Sambaza....

Usajili wake wala haukuwashtua wengi, haitoshi, mchezo wake wa kwanza akiwa na jezi za Yanga SC alijifunga na kusababisha penati Agosti, 2017.

Hakuwa na uwezo wa mkubwa katika kumiliki mpira, kuanzisha mashambulizi na hakuwa mtulivu.

Baada ya kujifunga katika game hiyo iliyikuwa ya kirafiki dhidi ya Singida United niliandika mahala na kusena, Abdallah Hajji ‘Ninja’ anaweza kuwa Nadir Haroub mpya katika kikosi cha Yanga kama atavumiliwa na kupewa muda zaidi.

Nikitolea mfano wa namna Nadir alivyokuwa wakati akijiunga na Yanga mwishoni mwa mwaka 2005 akitokea Zanzibar Ocean View. Nadir alikuwa akicheza mchezo wa kubutua zaidi mpira, huku akionekana asiye na uwezo mkubwa katika umiliki wa mpira.

Baadae nahodha huyo mstaafu wa timu za Taifa za Zanzibar Zanzibar Heroes’, Taifa Stars na Yanga si tu alikuwa kiongozi wa mfano bali alijikuza haraka kiuchezaji na kuwa beki bora katika soka la Tanzania kwa miaka zaidi ya kumi.

ABDALLAH NINJA

Licha ya kufunga magoli mawili katika michezo mitatu iliyopita ya Yanga katika ligi kuu Tanzania bara, Ninja ni mchezaji bora zaidi katika ngome ya kocha Mcongo, Zahera Mwinyi.

Tangu alipochukua nafasi ya nahodha Kelvin Yondan katika michezo miwili ya Yanga huko Kanda ya Ziwa mwezi uliopita beki huyo wa kati ameendelea kupandisha kiwango chake kila kukicha.

Amekuwa mzuri na pengine bora kuliko walinzi wote katika ligi kuu katika uchezaji wa tackling. Wakati walinzi wengi wa kisasa wakiogopa kucheza tackle kutokana na hofu ya kusababisha mikwaju ya penalti, Ninja amekuwa akifanya hivyo kwa umakini mkubwa.

Tackle zake mara zote hufanikiwa kwa asilimia 90 kwa sababu huwa hachezi faulo dhidi ya mchezaji wa timu pinzani. Ukiachana na uwezo wake wa kucheza tackle, Ninja ameendelea kukua kimpira hasa katika eneo la kusoma ‘nyendi’ za washambuliaji wa timu pinzani.

Inafurahisha sana kuona mlinzi ambaye hakuwa na uwezo wa kumiliki mpira walau kwa sekunde kumi miezi 16 iliyopita Leo hii akiongoza ngome ya timu inayoongoza ligi kwa tofauti ya alama nane.

Kuitwa kisha kupewa nafasi ya unahodha katika timu ya Taifa ya U23 mwezi uliopita kumemsaidia zaidi beki huyo wa kati katika suala la utulivu.

Kitu pekee ambacho Ninja anapaswa kukitilia mkazo katika uchezaji wake ni utulivu. Ana hanasa, nguvu na moyo wa ushindi. Rejea goli lake vs Biashara United FC wiki iliyopita, Yanga wakiwa nyuma 1-0 huku mchezo ukiwa umesalia robo saa kumalizika, Ninja alipandusha timu na baadae akamalizia pasi ya Amis Tambwe na kuisawazishia timu yake ambayo ilishinda 2-1.

Jana Alhamis matokeo yakiwa African Lyon 0-0 mlinzi huyo wa kati alipanda wakati Ibrahim Ajib alipokwenda kupiga mpira uliokufa na aliweza kuifungia timu yake goli pekee la ushindi katika mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa Sheikh Amr Abeid, Arusha.

Kwa hakika kijana huyu aliyesajiliwa kutoka Jang’ombe Boys ya Zanzibar Juni, 2017 amepiga hatua nyingi mbele katika mchezo wake na pole pole anaanza kupenya kuingia katika kundi la mabeki bora nchini.

Alipofungisha vs Singida United katika mchezo wa kirafiki mwaka jana alizomewa hadi na mashabiki wa klabu yake ya Yanga lakini kwa maendeleo yake kiuchezaji hivi sasa, Ninja hastahili tu makofi ya kupongezwa, bali heshjima. Niliona kipaji chake tangu wakati ule na niliamini atafunga midomo mibaya na tutamwongelea kwa heshima.

Sambaza....