Mashabiki wa Stars
Blog

Man of the Match alikuwa “SHABIKI”

Sambaza....

Furaha kubwa ndicho kitu ambacho kinachoweza kuelezea taswira halisi ya nyuso za Watanzania wengi.

Yanazungumzwa mengi sana. Mengi haya yalianza kuzungumzwa kabla ya hii mechi. Yani kipindi kile ambacho kikosi kimechaguliwa tu.

Unakumbuka ambavyo wengi walikuwa hawana imani na kikosi hiki ? Yani ilifikia hatua kila mtu akawa na kikosi chake.

Huyu alimtaka huyu, yule akamtaka huyu na yule tena akamkataa huyu ili mradi tu kila mmoja aonekane sahihi na kocha asiwe sahihi.

Hiki ndicho kitu ambacho kilikuwa kama mtihani wa kwanza kwa kocha Emmanuel Amunike kwenye hii mechi dhidi ya Uganda.

Ungewezaje kuishi ndani ya jamii ambayo kwa asilimia kubwa imekataa mawazo yako ?. Yani kwa asilimia kubwa unapigwa kwa unachokifanya ?

Hii ni hatua ngumu sana kwenye maisha ya mwanadamu lakini ndiyo hatua sahihi ambayo inaweza kumpeleka mwanadamu kwenye mafanikio.

Yes, Emmanuel Amunike amefika kwenye mafanikio. Mafanikio ambayo tumeyapigania kwa siku nyingi sana bila kufanikiwa.

Miaka 39 jasho letu limetiririka sana bila kufanikiwa. Lakini leo hii mwanaume kutoka Nigeria ametuwezesha kwenda Misri.

Mwanaume ambaye alicheza kwenye uwanja ambao wengi wa wachezaji wanatamani kuukanyaga, lakini yeye alifanikiwa kukanyaga nyasi za uwanja huo wa Nou Camp.

Alikanyaga kama mchezaji , mchezaji ambaye alivaa jezi ya Barcelona. Jezi ngumu sana kuvalika na siyo rahisi kwa mchezaji kuivaa. Lakini yeye alifanikiwa.

Mwanaume ambaye alifanikiwa kucheza timu ya Taifa ya Nigeria. Ile Nigeria ya Moto, achana na Nigeria hii ya kina Alex Iwobi.

Achana kabisa na hii ila yeye alicheza ile Nigeria ya Sunday Oliseh, Victor Ikpeba, Jay Jay Okocha, Taribo West, Hassan Chukwu, Peter Shorumu.

Samatta akiwashukuru mashabiki

Jana alikuwa amekaa kwenye benchi la ufundi akituongoza katika harakati za kukata kiu iliyodumu ndani ya miaka 39.

Tuliikata, hapana shaka huwezi acha kumsifia Emmanuel Amunike. Huyu ndiye kocha Jemedari ambaye alikuwa anaongoza jeshi letu.

Unaweza ukamsifia Emmanuel Amunike, ukachagua kumsifia mwingine utakayemuona anastahili kabisa kusifiwa.

Ukamsifia Simon Msuva kwa sababu ya kufunga magoli mawili muhimu ambayo yalitupeleka Misri kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39.

Unaweza pia ukachagua tena kumsifia John Bocco kwa pasi mbili za mwisho alizozitoa na kuzaa magoli mawili.

Au unaweza kuchagua kumsifia Mbwana Ally Samatta kwa kuwa nahodha imara dimbani. Kwa uwezo wake binafsi uliosababisha penati aliyofunga Erasto Nyoni.

Au unaweza kumsifia Erasto Nyoni mwenyewe kwa kufunga goli na kuhakikisha eneo la katikati mwa uwanja liko imara.

Uliwaona kina Aggrey Morris na Kelvin Yondani walivyosimama imara eneo la beki wa katikati ?. Hawa hawastahili sifa ? Hapana shaka wanastahili sifa kubwa sana.

Tena sana, kila mchezaji Jana alicheza kadri ya uwezo wake ili kutimiza tu jukumu kubwa ambalo Taifa zima lilikuwa linalitazama.

Kwa kifupi unaweza kuchagua mchezaji yeyote ndani ya uwanja kama mchezaji wako bora wa mechi kwa mechi ya Jana.

Lakini jana kuna mchezaji ambaye alitupa ushindi kabla hata mechi haijaanza. Huyu ni mchezaji wa kumi na mbili.

Yani shabiki. Shabiki ambaye alikuwa ameujaza uwanja. Hakukuwepo na nafasi yoyote ndani ya uwanja kwenye mechi ya Jana.

Mashabiki wa Stars

Hata nje ya uwanja kulikuwa na mashabiki wengi sana ambao walikuwa wanahitaji kuingia ndani ya uwanja lakini nafasi ndani ya uwanja haikuwepo.

Huyu ndiye aliyewasababisha Uganda waone wanafungwa kwenye ile mechi. Uganda walikuwa wanyonge sana tangu mwanzoni.

Wakati wanaingia kufanya mazoezi ya kupasha misuli unyonge wao ulikuwa unaonekana kwenye nyuso zao.

Hata wakati ambao wanaingia uwanjani kwa ajili ya kuchza mechi yenyewe walikuwa wanyonge sana kwenye nyuso zao.

Na hii ni kwa sababu moja tu iliyopelekea unyonge wao huo, shabiki. Shabiki ambaye alikuwa ameujaza uwanja.

Uwanja ulikuwa umetapika mpaka ulikuwa unatia uoga. Kila jicho la wachezaji wa Uganda lilivyokuwa linatazama juu lilikuwa linaingiwa na hofu na uoga.

Hii ilikuwa tofauti sana na kwa upande wa wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania. Kila wakati ambao wachezaji walivyokuwa wanatazama kwenye jukwaa kuna kitu kilikuwa kinawajaza ujasiri ndani yao.

Mashabiki wa Stars

Kitu chenyewe ni deni. Wachezaji walikuwa wanaona kabisa walikuwa na deni kubwa ambalo walikuwa wanadaiwa na mashabiki wa Tanzania.

Mashabiki ambao waliacha kazi zao na kuja kuwapa moyo. Mashabiki ambao walikuja kuonesha kuwa wako pamoja kwenye hili suala.

Ndiyo maana mwisho wa siku wachezaji wetu walipata nguvu ya kupigana kwa sababu ya mashabiki ambao walikuwa jukwaani, na Uganda walikuwa wameingiwa na hofu.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x