Emmanuel Amunike, kocha wa Tanzania
Blog

Aishi ndiye aliyewaondoa Erasto, Kapombe, Dilunga, Kichuya na Mkude Stars, au ni Amunike, Simba, TFF au muda?

Sambaza....

KOCHA mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ( Taifa Stars) Mnigeria, Emmanuel Amunike amewaondoa kikosini wachezaji watano kati ya sita aliowaita kutoka klabu bingwa nchini Simba SC katika kikosi chake ambacho kitawavaa Uganda ( Cranes) katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon.

Amunike- mchezaji nyota mshindi wa CAN 1994 ambaye alipata kuwa mchezaji bora wa Afrika mwaka 1994 amewaacha walinzi Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, viungo Hassan Dilunga, Jonas Mkude na Shiza Kichuya kwa kile alichokisema wachezaji hao kushindwa kujumuika katika kambi kwa wakati uliotakiwa.

Katika hili yuko sahihi, yeye ni kocha na mara zote makocha waliofanikiwa walifikia maamuzi na kuyasimamia, lakini kwa mtazamo wa kimpira tayari kocha huyo anaelekea kutengwa na upande Fulani, na jambo hilo halitaweza kumletea mafanikio yoyote.

Ndio, alihitaji wachezaji wote aliowaita wawepo kambini kabla ya Jumanne iliyopita ( Juzi) lakini ni mchezaji mmoja tu wa Simba aliyefika ndani ya wakati uliotakiwa. Golikipa namba moja Aishi Manula alijiunga na sehemu ndogo ya kikosi cha Stars siku ya Jumanne.

YUKO SAHIHI…..


Amunike yupo sahihi kuwaondoa wachezaji hao wa Simba kwasababu kama Aishi amefika kambini kwa wakati inamaanisha klabu yake haikuwa na pingamizi lolote sababu kama Simba ingegomea kuwaachia wachezaji wao bila shaka hata nyanda huyo hasingefika kambini. Hii inamaanisha, Erasto, Shiza, Kapombe, Dilunga na Mkude wamefanya hivyo kwa hulka zao wenyewe jambo ambalo ni utovu wa nidhamu.

Je, kocha huyo anaweza kuvumilia vitendo kama hivyo? Kwa mchezaji wa kulipwa kama yeye ambaye aliichezea klabu kubwa Ulaya FC Barcelona kwa mafanikio nyakati zake za uchezaji hawezi kuvumilia kuupuzwa na wachezaji.

Lakini bado ninapata mashaka kuwahukumu wachezaji hao wa Simba waliondolewa kwa sababu ukitoa Mkude, wengine- Erasto, Kapombe, Shiza na Dilunga hawana rekodi mbaya ya utovu wa nidhamu huko nyuma hivyo kuna uwezekano kukawepo na sababu zaidi ambazo zimepelekea kuondolewa kwao hivyo ilipaswa kwanza kocha huyo kukaa na kuzungumza na wachezaji hao na kama hasingeridhika na maelezo yao angewaondoa na si kuwaondoa kwa stahili aliyotumia.

KWANINI AISHI AMEWAHI?


Pengine kuwahi kambini kwa muda uliotakiwa kwa golikipa huyo namba moja wa Simba na Stars ndiyo kumempa sababu ya Amunike kuwaweka kina Erasto na wenzake katika kundi la watovu wa nidhamu, kwasababu haiwezekani mwenzao awasili kambini na wao wasifanye hivyo kwa kuwa kama ruhusu kutoka klabuni haiwezi kutolewa kwa mchezaji mmoja tu.

Aishi Manula

Nimekuwa nikisisitiza mara kadhaa kuhusu ‘kuheshimu muda’ kama tutaendelea kutoheshimu ‘MUDA’ bila shaka tutaendelea ‘kuwa wa hapa hapa milele’. Muda huu unapaswa kuheshimiwa na kila mmoja. Amunike ni kielezo tosha kuwa ni mtu anayeheshimu muda, lakini kwa mtazamo wangu ndani ya Shirikisho la Soka-TFF, na kwa baadhi ya wachezaji na watendaji wa klabu jambo hilo bado halijapewa kipaumbele kwa namna inavyotakiwa.

Nampongeza sana Aishi kwa maamuzi yake mazuri ya kimpira, amekuwa ni kijana mwenye nidhamu ndani na nje ya uwanja na kitendo chake cha kuwahi kambini Stars kimemuongezea alama nyingine nyingi.

TFF….


Inashangaza pale mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Boniphace Wambura anaposema wamehairisha kmichezo ya ligi kuu ambayo ilipaswa kufanyika kati ya Septemba mbili na tatu kwa sababu ya kocha wa Stars kuomba muda zaidi wa kuiweka timu yake kambini. Hii inamaanisha hata pale TFF bado hakuna anayeheshimu muda, sababu ni wao walipanga ratiba huku wakifahamu kuwa wiki ya pili ya Septemba Stars itakuwa na mchezo muhimu Kampala.

