Wachezaji wa Simba Pape Sakho na Clatous Chama wakishangilia moja ya magoli yao katika mchezo dhidi ya Horoya.
Mabingwa Afrika

Simba: Tumeshajifunza Sasa Tunawafunga Wydad na Kandanda Safi Tutapiga

Sambaza....

Simba Sc itawakaribisha Wydad Casablanca katika mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa katika Dimba la Benjamin Mkapa kesho saa kumi jioni huku kocha mkuu wa klabu hiyo akiahidi soka safi.

Robert Oliveira amesema wanajua wanakwenda kucheza na timu nzuri na bora lakino wamejiandaa vyema kupata ushindi na kuwaburudisha mashabiki kwa soka safi. 

“Katika Ligi ya Mabingwa hakuna timu nyepesi, Wydad ni timu bora kama ilivyo Simba na nyinginezo. Tumefanya maandalizi mazuri na timu ipo tayari kwa mchezo.

Robertinho Oliveira kocha mkuu wa Simba akiongea na waandishi wa habari kuelekea mchezo dhidi ya Wydad Casablanca.

Tumewasisitiza wachezaji kucheza vizuri tukiwa na hatuna mpira kwa sababu itatusaidia kuwasoma wapinzani, tunahitaji kushinda pamona na kucheza vizuri,” amesema Robertinho.

Nae mlinzi wa kulia wa Simba Shomary Kapombe amesema wameshacheza sana robo fainali na sasa ni wakati wa kuonyesha wao ni bora na kuvuka kwenda nusu fainali. Mlinzi huyo pia aliongeza wameshapa funzo kutoka kwa Raja Casablanca na sasa mchezo huu wataumalizia nyumbani.

“Tumejiandaa vizuri, tunataka kuwaonyesha Watanzania kuwa tunaweza na tupo tayari. Tumekuwa tukitolewa katika hatua hii lakini sasa tupo tayari kuwaonyesha Watanzania na Wanasimba kuwa tunaweza.

Shomary Kapombe.

Tulipoteza nyumbani dhidi ya Raja Casablanca lakini tumekuja na mbinu mpya ambazo tunaamini zitatusaidia. Tunataka kutumia uwanja wa nyumbani kumaliza mechi kwa kuwa tunadhani kule Morocco itakuwa ngumu kwetu,” alisema Kapombe.

Simba wanakwenda kesho kuingia katika Dimba la Benjamin Mkapa wakijua ushindi mnene ndio utakaowavusha na kwenda nusu fainali kwani mchezo wa pili ugenini utakua mgumu kwao kutokana na jinsi timu za Kiarabu zinavyocheza zikiwa nyumbani.

Simba kesho itaendelea kumkosa Aishi Manula kutokana na majeraha wakati kwa upande wa Sadio Kanoute “Putin” yeye amepona na ameonekana akifanya mazoezi na wenzake katika mazoezi ya mwisho ya Simba yaliyofanyika leo katika uwanja wa Benjamin Mkapa.

Sambaza....