Mabingwa Afrika

Haji Manara uko kimya sana, leo ni siku yako

Sambaza kwa marafiki....

Haipendezi wewe kukaa kimya, haipendezi wewe kutotia neno lolote kwenye mechi ya Leo. Mechi ambayo inahitaji sana mdomo wako ili kujaza uwanja wa Taifa.

Mdomo wako una thamani kubwa kwa sana. Thamani ambayo umeitengeneza wewe mwenyewe kulingana na soko letu la mpira.

Ulilijua soko letu linahitaji nini, uliona kabisa ni nini wanunuzi wa mpira wetu wanataka na wewe ukawapa kulingana na matamanio yao.

Mashabiki wengi wanatamani majigambo, wanatamani kuonekana wao ni Mwamba mkuu mbele ya miamba midogo midogo.

Unataka kuwakamata wanunuzi wa wetu wa mpira ?, wasifu hata sehemu ambayo hawatakiwi kusifiwa. Hapa utawakamata sana.

Na utakuwa nao karibu sana na watakuunga mkono sana na kuwa wafuasi wako kwa kiasi kikubwa. Hata kipindi ambacho utakapowaambia wafanye kitu watafanya tu.

Ukiwaambia waje uwanjani watakuja kwa wingi , ukiwaambia waje kununua jezi katika duka lililochaguliwa kwa ajili ya kuuza jezi wataenda tu.

Kwa sababu moja tu , umewapa kitu ambacho wanataka. Umewaambia timu yao ni bora kuzidi timu yoyote. Umewazodoa vya kutosha Yanga.

Hapa ndipo Haji Manara alivyofanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwateka mashabiki wa Simba.

Aliwaambia Simba ni brand kubwa kuliko brand yoyote Tanzania. Yani kwa kifupi kuliko hata brand ya neno Tanzania.

Waliamini na alizidi kuwaaminisha, wachache waliokataa kauli yake hawakumfanya asiendelee kupigania kauli yake.

Alisimamia kauli yake haswaa na ikapita na wengi wakaamini kuwa Simba ni brand kubwa sana kuliko brand yoyote hapa Tanzania.

Hii ikapita, akawaaminisha Simba ni timu bora sana. Timu ambayo inaweza kupata matokeo chanya katika uwanja wowote.

Timu yenye kikosi imara haswaaa!, wana Simba waliamini sana na kumwamini mno Haji Manara, Haji Manara akawa na wafuasi wengi mno.

Wafuasi ambao aliwatumia kwa manufaa ya klabu ya Simba na manufaa yake binafsi kibiashara, jambo ambalo siyo dhambi.

Kupitia wafuasi hao Haji Manara amefanikiwa sana kuwa balozi wa makampuni mbalimbali ya biashara.

Kupitia kupata wafuasi wengi amefanikiwa kuja na bidhaa yake ya manukato. Bidhaa ambayo isingekuja bila hao wafuasi.

Wafuasi hao hao aliwatumia kujaza uwanja wa Taifa kwenye shughuli mbalimbali za klabu ya Simba.

Unakumbuka sherehe za Simba Day zilivyokuwa zinafana kwa kiasi kikubwa?, zilivyokuwa zinajaza mashabiki wengi?

Unakumbuka hata kwenye mechi za kimataifa zilivyokuwa zinajaza watu ?, unakumbuka kampeni iliyofanywa kwenye mechi dhidi ya Nkana red Devil?

Unaukumbuka ule umati?, umati ulioshangilia kwa nguvu baada ya goli la Chama ?, bila shaka umati huo unaukumbuka vizuri sana.

Ule Umati ulisababishwa na mtu mmoja, Haji Manara. Huyu alishiriki kwa kiasi kikubwa kuwaaminisha watu kuja kuwa sehemu ya kihistoria ya mechi hiyo.

Najua kabisa kwa sasa klabu ya Simba inapitia matokeo mabovu, wamefungwa mechi mbili mfululizo kwenye ligi ya mabingwa barani Afrika.

Tena kwa jumla ya magoli 10, magoli mengi sana , magoli yanayokatisha tamaa sana. Kuna wimbi kubwa la mashabiki kwa sasa wamekata tamaa.

Mtu pekee ambaye anatakiwa kujitokeza kwa sasa na kuwapa moyo mashabiki wa Simba ni Haji Manara.

Huyu ambaye alishiriki kuwashawishi mashabiki kujaza uwanja kwenye Simba Day, ni huyu huyu aliyewaaminisha mashabiki kuwa wanaweza kuujaza uwanja kwenye mechi ya Nkana Red Devil.

Ndiyo huyu huyu aliyewaaminisha mashabiki wa Simba kuwa timu yoyote kwenye uwanja wa Taifa haiwezi kutoka inapocheza na Simba.

Mechi hii ya Leo inahitaji sana neno la Haji Manara. Neno la kuwakumbusha mashabiki kuwa Simba iko taifa.

Na hakuna timu inayoweza kuifunga Simba kwenye uwanja wa Taifa kwa hiyo wasisite kuwa sehemu ya historia ya kumfunga Mwarabu Taifa.

Tafadhali tumia viungo rasmi kusambaza habari zetu. Facebook, Twitter au Barua Pepe. Kama utataka kutumia habari zetu tuandikie kupitia habari@kandanda.co.tz