Sambaza....

Yanga SC, imepata alama ya kwanza katika hatua ya makundi ya kombe la Shirikisho Afrika kufuatia sare tasa ya bila kufungana na Rayon sports ya Rwanda, katika mchezo wa kundi D ulipigwa kunako uwanja wa taifa jijini Dar es salaam

Sare hiyo, inaifanya Yanga kuendelea kuburuza mkia kunako kundi hilo linaloongozwa na USM Alger yenye alama nne, huku Gol Mahia na Rayon zikiwa na alama mbili kila mmoja

Mchezo huo ulioamuliwa na waamuzi kutoka Angola, Helder Martins De Carvalho aliyesaidiwa na washika vibendera Ivanido Meirelles De O Sanche Lopez na Wilson Valdimiro Ntyamba timu zote zilicheza kwa tahadhari kubwa huku zikipoteza nafasi kadha za kufunga

Mzambia Obrey Chirwa, alipoteza nafasi ya kufunga kunako dakika ya 82, baada kugongesha mwamba wa juu kufuatia kazi nzuri ya kinda Yusuf Mhilu, huku Rayon wakitumbukiza mipira kimakosa mara mbili katika nyavu za Yanga

Ikumbukwe kuwa, Yanga ilianza vibaya mechi yake ya kwanza kwa kuchapwa mabao 4-0 na USM Alger kunako dimba la Julai 5, 1962 mjini Algiers

Michuano ya kombe la Shirikisho inasimama kwa sasa kupisha fainali za kombe la Dunia mwezi ujao nchini Urusi na Yanga inataraji kumaliza mechi za mzunguuko wa kwanza kwa kuwafata Gor Mahia jijini Nairobi Julai 18 mwaka huu

Sambaza....