Kiungo wa Azam Fc Sospeter Banyana
Stori

Ni kweli Ligi Kuu Bara Inakua kwa Kasi?

Sambaza....

Mchezo wa soka ni moja kati ya shughuli inayojaza watu wengi katika viwanja mbalimbali vya mpira. Hasa timu hasimu Yanga na Simba zichezapo, zote zikitokea jiji la kibiashara la Dar es Salaam.

Kwa miaka ya hivi karibuni ligu kuu Tanzania bara ya mchezo wa soka wa wanaume imeonekana kukuwa. Na ikitoka katika tarakimu mbili kwa ubora na kuingia katika tarakimu moja.

Taarifa ya Shirikisho la kimataifa la historia na takwimu za mpira wa miguu (IFFHS), iliitangaza ligi hiyo kuwa ya tano kwa ubora barani Afrika mwaka 2022. Ikiwa imepanda kutoka nafasi ya 10 Afrika.

Kimataifa ilipanda kutoka nafasi ya 62 hadi 39. Kwa Afrka iko nyuma ya ligi ya Misri, Algeria, Morocco na Sudan. Kwa kuzingatia takwimu hizi hii itakwa ni ligu bora Afrika Mashariki.

Orodha ya Ligi 10 bora Afrika.

Udhamini Mnono!

Wiki hii Rais Mstaafu wa Tanzania Jakaya Kikwete amezungumzia suala la wachezaji wa kigeni kutawala soka la Tanzania na kuishauri Serikali kukaa na TFF, Shirikisho la Soka Tanzania, kuja na mkakati wa kuzalisha wachezaji bora wazawa.

‘Katika wale wanaosifiwa wachezaji wa Tanzania hawamo. Kwa sasa ukiuliza mchezaji gani maarufu Simba utasikia Baleke, utasikia kacheza mechi sita tu, Yanga kule utasikia Mayele sasa wakiondoka?’

Hofu ya mstaafu Kikwete ni juu ya wachezaji wazawa. Ila wingi wa wachezaji wa kigeni ni dalili ya uwekezaji wa kununua wachezaji kutoka nje umekuwa. Inaeleweka wachezaji wapya – wageni ni ghali zaidi.

Kupitia mtandao wake kampuni ya Sportpesa, iliandika Novemba 2021, ‘wakati SportPesa inatimiza miaka minne ya kuzaliwa hapa nchini, tayari udhamini wake wa miaka minne wa kumwaga kitita cha zaidi ya Sh. bilioni moja kwa kila mwaka, ndio unaoshikilia rekodi ya kuwa udhamini mkubwa zaidi katika historia ya Yanga.”

Sabrina Msuya meneja mahusiano wa Sportpesa.

Udhamini na uwekezaji unaonekana pia kukuwa katika timu nyingine za ligi kuu ya Tanzania bara. Hivi karibuni timu ya Simba ilisaini mkataba wa bilioni mbili kila mwaka wa utengenezaji na usambazaji wa jezi na kampuni ya Sandaland. Ikiwa ni mara mbili ya kitita cha mkataba na kampuni ya awali.

Wingi wa Mashabiki.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makaazi ya 2022, Dar es Salaam inashika nafasi ya kwanza miongoni mwa mikoa ya Tanzania kwa kuwa na watu wengi – milioni 5,383,728. Barani Afrika pia, jiji hili lipo katika orodha ya majiji kumi yenye watu wengi.

Sehemu kubwa ya mashabiki wa vilabu vikubwa wapo Dar es Salaam. Na timu kubwa za ligi hiyo zipo katika mkoa huo huo. Timu ya Simba na Yanga zinaongoza kwa kuwa na mashabiki wengi wa soka.

Wingi wa mashabiki sio muhimu tu kushabikia kwa kelele. Vilevile, wana umuhimu kwenye kuingiza mapato ya timu. Uuzaji wa tiketi ni eneo moja. Ununuzi wa wa vifaa vya timu kama jezi ni eneo jingine la mapato. Kampuni za kibiashara zinazotaka kuwa wafadhili wa timu huzingatia wingi wa mashabiki ili kuwekeza.

