BlogMabingwa Afrika

Kwa kutumia kanuni hii, Simba haoo robo fainali Klabu Bingwa Afrika.

Sambaza....

Kamwene!… sio mbaya kuanza na salamu maana ndio utamaduni wetu watanzania. Katika soka kuna mambo mengi sana kiasi kwamba muda mwingine unaweza ukasahau hata kutoa salamu, kutokana na vurugu mechi za hapa na pale.

Nichukue nafasi hii pia, kutoa pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na watanzania kwa ujumla kwa kumpoteza kijana, mdau wa habari Ndugu Ruge Mutahaba, hakika tulimpenda lakini MwenyeziMungu amempenda zaidi, Jina lake liendelee kuhimidiwa. Mungu ampumzishe kwa amani!

Ligi kuu Tanzania bara ikiendelea kupamba moto, mashabiki na wadau wa soka barani Afrika, macho na masikio yao yapo karibu kabisa na ligi ya mabingwa Afrika. Kwa Afrika mashariki tunawakilishwa na Simba SC, MNYAMA.

Shauku ni kubwa kutokana na hali ya kundi D, huku kila timu katika kundi hilo ikiwa imesaliwa na mechi 2 pekee, moja ugenini na moja nyumbani huku ushindani ukiongezeka kutokana na tofauti ya alama kutoka nafasi ya 1 hadi ya 4.

Kundi D, hadi sasa mambo yako hivi, Al-Ahly wana alama 7, Simba alama 6, JS Saoura wana alama 5 na AS Club Vita wana alama 4. Simba na Al -Ahly wote wameshinda mechi 2 kati ya 4 walizocheza, wakati JS Saoura na AS Club Vita wakishinda mechi 1 kila mmoja.

Kutokana na msimamo huu, kama ni kufuzu kwenda robo fainali basi Simba na Al ahly wangefuzu kwakuwa wako nafasi mbili za juu. Hata hivyo kwa mujibu wa mechi za kundi D hadi kufikia hapa, kumekuwa na mfumo Fulani wa upataji matokeo, kwa mimi naweza kuuita ni KANUNI za kundi D.

Timu zote zinaonekana kuwa mbogo hasa zikiwa uwanja wake wa nyumbani. Simba na Al ahly zimefanikiwa kupata ushindi katika mechi zote mbili walizocheza nyumbani, Simba akifungwa zote mbili za ugenini na Al ahly akitoka sare moja ya nyumbani na kufungwa 1.


JS Saoura na AS Club Vita nao wameshinda mechi 1 za nyumbani na kutoa sare moja za nyumbani kwa kila mmoja, tofauti na Simba na Al ahly, timu hizi mbili zimekubali sare uwanja wake wa nyumbani. JS Saoura akitoka sare na Al ahly huku AS Club Vita akitoka sare na JS Saoura.

Timu zote nne , hakuna hata timu moja iliyowahi kupata ushindi ugenini, ushindi mkubwa ni sare, ambapo Al ahly na JS Saoura ndio waliofanikiwa kupata sare hizo. Kwa kuitazama timu moja hadi nyingine, kwa taswira za upataji matokeo kundi D litaonekana hivi;

Al- Ahly.
Wamecheza mechi 4, wameshinda 2 nyumbani dhidi ya Simba na AS Club Vita , wametoa sare 1 ugenini dhidi ya JS Saoura na kufungwa 1 ugenini dhidi ya Simba. Al –Ahly amebakiza mechi 2, dhidi ya AS Club Vita (ugenini) na JS Saoura ( nyumbani).


Kila timu inaonekana kuwa vizuri nyumbani, timu mbili tu ndio zimetoa sare zikiwa nyumbani. Maana yake ni kwamba Al ahly anaweza kutoa sare nyumbani kwa AS Club Vita kama aliavyofanya kwa JS Saoura.

Kwahiyo katika mechi hizi mbili, Al Ahly anaweza kujikusanyia alama 4, moja dhidi ya AS Club Vita ( ugenini) na 3 dhidi ya JS Saoura (nyumbani). Kama mambo yataenda hivi maana yake Al Ahly atakuwa na alama 10- 11.
Simba SC.
Imecheza mechi 4, imeshinda 2 (nyumbani) dhidi ya JS Saoura na Al alhy, wamefungwa 2 (ugenini) dhidi ya AS Club Vita na Al ahly. Simba hawajawahi pata sare nyumbani au ugenini. Mechi zote walizopoteza ugenini, wamepoteza kwa kufungwa goli nyingi, 5 kila mechi.


Simba amebakiwa na mechi mbili, moja ugenini dhidi ya JS Saoura, JS Saoura ambao kwa mujibu wa rekodi, walishawahi kutoa sare nyumbani dhidi ya Al ahly, hivyo kuna uwezekano mkubwa wa Simba kupata sare pia.

Js Saoura, ushindi wao mkubwa nyumbani ni wa goli 1-0 dhidi ya AS Club Vita. Wembamba wa ushindi huu unamaanisha kuwa Simba ina nafasi kubwa ya kupata sare. Pia kwa upande wa pili, JS Saoura nao wana nafasi ya kumfunga Simba nyumbani, kwakuwa, kundi hili limekuwa lina kanuni kama hii, yaani si mkubwa si mdogo akiwa nyumbani ana nafasi ya kushinda.


