Stori

Matamasha Yetu, Mashabiki, Pesa na Jamii

Sambaza....

Imekuwa ni kawaida sasa kwa timu za Tanzania kufanya matamasha ya utambulisho wa timu na wachezaji wapya kabla ya msimu mpya wa mashindano kuanza.

Matamasha ya utambulisho wa timu kabla ya msimu kuanza imeanza kuwa tamaduni yetu. Timu ya Simba ndo waanzilishi wa matamasha haya ya timu nchini mnamo mwaka 2009 na kupelekea baadhi ya vilabu vingine kushawishika kuwa na siku zao maalumu za kutambulisha timu mbele ya mashabiki zao.

Mfano sasa tunaona Yanga, Azam, Namungo, Singida Fountain Fc na timu nyingine za ligu kuu Tanzania Bara huwa na utaratibu wa kufanya matamasha ya utambulisho wa wachezaji wao mbele ya mashabiki wao.

Kila mwaka maboresho makubwa yanaonekana, kila mwaka matamasha yanaonesha kukua tofauti na awali ambapo hata muitikio wa mashabiki ulikuwa mdogo tofauti na sasa ambapo muitikio wa mashabiki ni mkubwa sana, dhana ya matamasha iko vichwani wanafahamu na wanaelewa nafasi ya ushiriki wao katika matamasha.

Fauka na hayo, Matamasha sasa yamekuwa zaidi ya burudani wafanya biashara na makampuni wanayaona kama fursa ya kujitangaza na kuuza huduma zao, kwamfano Tamasha la Simba day lilizaminiwa na CRDB Bank ikiwa ni sehemu ya ushirika wao kama wadhamini, NMB nao hawakuwa nyuma kuidhamini wiki ya Wananchi “Yanga” .

Viongozi wa Yanga na CRDB Benki wakitia saini mkataba wa ushirikiano wa Wiki ya Wananchi.

Timu zetu zinapata mapato makubwa sana kupitia matamasha haya kwa kujikusanyia pesa kutoka kwa wadhamini mbalimbali na kubwa zaidi ni viingilio vya mlangoni (getini) ambapo mashabiki hununua tiketi ili kuingia uwanjani.

Hamasa ni kubwa na muitikio wake unashangaza, makampuni yanamiminika na wadhamini wanafurika wanataka kuitumia fursa, wanataka jukwaa la matamasha ili kujitangaza, wanataka nafasi ili kujiuza na kutangaza huduma kwani kupitia Azam tv matukio yote yanakuwa mubashara hivyo wanapata nafasi ya kuonekana kwa walaji wengi.

Lakini pia matamasha yamekuwa ni sehemu ya jamii kwani yanaigusa jamii moja kwa moja hususani watu wenye uhitaji maalumu pamoja na usafi.

Takwimu za mashabiki wa Simba za uchangiaji damu katika wiki ya Simba Day.

Kwamfano, katika #Wikiyamwananchi# (Yanga) na wiki ya #Unyamamwingi# (Simba) ni kielelezo tosha cha kuonyesha kuwa matamasha haya ni sehemu ya jamii.

Mashabkiki wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali kama vile usafi wa mazingira, uchangiaji damu salama na kubwa zaidi ni hamasa na michango kuwachangia watu wenye uhitaji kama vile wazee, watoto yatima na wanaoishi kwenye mazingira magumu na kubwa kuliko vilabu vimekuwa vikiunga na kutia mkono wake katika haya.

Kwamfano katika wiki ya #unyamamwingi# (SIMBA) kulifanyika mnada wa kibegi cha uzinduzi wa jezi na jezi zake na walipata kiasi cha zaidi ya millioni 30 na zote hizi walizigawa kwa watu wenye uhitaji.

Kibegi cha Simba kikiwa safari katika mlima Kilimanjaro, ambacho kilipgwa mnada.

