Said Juma Makapu
Ligi Kuu

Viongozi Yanga SC wanapaswa kujitathimini

Sambaza....

Habari za Jumatatu ewe mshabiki na mdau wa soka la Tanzania, ni matumaini yangu kuwa mzima afya kabisa………Na hakika tunapaswa kumshukuru Mungu kwa kutuonesha siku nyingine kwa uwezo wake ndio maana tupo.

Mengi mazuri ametufanyia likiwemo la kila Mwanadamu kumpa Upeo wake wa kufikiri ili aweze kuwaza awazacho…….katika hili hakuumba akili mbovu ila huja kwa bahati huku zingine zikitokea kutokana na zinavyotumiwa

Ebu tuliache hilo kwa maana sio lengo kuu la Makala yangu ya leo……… Hapo jana tulishuhudia mabingwa wa zamani wa ligi ya Vodacom Tanzania bara nawazungumzia Yanga SC, wakiondoshwa mapema kunako michuano ya Sportpesa Super Cup kule nchini Kenya

Tatizo linaweza kuwa sio kuondoshwa tu kunako michuano hiyo, bali ni mwenendo mzima wa klabu hiyo tangu kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Mahboob Manji, hapa tukaishuhudia ikianza kupita katika njia ngumu kabisa

Yanga ikawa kama mtoto yatima anayeishi katika mazingira magumu, na kwa bahati mbaya hata ndugu nao walianza kumtelekeza na kushindwa kushikamana ili kutoa huduma kwa mlengwa

Asilimia kubwa ya makundi ya wale waliojiita Makomandoo wa klabu hiyo walijitoa, mara baada ya Manji kuondoka walikataa kusimama kidete….lakini yote kwa yote udhaifu mkubwa umeiponza klabu

Tatizo lingine ni Viongozi na hili ndilo tatizo Mama kwenye klabu hiyo, wengi wanaonekana hawakuwa tayari kuongoza klabu bila ya uwepo wa Manji ndio maana alipoondoka tu na wao walishindwa kusimama kama viongozi wa klabu na muda kujifanya wako bize na shughuri zao binafsi

Kwa muda mlefu sasa Yanga imekuwa ikiongozwa na watu watatu tu, hao ndio wanapambana kila uchwao kuhakikisha mambo yanaenda, Makamu Mweyekiti yupo bize na shughuli za TFF ni kama wameshindwa kuwa pamoja

Ni wazi timu haiwezi ongozwa na Afsa Habari, Katibu pekee……timu ni tume yote iliyopo madarakani

Binafsi sitaki kuamini kuwa matokeo mabaya ya Yanga SC ni kutokana na kukosa pesa pekee………. .bali mtazamo wangu ni mmong’onyoko wa kiuongozi ndani ya klabu hiyo ndio unaoitafuna hawa ni kama wameshindwa kuongea Lugha moja na kujua kipi wafanye kwa masilahi ya klabu yao

Dunia ya leo watu hawatafuti kwanza pesa ili wafanikiwe, bali ni Mawazo, Mikakati, Mbinu na Maarifa hutangulia kwanza ili pesa ikija isimame katika nguzo imara

Ndio maana binadamu wenye Mawazo chanya, uwezo wa kusimamia na kuongoza jambo, tafakaria makini, mtazamo wa mbali na karibu. Ndio watu ambao hupendwa sana na watu wenye fedha zao ili waweze kufanikiwa na kuhakikisha ulinzi wa mitaji yao

Katika hilo viongozi Yanga wanapaswa kujitathimini walipotoka, walipo sasa na wanapoelekea……..imani yangu majibu watayapata

Huu sio wakati wa wao kunyoosheana vidole ama kumtafuta mchawi, bali wanapaswa kuwaeleza matatizo Wanachama wa klabu hiyo kabla kuangalia nani awasaidie

Pia sio wakati wa kumuona anayewakosoa ni mamluki, sio shabiki au Mwanachama wa Yanga SC bali wanapaswa kuanzia hapo wanapokosolewa ili kuitafuta njia sahihi ya kujinasua katika matatizo yanayowakabiri….kwa maana busara inaelekeza kuwa ili uwe bora kubali kukosolewa

Nimalize kwa kusema kuwa Watu wengi katika maisha hawashindwi kwa sababu wana malengo makubwa na wanashindwa kuyafikia bali huwa na malengo madogo sana kiasi ambacho hata wakiyafanikisha huendelea kubaki katika kundi la walioshindwa.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x