Sambaza....

Chama alifunga ‘goli la video’ dakika ya 90′ na kuipa Simba SC ushindi muhimu uliowapeleka hatua ya makundi Ligi ya mabingwa Afruka kwa mara ya pili kihistoria na ya kwanza baada ya kupita ‘muongo’ mmoja na nusu.

Ushindi wa 3-1 ambao ‘Wekundu wa Msimbazi’ wameupata jioni hii katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Nkana FC ya Zambia umeipeleka mabingwa hao watetezi wa Tanzania Bara hatua ya 16 bora kwa ushindi wa jumla 4-3 kufuatia awali kupoteza 2-1 mjini Kitwe, Zambia mbele ya ‘Mashetani Wekundu’ hao ambao sasa wameangukia katika michuano ya Confederation Cup.

AUSSEMS

Licha ya ushindi jioni ya Leo kocha Mbelgiji anapaswa kusahau shangilia yake baada ya ‘goli lisilotarajiwa’ na yeyote kutoka kwa Chama dakika ya mwisho kabla mwamuzi wa akiba kuinua ubao kuonyesha dakika tatu za nyongeza.

Kuumia kwa mashambulizi na mfungaji wa goli la pili Mnyarwanda, Meddie Kagere ndani ya robo saa ya kwanza baada ya kuanza kipindi cha pili kulitoa nafasi kwa Hassan Dilunga. Licha ya kufanya makosa katika upangaji wa kikosi, Aussems pia alikosea kumuwaisha Dilunga na kuendelea kumuacha nje Said Ndemla.

Kumuacha nje ya kikosi kilichoanza mchezo beki Mganda, Jjuuko Murshid kulichangia Nkana kutangulia kufunga dakika ya 16′ tu ya mchezo kutokana na walinzi wa kati wa Simba, Muivory Coast, Paschal Wawa na Erasto Nyoni ‘kukabia macho’ wakati Walter Bwalya akifunga.

Karma,Aussems asingeshtuka na kumpa nafasi beki huyo wa timu ya Taifa ya Uganda na mashambulizi aliyozuia ndani ya dakika 30′ alizokuwa uwanjani Red Devils wangefunga tena.

Kuingia kwa Jjuuko kuchukua nafasi ya Mghana, Nicholas Gyan kukimaanisha Nyoni angesogea pembeni upande wa beki namba mbili na Wawa kucheza na Jjuuko katika beki ya kati na Mohamed Hussein ‘Zimbwe JR’ katika beki tatu. Hivi ndivyo Aussems alipaswa kuanza mchezo, na si kama alivyofanya.

Kumuacha nje Jjuuko kwa saa nzima ilikuwa kosa la kwanza kufanywa na Aussems na lilimgharimu kwa dakika 89′ na kuwapanga kwa mara nyingine kwa wakati mmoja, Mganda, Emmanuel Okwi, Kagere na nahodha John Bocco lilikuwa kosa lake la pili, shukrani lilifunikwa na goli la Chama ambalo lilimfanya ashangilie kwa nguvu na hisia kali.

Nkana FC kuna wakati kati ya dakika 75-83 walitawala sana kiungo na Jonas Mkude mfungaji wa goli la kuwasazisha la Simba dakika ya 29′ na patna wake Mghana, James Kotei katu hawatamsahau mpishi wa goli pekee la Wazambia hao, Harrison Chisala ambaye alitawanya mipira kila pembe ya uwanja kwa pasi zake za kushambulia.

Kuhaha kwa kiungo cha Simba mbele ya watazamaji wao zaidi ya 50,000 katika uwanja wa Taifa ni ishara kuwa Aussems anapaswa kubadilisha haraka mbinu zake vinginevyo watakuwa ‘Jamvi la Wageni,’ huko katika makundi.

CHA KUFANYA

Kwanza ni kumjenga zaidi Jjuuko ili awe mchezajj asiyekosekana kikosini. Pili, kutowaanzisha kwa wakati mmoja Okwi, Kagere na Bocco kwa sababu wote watatu si wakabaji na uwepo wao kwa pamoja ni mzigo mzito kwa viungo.

Tatu, Zimbwe Jr aneteswa sana na mlinzi wa kulia wa Nkana, Hassan Kessy kwa dakika zote 180 na Kelvin Kampamba amemuonyesha Aussems namna mlinzi wake huyo wa kushoto anavyopitika kiurahisi.

Kiwango cha Mghana, Asante Kwassi Jumatano hii wakati Simba iliposhinda 2-1 dhidi ya KMC fC katika ligi kuu na kile alichokionyesha msimu uluopita ni wazi Mghana huyo anapaswa kuanza mbele ya Zimbwe Jr katika beki Tatu.

Huu si tena wakati wa Aussems kushangilia goli la muijiza ya Chama, ili asiwe jamvi la wageni katika hatua ya makundi afanye jitihada kama kocha kupandisha viwango vya Jjuuko na Kwassi kama anaona hawajakidhi mahitaji yake. Hao ni wachezaji muhimu mno katika ngome yake akiamua wawe.

Sambaza....