Kwa mazingira yetu, TFF ilipaswa kuona umuhimu wa kurefusha muda wa kambi ya timu ya Taifa si Amunike. Hivyo walichotakiwa licha ya kuwepo kwa kalenda ya Fifa na Caf, lakini walipaswa nao katika kalenda yao kuzingatia muda wa kambi ya Stars hivyo hawakupaswa kupanga ratiba yao ya michezo ya ligi kuu kati ya Septemba mbili na tatu.

Wakati mwingione hasa wakati huu ambao ligi kuu haina mdhamini ilipaswa kwani kitendo cha kuziambia klabu ‘hakutakuwa na mechi’ wakati ratiba inaonyesha zitakuwepo ni kuvuruga program za walimu na hata kama Simba ingewazuia wachezaji wake ilikuwa sahihi kwa sababu sheria za Fifa zinawapa uhuru klabu kuwashikilia wachezaji wao hadi masaa 48 kabla ya majukumu ya timu za Taifa.

Tazama, Alhamis hii nahodha Mbwana Samatta atakuwa katika majukumu ya klabu huko KRC Genk, vipi kuhusu Shaban Iddi, Farid Musa ambao klabu yao ya Tenerife itakuwa na michezo ya Segunda huko Hispania mwishoni mwa wiki hii? Je, hawa nao tuwaweke katika kundi la utovu wa nidhamu au kundi la wanaoheshimu muda klabuni kwao na program zilizopo?

Abdi Banda yeye alikuwa na mchezo wa ligi kuu ya Afrika Kusini jana Jumatano, labda pia kina Erasto, Mkude, Dilunga, Kichuya na Kapombe wameona bado walikuwa na muda wa kutosha kabla ya kujumika na wenzao, lakini hawakuheshimu muda waliotakiwa na kocha japo ni muda huo huo haukuheshimwa na TFF.

Beno Kakolanya, Kelvin Yondan na wachezaji wengine wa Yanga walioitwa Stars jana Jumatano walikuwa Kigali kuichezea klabu yao katika michuano ya Caf Confederations Cup hii inamaanisha bado kuna mahala tunakosea hasa watendaji wetu wa kimpira.

BUSARA….


Ni pigo kwenda Uganda bila wachezaji hao wazoefu na wenye mchango mkubwa kikosini. Sawa, Salum Kimenya ni namba mbili mzuri kikosini Tanzania Prisons, Salum Kihimbwa ni winga mzuri kikosini Mtibwa Sugar FC, Paul Ngalema ni mlinzi mzuri wa kushoto pale Mtibwa, David Mwantika ni mtu ambaye si mgeni katika beki ya kati pale Stars.

Hakuna shaka kuhusu ubora wa kiungo Frank Domayo anayetoka Azam FC na uzoefu wake katika michezo ya kimataifa, hata Kelvin Sabato amekuwa na miezi nane hadi kumi ya kuvutia pale Mtibwa lakini bado si sahihi kwenda Uganga bila Erasto, Kichuya, Kapombe, Dilunga, Kichuya na Mkude walio katika kiwango bora hivi sasa, lakini, je, ni sahihi kuwaondoa machaguo yetu ya kwanza kwa sababu zilizotolewa na Amunike?

Kapombe

Kama tunahitaji mafanikio huko na kama Amunike anahitaji kupata sapoti kutoka kila upande alipaswa kujiuliza kwanza kuhusu sababu zilizowachelewesha wachezaji hao japo hawajaheshimu muda ambao pia waajiri wake-TFF hawaku uheshimu ndio maana wamepanga ratiba ya ligi na kuipangua ghafla jambo ambalo linaharibu program za walimu klabuni.

Katika hili siwezi kuwa upande wa Amunike- ila naheshimu msimamo wake na nitapenda zaidi kuona akiusimamia, siwezi pia kuwa upande wa kina Erasto kwa sababu kwanini Aishi amefika kwa wakati kambini na wao wasifanye hivyo, lawama zote ni za TFF ambao wana-copy na ku-paste tu kalenda za Fifa na Caf bila kutazama ni utamuduni wetu katika soka la Tanzania na kambi za timu za Taifa.

Wako wapi kina Farid, Shaaban Iddi, Samatta, Himid Mao, Saimon Msuva na Abdi Banda? Siku ambayo kina Nyoni, Kapombe, Shiza, Dilunga na Mkude wanaondolewa Stars nyota wetu wa kimataifa wapo katika majukumu yao ya klabu ng’ambo ya nchi, kwanini? Ni kwasababu muda unaheshimu sana na wenzetu si wachezaji wala TFF yetu. Tubadilike.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x