Shirikisho Afrika

Wananchi Waondoka na Kikosi Kamili Wakiwa na Matumaini Kibao

Sambaza....

Wananchi Yanga tayari wameshaanza safari ya kwenda kuandika historia katika michuano ya  Shirikisho Afrika nchini Nigeria wakiondoka na wachezaji wao wote muhimu kuelekea mchezo huo dhidi ya Rivers United.

Yanga wameondoka alfajiri ya leo wakipitia Ethiopia na kuunganisha ndege mpaka nchini Nigeria wakitegemewa kufika majira ya saa sita na nusu mchana tayari kabisa kuvaana na wenyeji wa Rivers United katika dimba la Godswill Akpabio siku ya Jumapili April 23 saa kumi jioni.

Kuelekea mchezo huo Yanga imeondoka na kikosi chake chote cha wachezaji tegemeo huku wakiwaacha nchini nyota wake wachache kwasababu mbalimbali ikiwepo majeruhi na sababu za kiufundi.

Wachezaji wa Yanga Stephane Aziz Ki na Mudathir Yahya wakiwa safarini.

Wachezaji wa Yanga walioondoka nchini alfajiri ya leo ni, Walinda mlango: Metacha Mnata, Djigui Diara na Eric Johora, Walinzi: Ibrahim Bacca, Bakari Nondo, Dickson Job, Kibwana Shomary, Djuma Shaban, Mamadou Doumbia na Lomalisa Mutambala. Viungo: Farid Mussa, Zawad Mauya, Mudathir Yahya, Yanick Bangala, Khalid Aucho, Salum Aboubacar, Tuisila Kisinda na Jesus Moloko.  Washambuliaji: Fiston Mayele, Aziz Ki, Benard Morrison, Kenedy Musonda na Clement Mzize.

Kikosi cha Yanga kinawakosa Denis Nkane, Crispine Ngushi, David Bryson na Dickson Ambundo kwenye safari hiyo walioachwa kwasababu mbalimbali.

Yanga wanahitaji kupata matokeo mazuri wakiwa ugenini kama watashindwa kupata ushindi basi walau sare ama wakifungwa basi wapoteze mchezo kwa tofauti ndogo ya magoli kwani wana faidi ya kumalizia mchezo wa pili nyumbani hivyo ni rahisi kwao kupata matokeo.

Mara ya mwisho Yanga kukutana na Rivers walikubali kichapo cha bao moja bila katika mechi zote mbili za nyumbani na ugenini.

Tayari Yanga wameshajiapiza kwenda kulipa kisasi kwa Wanaijeria hao kwani ni msimu uliopita tuu walitolewa na Rivers United katika hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ni kama wana bahati kuelekea mchezo huo kwani wenyeji wao Rivers walikataliwa na CAF kutaka kurudi katika uwanja wao wa nyumbani ambao ulifungiwa ili kufanyiwa marekebisho na hivyo kandanda litapigwa uwanja wa  Godswill Akpabio katika Jimbo la Akwa Ibom Kusini mwa Nijeria.

Sambaza....