Sambaza....

Wakati mataifa mbalimbali ya Afrka yakiwa katika maandalizi ya kucheza michezo ya kuvufuzu kwa CA 2019-Cameroon, baadhi ya makocha wa klabu wamejumuika na timu hizo za Taifa. Mwinyi Zahera raia wa Congo DR ambaye ni kocha mkuu wa Yanga SC amerejea kwao kujumuika na timu yake ya Taifa, pia Hemed Morocco ambaye ni kocha mkuu wa Singida United yeye amejumuika na Mnigeria, Emmanuel Amunike kama msaidizi wa timu ya Taifa ya Tanzania.

Najiuliza kwa wakati huu ( siku saba hadi kumi) klabu zao zinafundishwa na nani? Je, wasaidizi wao wanatosha kuendelea kuwekeza mbinu kwa wachezaji waliosalia klabuni? Wakati mwingine ni lazima tukubali kuwa ‘mshika mawili, moja humponyoka.’ Napowaza na kufikiria kuhusu makocha hao wakuu wa Yanga na Singida United kuwa katikas majukumu mengine nje ya klabu zao, namkumbuka kocha mwenye ujasiri-marehemu James Siang’a.

Siang’a ( mwenyezi Mungu amrehemu) wakati akiwa katika ubora wake kiufundishaji mwaka 2003, timu ya Taifa ya Kenya ilimuhitaji, na wakati huo huo uongozi wa FAT-sasa TFF chini ya Muhidin Ndolanga nao ulimuhitaji na kocha huyo alikubali kujiunga Stars wakati huo huo akiwa ni kocha mkuu wa Simba SC, lakini baada ya mchezo mmoja tu kama sijasahau ule ambao Stars ilichapwa na Benini, Siang’a alikataa kuendelea kuwa ‘kiraka wa muda’ na kusisitiza kuwa hawezi kuwatumikia ‘mabwana wawili kwa wakati mmoja.’

Ni zaidi ya miaka 14 imepita tangu wakati ule lakini hivi sasa tunaendelea kuona Yanga na Singida zikiwakosa makocha wao wakuu ambao waliiingia nao mikataba na kuwalipa mishahara mikubwa wakiwa nje ya klabu wakifundisha timu nyingine. Unaweza kusema ni uzalendo, lakini kwa nyakati hizi za sasa jambo hilo halipaswi kuendelea.

Yanga na Singida United zinapaswa kuwaambia makocha wao hao wachague moja- kuendelea kubaki klabuni au kuchukua kazi waliyonayo katika tiimu zao za Taifa. Kikawaida, miezi ya Machi, Juni, Septemba na Novemba timu za Taifa kote duniani huwa na michezo. Inaweza kuwa ya kufuzu kwa michuano Fulani ( mfano sasa mataifa ya Afrika yanasaka tiketi za kufuzu CAN ijayo) ama michezo ya kirafiki.

Sasa je, ni sahihi kwa vipindi hivyo kila vinapofika makocha hao wa klabu kuziacha timu zao kwa siku saba hadi kumi? Mwezi uliopita tuliona kocha mkuu wa JKT Tanzania, Bakari Shime akiifundisha timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania huko Kigali Rwanda katika michuano ya Cecafa, ndiyo aliipa taji muhimu katika nchi lakini ukweli klabu yake ilimkosa mtu muhimu kwa wiki mbili na matokeo yake bado wanaangaika kujiweka sawa katika ligi hivi sasa.

Kocha mkuu wa klabu kwanini akubali ‘kuwa kiraka wa muda’ sehemu nyingine? Hata kama ni utaifa inamaana hakuna makocha wengine? Siafiki ili la kina Zahera, Morocco na Shime kuwa na majukumu mengine kiufundishaji wakati ni waajiriwa rasmi katika klabu zao kama makocha wakuu. Kuwaachia kazi makocha wasaidizi kwa siku 40 ndani ya miezi kumi upande wangu naamini ni sababu mojawapo inayocweza kuchangia klabu kushindwa kufikia malengo yake.

Sambaza....