Soccoia Lionel
Ligi Kuu

Wafaransa wa A.Lyon ni muendelezo wa ‘filamu za kuchekesha’ za Zamunda

Sambaza....

Wakati anatua nchini kocha Mfaransa, Soccoia Lionel alisema kuwa amekuja nchini kuisaidia African Lyon kufikia kiwango cha juu, lakini baada ya michezo tisa, ushindi mara moja, sare tatu na vipigo vitano katika ligi kuu Tanzania Bara kocha huyo pamoja na mshambulizi Mfaransa, Victor Da Costa wamebwaga manyanga katika klabu hiyo ya kuondoka nchini.

Rahim Zamunda ni mmiliki wa klabu ya African Lyon na katika kipindi cha miaka saba iliyopita timu hiyo imeshuka daraja mara tatu lakini imekuwa na matokeo mazuri katika ligi daraja la kwanza na hivyo imekuwa klabu ya ‘kupanda na kushuka.

Zamunda akiwa na Kochawa A.Lyon

Nakumbuka, miaka mitano iliyopita mmiliki wa klabu hiyo, Rahim Zamunda aliwahi kutishia kunipeleka mahakamani mara baada ya kuandika kuhusu hali mbaya ya kiuchumi iliyokuwepo klabuni hapo na kupelekea wachezaji kutolipwa mishahara kwa zaidi ya miezi mitatu hivyo wachezaji wengi wakaanza kucheza ligi za mitaani ‘Ndondo’ ili angalau kuweza kupata pesa ya kuwafanya waishi.

Hata kabla ya wakati huo ( 2013) klabu hiyo kwa muda wote iliyo chini ya Zamunda imekosa ‘uhai’. Imekuwa ni klabu ya klabu zenye kulipa maslai madogo huku wachezaji wengi wa kigeni wakiingia na kutoka; taarifa nyingine zikidai nyota wengi wa klabu hiyo usainiwa ‘kiujanja-ujanja’.

Mfano, Da Costa, wakati atatua nchini mwanzoni mwa msimu huu ilisemwa kwamba Mfaransa huyo amesaini mkataba wa miaka miwili lakini kwa taarifa za ndani ni kwamba nahodha huyo wa Lyon alisaini mkataba wa miezi sita tu yeye sambamba na kocha wake, Lionel.

Zamunda kama kweli anahitaji klabu yake ikue kimpira na kiuchumi ni lazima akubali kuwaajiri watu ambao wanaweza kumsaidia katika suala la masoko na si kila kitu kubaki upande kwa vile tu ni mmiliki. Anatakiwa kuwa mkweli katika mawazo yake na si kudanga.

Kuna wakati alileta kocha kutoka Argentina sijui nini kiliendelea, pia amewahi kuleta watu toka Ureno sijui waliishia wapi na sasa amekuja na Wafaransa ambao nao ‘wamekimbia’ kwa sababu za kimaslai. Kwa klabu kama African Lyon kuwasaini kocha Mfaransa na straika Mfaransa hakukuwa na maana ya kimpira labda kama nyuma ya pazia kuna mambo mengine.

Rekodi ya Africa Lyon katika Ligi Kuu sasa

Nakuwa najiuliza ni kwanini mmiliki wa klabu hii amekuwa na kawaida ya kuwaacha makocha wazawa wanaopambana kuipandisha daraja timu yake kila inaposhuka daraja na kuwaleta ‘wazungu’ ambao kimsingi kuwalipa kwake ni ghali mno huku uwezo wao ukiwa mdogo?

Zamunda amekuwa mtu wa kulazimisha mambo yasiyowezekana wakati mwingine, kumbuka wakati ule alipoishutumu TFF kumuhujumu baada ya uongozi wa rais wa Shirikisho wakati huo Leodgard Tenga kumkatalia kuingia mkataba na kampuni ya simu ya Zantel.

TFF ilikuwa sahiihi kwa wakati ule kwasababu kulikuwa na vipengele vya kimkataba na Vodacom wa kuzuia wadhamini wenye maslai ‘mfanano’ na Voda kujitangaza katika jezi za klabu. Haitoshi, kumbuka wakati Fulani Zamunda huyuhuyu alirumbana sana na utawala wa Tenga kwa sababu ulimkatalia kutangaza jina la Seatle Sounders FC ya Marekani katika jezi za Lyon- yaani Zamunda alihitaji klabu yake kutumia jezi zenye kuitangaza klabu hiyo ya ligi kuu ya Marekani katika kifuani mwa jezi zao.

Kwa namna ambavyo amekuwa akiiendesha klabu hiyo ni wazi anaonyesha ni mtu asiye na malengo makubwa kimpira zaidi ya kwamba amekuwa akihitaji kupata zaidi pasipo kutazama ni kwa njia gani. Leo hii Lyon inadanganya kuhusu mikataba ya wachezaji wake ili iweje?

Ni kweli Wafaransa wao walisaini miaka miwili kama ilivyosemwa awali? Nachofahamu ni kwamba walisaini miezi sita sita tu na lengo kubwa ilikuwa ni sababu za kibiashara si kimpira. Ukitazama ubora wao kwa kocha Leonel na mshambulizi Da Costa unaweza kujua ni kwanini watu hawa walitoka kwao ulaya tena nchini Ufaransa na kuja sehemu hii isiyo na mipango!

Kuna mambo yanachekesha kama si kufurahisha katika soka la Tanzania- mfano hili la Wafaransa wa Lyon, kwa klabu kama hii ambayo inashindwa kuwalipa wachezaji wa ndani mishahara ya Tsh.600, 000 kumchukua mzungu na kumlipa zaidi ya dola 1000 kwa mwezi ni ‘ujinga’ ambao ndani yake huzalisha upambavu. Zamunda amekuwa na vichekesho vingi na katika hili anapaswa kujitazama upya kama kweli yeye ni mwanasoka-mfanyabiashara. Aachane na mambo ya kuchekesha.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x