‘Ukizungumzia ushabiki wa hapa (Tanzania), na wa pale nyumbani Kenya, mashabiki hapa wana shauku na wanakwenda uwanjani, wanajaza uwanja na wanaunga mkono wachezaji na timu,” Francis Kahata, mchezaji wa soka kutokea Kenya akizungumza na Azam Tv.

Francis Nyambura Kahata.

Soka Mubashara
Mchambuzi wa soka na msemaji wa zamani wa timu ya Simba, Ezekiel Kamwaga anasema, ligi kuu ya Tanzania bara ina bahati ya kuwa moja kati ya ligi chache barani Afrika zinazooneshwa mubashara katika runinga.

‘Kuna uwekezaji mkubwa umefanyika katika televisheni. Kiasi ambacho watu wanatazama timu zao zinapocheza. Ingekuwa hatuioni Liverpool au Manchester City ikicheza, hizo timu zisingekuwa na mashabiki Afrika wala ligi yao isingekuwa maarufu,’ anasema Kamwaga.

Ukuwaji wa teknolojia inasaidia pakubwa uwekezaji wa aina hii kuzidi kurahisishika. Ligi inapooneshwa mubashara huchochea kuifanya iwe maarufu, izidi kuwa na mashbiki na kutambulika nje ya mipaka ya nchi.

Mashabiki wa klabu za Simba na Yanga wakishuhudia “Dabi”

Kuvuma Afrika
Mwaka huu Yanga imefanikiwa kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika. Pamoja na kwamba imekosa ubingwa lakini imeshika nafasi ya pili katika ligi kubwa Afrika baada ya ile Ligi ya Mabingwa.

Mafanikio ya namna hii husaidi kutangaza soka la Tanzania katika bara zima la Afrika. Kwa upande mwingine, nayo timu ya Simba hufanya kazi kubwa kulitangaza soka la Tanzania barani Afrika, kupita ushiriki wake wa Ligi ya Mabingwa.

Time zinapovuma na kusikika Afrika nzima, zinaongeza thamani ya ligi ya ndani. Ndiposa, haishangazi kuiona ligi hiyo ikishika nafasi ya tano kutoka nafasi ya kumi barani Afrika.

Nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto akivaa medali ya mshindi wa pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Changamoto.

Kuna changamoto ya ligi hii kutozalisha wachezaji wengi wanaocheza katika ligi kubwa duniani hasa zile za bara Ulaya.

Mafanikio ya timu za mataifa ya nchi za Afrika Kaskazini na Afrika Magharibi kuingia kwa wingi katika kombe la dunia, au kuchuana wao kwa wao katika kombe la Afrika, kunachangiwa pakubwa na wingi wa wachezaji wazoefu wanaocheza vilabu vikubwa Ulaya.

Uzoefu wa wachezaji hawa ndio huzifanya timu zao za taifa kuwaka katika makombe makubwa ulimwenguni. Fainali ya Kombe la Afrika ilizikutanisha Egypt ya Afrika Kaskazini na Senegal ya Afrika Magharibi. Wakiongozwa na wachezaji wao Mohamed Salah na Sadio Mané.

Vicent Aboubacar [Jezi namba 10] akifunga bao mbele ya walinzi wa Brazil katika mchezo wa kombe la Dunia

Ukilitazama kombe la dunia la Qatar 2022. Afrika iliwakilishwa na nchi tano, tatu za Afrika ya Magharibi – Cameroon, Senegal na Ghana na mbili za Afrika ya Kaskazini – Morocco na Tunisia. Zote zikiwa na wachezaji wenye majina makubwa ulimwenguni.

Hili ni eneo ambalo timu za ndani zikifanikiwa kupeleka wachezaji wengi nje. Kutaongeza mara mbili thamani ya ligi na kunufaisha pakubwa timu ya Taifa kwa kuwa na wachezaji vinara na wazoefu.

Chanzo: BBC


Sambaza....