Sambaza....

Kwa jicho la kawaida unaweza usiione sawasawa kazi ya miguu yake, lakini ukimtazama kwa jicho la kiufundi unaweza ukagundua vitu vingi sana na ni mchezaji mwenye madhara makubwa kwa wapinzani waliokutana na Yanga sc mpaka sasa, sio mchezaji mwenye vitu vingi lakini yeye amekuwa akifanya vile vya msingi vinavyoisaidia timu yake kupata matokeo bora

Huyu sio mwingine ni Pius Buswita, kiungo mshambuliaji wa mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania bara Yanga sc, ni mchezaji mwenye kipaji halisi cha soka na asiye na makuu amesimama kama siraha ya kocha George Lwandamina kwa hakika amekuwa akitoa kile ambacho kocha huyo anakihitaji

Ndio….Lwandamina amegundua namna gani anaweza kumtumia Buswita, na kumpa kile anachohitaji kwa maana huyu sio mchezaji wa kumpa majukumu mengi ya kukaba ila ni mchezaji anayeweza kukurahisishia upatikanaji wa mabao, kama sio yeye kufunga basi atatoa pasi kwa mwingine ili afunge

Mwanzoni kabisa mwa msimu huu wa 2017/18 ilionekana kama Ibrahim Ajib ndiye angeweza kuibeba Yanga mabegani hasa baada ya Donald Ngoma kuonekana kutokua sawa, lakini taratibu hali ikaonekana kubadilika licha Ajib kufunga bado pembeni yake alionekana Buswita na bahati mbaya kwa Ajib kiwango chake kimeonekana kushuka kidogo tofauti na mwanzoni mwa msimu

KWA NINI BUSWITA?

Jibu ni rahisi tu kwa mchezaji huyo licha kujitambua kuwa anajua mpira, lakini amekua sio mvivu wa mazoezi ndio maana kazi ya kupambana uwanjani imekua sio ngumu kwake, Buswita anapambana kwa machozi, jasho na damu anayatendea haki majukumu anayopewa uwanjani,

Image result for Buswita

Mara nyingi wachezaji wa aina Buswita ni wavivu wa mazoezi sio wachezaji wanaopenda kujituma sana, hiyo imekuwa tofauti kwake ni mchezaji anayefanya sana mazoezi anaonesha kuna kitu anachokitafuta kwenye mpira na sitoshangaa nikisikia anapitia mule walipopita kina Mbwana Samatta na Simon Msuva wachezaji hawa licha kujijua kuwa wanajua mpira lakini hawakuwa wavivu mara nyingi walijituma sana

AMEKUWA NI SIRAHA INAYOBADIRISHA MIKONO YA LWANDAMINA

Licha ya kocha George Lwandamina kutembea akiwa na jeshi dogo lakini amekuwa akijivunia wingi wa siraha anazoweza kubadirisha namna ya ushikaji na zikamsaidia kupambana katika ubora ule ule, moja kati ya siraha hizo ni Pius Buswita kiungo mshambuliaji anayemudu kucheza nafasi nyingi za mbele, amekuwa akimtumia kama kiungo wa pembeni lakini kuna wakati anampanga kama kiungo mshambuliaji ama mshambuliaji wa mwisho akicheza kama falsa 9 na nafasi zote hizi Buswita hucheza katika ubora uleule

Huyu ni mchezaji mwingine anayemfanya Lwandamina kupiga hatua moja mbele huku akitabasamu kila uchwao, ukimuondoa Papy Tshishimbi basi mchezaji mwingine anayefata ni Buswita katika kumuongezea chaguzi kocha huyu

Hiki ni kitu kingine kinachomfanya Buswita kuwa mchezaji wa pili anayeibeba Yanga mabegani mwake, uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani, kutengeneza nafasi na pia kufunga mabao licha ya kufunga mabao matano kwenye ligi kuu lakini amehusika katika upatikanaji wa mabao mengi ya Yanga msimu huu

Ndio maana kwa jicho langu, namuona muuaji wa kimyakimya asiyetajwa sana asiyetajwa kwenye kikosi cha Yanga, kwa maana Buswita sio mchezaji anayecheza na jukwaa hawezi kufanya kama Haruna Niyonzima au Ibrahim Ajib, sio mburudishaji kama hao lakini ni mchezaji anayevutia kumtazama kwa jicho la kiufundi

Huyo ndiye Pius Buswita muuwaji wa kimyakimya, mwenye hari ya upambanaji

Sambaza....