Mechi ya pili ni dhidi ya AS Club Vita nyumbani. Simba tayari imeshinda mechi zake zote za nyumbani hivyo ina nafasi kubwa ya kushinda dhidi ya Vita. Kwa mantiki hiyo Simba ina nafasi ya kupata alama 4 kwa mechi mbili zilizobaki, na kama watakosa sana basi alama 3 ni lazima.


Jumla Simba itakuwa na alama 9-10. Mchezo wao wa kwanza ni dhidi ya JS Saoura nchini Algeria, kwahiyo mechi hiyo ndio italeta mwanga kwa Simba kukusanya alama 4 au 3, yote yanategemea hali za wachezaji wa timu zote mbili na “game approach” za walimu.
JS Saoura.
Klabu hii imeshinda mechi 1 ( nyumbani) dhidi ya AS Club Vita, wamepata sare 2 moja nyumbani dhidi ya Al ahly na nyingine ni dhidi ya AS club Vita ugenini.

Mechi yao ya kwanza watakuwa nyumbani dhidi ya Simba na kwa nafasi yao wanaweza kupata matokeo ya aina mbili, kushinda au kupata sare tena.

Mechi ya pili ya JS Saoura ni dhidi ya Al ahly (ugenini). Mechi ya kwanza baina ya timu hizi mbili, JS Saoura walilazimishwa sare nyumbani kwao. Maana yake mechi ya pili Al ahly watakuwa nyumbani bila shaka watapata alama zote tatu, kwakuwa mechi zake zote mbili za nyumbani ameshinda kwa jumla ya goli 7, hivyo lazima na hii ashinde.

Mechi za JS Saoura zikiisha, huenda akajikusanyia alama 1 -3 na mwisho wa siku huenda akawa na alama 5-8.

AS Club Vita.
Katika michezo yake minne aliyocheza ameshinda moja nyumbani dhidi ya Simba, amefungwa mechi mbili ugenini dhidi ya Al ahly na JS Saoura na ametoa sare moja nyumbani dhidi ya JS Saoura.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Mechi zake zilizosalia ni dhidi ya Simba ugenini na dhidi ya Al ahly nyumbani. Katika mechi yao dhidi ya Al ahly, kuna uwezekano mkubwa wa kushinda au kupata sare. Rekodi zinaonyesha, wameshinda dhidi ya Simba, wakapata sare dhidi ya JS Saoura, kwahiyo wana weza kupata ushimdi na kutoa sare pia.

Kwa mechi ya Simba ugenini kuna hatihati ya kukosa alama zote tatu. Kumbuka mechi zote alizocheza Simba uwanja wa taifa ameshinda, hivyo nafasi ya Simba kushinda ni kubwa ukizingatia itakuwa ni mechi ya mwisho.

Ugumu wa mechi ya Simba vs As Club Vita utachagizwa na matokeo ya mechi za awali yaani Simba dhidi ya JS Saoura na AS Vita dhidi ya Al ahly. Jumla AS Club Vita wanaweza kupata alama 1-3 katika michezo yake miwili iliyosalia na mwisho wa siku kuwa na jumla ya alama 5-7.

Utabiri wa Msimamo wa Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi D baada ya mechi zote kumalizika

Kwa mantiki hii, Msimamo wa kundi D utakuwa kama ifuatavyo Al Ahly atakuwa anaongoza akiwa na alama 10-11, Simba watakuwa wa pili na alama zao 9-10, JS Saoura watakuwa na alama 5-8 na mwisho ni AS Cub Vita na alama 5-7.

Hadi kufikia hapa, kundi D tayari kumeshakuwa na kanuni kutokana na aina ya matokeo, na hata wachezaji kisaikolojia watakuwa wameshajiwekea kuwa nyumbani ni lazima kushinda, wakati ugenini si lazima.

Maana yake pia, kila timu inaweza kupata matokeo nyumbani, na inaweza kupata matokeo ugenini kwa JS Saoura na AS Club Vita japo sare, ndio maana Simba inakuwa na nafasi kubwa ya kufuzu robo fainali, kwakuwa inaweza kupata japo sare ugenini dhidi ya JS Saoura na kisha kushinda dhidi ya AS Club Vita na kuwa na jumla ya alama 10.

Msimu wa 2017/18 Kombe la mabingwa Afrika, timu nyingi zilifuzu zikiwa na alama kuanzia 13 kushuka chini hadi 8. Ukiangalia Msimu huo, kundi A Al-Ahly na Esperance de Tunis zilifuzu zikiwa na alama 13 na 11 mtawalia, kundi B TP Mazembe ikiwa na alama 12 iliambatana na ES Setif ikiwa na alama 8 kwenda robo fainali, Kundi C Wydad Casablanca na Horoya zilifuzu kwa kujikusanyia alama 12 na 9 mtawalia, na kundi D Etoile du Sahel akiwa na alama 12 akiambata na 1* de Agosto waliokuwa na alama 9 kufuzu robo fainali.

Kwa mantiki hiyo, Simba kuwa na alama 10 na kufuzu robo fainali ni utamaduni kwa vilabu vingi vilivyofuzu hatua hii kwa miaka mingi sasa. Hata hivyo wana nafasi kubwa ya kupata alama 4 kati ya 6 wanazo zigombania nawaona Simba wameimalika maeneo mengi kiasi cha kuwawezesha kupata japo sare ugenini na kupata alama tatu uwanja wa taifa. Kila la heri Klabu ya Simba.

[poll id=”9″]

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x