Simba Sc Mabingwa wa Ngao ya Jamii 2023-2024
Stori

Simba Yaweka Historia, Mrithi wa Manula Aleta Kizaazaa Mkwakwani

Sambaza....

Wekundu wa Msimbazi Simba wamefanikiwa kuibuka na ushindi katika mchezo wa fainali ya Ngao ya Jamii kwa mikwaju ya matuta mbele ya Watani zao Yanga.

Simba wamefanikiwa kutwaa taji hilo kupitia mikwaju ya penati baada ya dakika tisini kukamilika kwa suluhu na kupelekea mlinda mlango Ally Salim kuibuka shujaa.

 

Katika mchezo huo uliokua mzuri na wakuvutia Yanga itabidi wajilaumu wenyewe kwani walicheza vyema huku wakitengeneza nafasi kadhaa za wazi na kushindwa kufunga bao.

Yanga walitawala vyema mchezo huo huku wakicheza vizuri mno, washambuliaji wake Clement Mzize na Kenedy Musonda kama wangekua makini zaidi huenda wangeipatia bao timu yao na kuipa uongozi Yanga pasi na kufika mikwaju ya penati.

Yanga ambao waliwazidi umiliki wa mpira Simba, mashuti yaliyopigwa langoni na kuutawala vyema mchezo lakimi walishindwa kufunga walau bao moja ili kuumaliza mchezo katika dakika tisini.

Winga wa Simba Willy Onana akithibitiwa na walinzi wa Yanga.

Katika mikwaju ya penati shujaa wa Simba alikua ni Ally Salim ambae alifanikiwa kucheza penati tatu za nyota wa Yanga Khalid Aucho,  Komassi Yao na Pacoune Zouzua na kupelekea kufuta makosa ya Moses Phiri na Saido Ntibazonkiza waliokosa penati kwa upande wa Simba.

Kwa upande wa Yanga ni Aziz Ki pekee ndio aliyefunga penati wakati kwa Simba ni Mzamiru Yassin, Willy Onana na Jean Baleke ndio waliofunga penati zao na kupelekea mchezo kumalizika kwa Simba kushinda penati tatu kwa moja.

Baada ya ushindi huo Simba inaingia katika rekodi yakutwaa Ngao ya Jamii kwa mara yakwanza katika mtindo mpya wakushirikisha timu nne.

Shomary Kapombe akimuacha Lomalisa Mutambala.

Pia kwa ushindi huo unaifanya kuizuia Yanga isitwae taji hilo mara tatu mfululizo. Kama Yanga angeshinda leo maana yake angekua ametwaa Ngao mara tatu mfululizo tena mbele ya Simba.

Katika mchezo wa awali wa kutafuta mshindi watatu Azam Fc walifanikiwa kuifunga Singida FG Fc mabao mawili kwa sifuri. Magoli ya Azam yalifungwa na Prince Dube na Abdul Sopu.

 

Sambaza....