufanya kwa Charles?

Ni kweli Boban ana thamani ya Tsh.25 milioni kwa miezi sita tu? Nina wasiwasi na Nyika na kama ningekuwa mwenye mamlaka ningeunda kamati ya wachunguzi kumchunguza na kama ikibainika ni mpigaji haraka nampeleka mahakamani.

Sambaza....