Sambaza....

Tanzania ilikuwa mgeni wa Uganda ambayo imekuwa na matokeo mazuri nyumbani kwao.

Ulikuwa mtihani mgumu sana wa kwanza kwa Emmanuel Amunike, lakini kwa kiasi kikubwa anastahili pongezi.

Kipi alichokionesha katika mechi yake ya kwanza ya ugenini ?

Kwanza mfumo wake ulikuwa tofauti na mfumo ambao wengi tulikuwa tunautegemea ambao aliamua kuanza na mfumo wa 3-4-3.

Kipi kilifanikiwa ndani ya huu mfumo ?

Utulivu na umakini wakati timu ilipokuwa inashambuliwa ndicho kitu kikubwa ambacho Taifa Stars ya Emmanuel Amunike ilionesha.

Kipi kilikuwa kinakosekana ?

Hakukuwepo na kiungo wa kati ambaye ni mbunifu, viungo wawili wa kati ambao walianzishwa walikuwa na asili ya kuzuia ( Frank Domayo na Mudathir Yahaya) na hii ni kwa sababu Emmanuel Amunike alipanga kuzuia katika mchezo huu na kushambulia kupitia pembeni.

Washambuliaji watatu walioanza katika mechi ya leo walikosa utulivu kwenye nafasi ambazo walizokuwa wanazipata.

Kulikuwa na ulazima wa washambuliaji watatu wa Taifa Stars kwa leo kucheza muda wote ?

Thomas Ulimwengu hakutakiwa kumaliza mechi hii kwa sababu dakika 15 za mwishoni zilihitaji mshambuliaji ambaye anaweza kukaa karibu na lango kutokana na mashambulizi ambayo Taifa Stars waliyokuwa wanayapata.

Lakini kuna muda Thomas Ulimwengu alikuwa anahama eneo lile, kama angekuwepo mchezaji ambaye ana uwezo wa kukaa eneo lile kama Shaban Chilunda kulikuwa na asilimia kubwa ya mechi hii kumalizika kwa ushindi wa Amunike.

Je alifanikiwa kwenye lengo la kujizuia?

Kwa asilimia kubwa Emmanuel Amunike alifanikiwa hapa. Kitu pekee ambacho kilichokuwa kinakosekana kwa mabeki watatu wa kati ( Abdi Banda, David Mwantika na Agrey Morris ) ni uwezo mdogo wa kumiliki mpira.

Unapokuwa unacheza na mabeki watatu, unatakiwa uwe na mabeki watatu wa nyuma wenye uwezo wa kumiliki mpira.

Kuna mwanga wowote chini ya Emmanuel Amunike?

Tumecheza na timu ambayo kwa mechi nane zilizopita imeshinda mechi moja tu, ni timu ambayo kwa hivi karibuni imekuwa ikihangaika kupata matokeo. Hivo bado tuna muda wa kumpa kutuonesha kuwa anaweza kutufikisha sehemu ambayo Mara nyingi huwa tunaota kufika.

Sambaza....