Matamasha yamekuwa ni baraka, matamasha yameleta hamasa ya kupenda soka, matamasha yanachagiza mapinduzi ya soka, lakini bado matamasha haya hayajakata kiu ya mashabiki, bado matamasha haya yanauliza maswali mengi bila majibu, bado matamasha yanazua migogoro ya kinafsi baina ya mashabiki lakini bado matamasha yanawabagua mashabiki.

Mwingine atajiuliza kivipi ilihali tunaona yamefana kwelikweli? Basi nikutoe shaka Kandanda.co.tz iko hapa kukutoa wasiwasi huo;

Kupeleka matamasha mikoani.
Imekuwa ni kawaida kwa timu zetu zenye uzani mkubwa(Simba, Yanga, Azam) kufanya matamasha yao jijini Dar es salaam, hii haijakaa sawa kwani baadhi ya mashabiki wanataka kuziona timu zao na wako mbali na Dar na hawana uwezo wa kufika Dar, isitoshe mashabiki wengi wako mikoani hivyo itakuwa jambo la busara sana kama matamasha haya yataanza kupelekwa mikoani tofauti na makao makuu ya timu.

Kwanza itavutia mashabiki wengi na pia itawapa ile thamani ya kujiona wako karibu na timu yao hivyo kuufanya ushiriki wao kuwa wa kikamilifu na wenye tija kwa shabiki na timu kwa ujumla, lakini pia kutawapa wadhamini na makampuni yenye ubia na vilabu kuonekana na kuuza huduma zao kwa walaji wengi zaidi tofauti na Dar es salaam pekee.

Mashabiki wa Yanga katika Dimba la CCM Kirumba.

Kuboresha mfumo wa Tiketi
Mara zote hamasa ikiwa kubwa basi tarajia muitikio mkubwa, watu wakiitwa kwa hamasa kubwa watakuja kwa wingi wao. Licha ya kuuza na kugawa tiketi kieletroniki lakini bado tuko nyuma sana katika kuingia viwanjani na namna ya ugawaji tiketi kiasi cha baadhi ya mashabiki kupata usumbufu licha ya kulipia tiketi zao kwa wakati lakini bado wanapata karaha, kwamfano katika Tamasha la siku ya Simba mnamo tarehe 6 mwezi huu tumeshuhudia baadhi ya mashabiki wamekosa nafasi ya kuingia uwanjani ilihali tiketi wanazo.

Huku ni kumsumbua shabiki na huku ni kumkosesha thamani, timu hazijali kuhusu mashabiki wao bali wanajali kile wanachopata na wakishapata basi hawajali tena, na hii inafukuza mashabiki kwani shabiki anaona ni bora abaki nyumbani kuliko kwenda uwanjani kwani atakutana ghasia, hivyo vilabu vilitizame hii ili viweze kuwavutia mashabiki wengi kuja uwanjani.

Hali inavyokua pale mashabiki wanapojitokeza kwa wingi katika viwanja vyetu.

Kuongeza wawekezaji na wadhamini wengi ili kupunguza viingilio na kuvifanya viwe rafiki kwa mashabiki
Matamasha ni burudani na mashabiki wanatakiwa kuifurahia burudani. Kuongeza wadhamini na wawekezaji katika matamasha kutasaidia timu kuweza kumudu gharama za uendeshaji tamasha bila kutegemea viingilio vya getini na hii itasaidia kuvipunguza na kuvifanya viingilio kuwa rafiki kwa mashabiki hata wenye uwezo wa chini kuweza kumudu gharama za tiketi.

Kwamfano tamasha la Yanga la mwaka huu #mwananchiday# viingilio vilikuwa vikubwa sana, kiingilio kidogo zaidi kilikuwa 10,000 kiasi ambacho sio mashabiki wote wa Yanga waliweza kukimudu na kusababisha baadhi ya mashabiki kutokufika uwanjani na kupelekea baadhi ya majukwaa kuwa tupu katika kilele cha siku hiyo.

NB: UKIONA VYAELEA UJUE VIMEUNDWA.

Sambaza....