Sambaza....

Joseph Omong, jina ambalo lilikuwa na ukakasi mkubwa ndani ya masikio ya mashabiki wengi wa Simba.

Hawakutaka kumsikia katika masikio yao, hata macho yao waliyatia upofu ili mradi wasimuone tu.

Ilikuwa inakera kwao kumuona Joseph Omong katika benchi la ufundi. Kwao wao hawakukumbuka rekodi ambazo Joseph Omong aliwahi kuziweka huko nyuma.

Hakuna aliyekuwa na kumbukumbu kuwa Joseph Omong alifanikiwa kubeba kombe la CAF akiwa na Leopards.

Hakuna aliyekuwa na kumbukumbu kuwa Joseph Omong aliingia kwenye orodha ya makocha watatu ambao walikuwa wanawania ukocha bora Afrika.

Kwa kifupi hakuna aliyekuwa anakumbuka chochote kuhusiana na mafanikio ya nyuma ya Joseph Omong.

Wengi hawakutaka kuyaimba kwa kujisifu mafanikio yake ambayo aliyapata katika timu nyingine, matamanio yao yalikuwa kumuona Joseph Omong akipata mafanikio na timu ya Simba.

Waliamini ilikuwa timu bora yenye wachezaji bora ambao walisajiliwa kwa gharama kubwa.

Walitaka kuona gharama za usajili zikionekana ndani ya uwanja. Walitaka kuona nyasi za viwanja mbalimbali zikifurahia kwa soka la mahaba kutoka timu ya Simba.

Urembo kwenye mpira ulikuwa nguzo ya furaha ya mashabiki wa Simba. Hawakutaka kuona timu ikishinda katika mazingira magumu, mazingira ambayo timu ilipata ushindi mwembamba tena timu ikicheza soka lisilo la kuvutia.

Hapa ndipo ugomvi ulipokuzwa, ugomvi ambao uliwafanya mashabiki wa Simba wawe na nguvu kuzidi Joseph Omong.

Maisha yake Msimbazi yaliisha, akaondoka na kuwapisha wengine waje kujaribu.

Aliondoka na kuwaacha mashabiki wa Simba wasubiri nani anaweza kuja kukaa kwenye kiti ambacho Joseph Omong alishindwa kukikalia na kuwapikia chakula kitamu.

Masoud Djuma alikuja Dar es salaam, tena alikuja na historia nzuri. Historia ya kuipa Rayon Sports ubingwa wa ligi ya Rwanda.

Tena akiwa kocha kijana, kitu hiki kilikuwa kivutio kwa wengi.

Waliamini kwa dunia ya sasa ni vizuri kuwa na kocha kijana ili aweze kuelewana na wachezaji ambayo kiumri ni vijana.

Picha wa makocha waliaonza kupata mafanikio wakiwa kwenye umri mdogo ilianza kuwepo kwenye vichwa vya mashabiki wa Simba.

Walimkumbuka Jose Mourinho na FC Porto yake, kabla hawajamaliza kumkumbuka Jose Mourinho picha Pep Guardiola ilikuja kichwani mwao.

Walimuona Masoud Djuma atakuja kuwa kocha mwenye mafanikio makubwa akiwa na umri mdogo, umri ambao ulimwezesha Zinedine Zidane kushinda kombe la Klabu bingwa ulaya mara tatu na ndiyo umri ambao Mauricio Pochettino anatengeneza bomu la nyuklia pale White Hart line.

Ndiyo umri ambao wengi waliuamini kupitia ngozi ya Masoud Djuma. Walimkaribisha vizuri.

Imani ilizidi kuongezeka kwake baada ya kuifanya Simba icheze soka ambalo wengi walikuwa wanalitamani tena timu ikishinda magoli mengi.

Kuna wengi walitamani kumuona Masoud Djuma akibaki kama kocha mkuu, hawakutaka kuzisikia hàbari za ujio wa kocha mpya aliyekuwa anasemekana yuko njiani.

Pierre Lenchantre alikuja lakini hakukaa sana akaondoka na kumwacha Masoud Djuma akimsubiri kocha mwingine mkuu ambaye atakuwa anamsaidia kimajukumu.

Kocha ambaye mpaka sasa hajaonekana kuwafurahisha mashabiki wengi kwa sababu anaifanya Simba ionekane katika picha ya Simba ya Joseph Omong.

Wengi hawafurahishwi na Simba hii kwa sababu kocha hajagundua kitu sahihi cha kuwapa mashabiki wa Simba na kwa bahati mbaya kitu hicho anakijua Masoud Djuma.

Masoud Djuma ambaye yuko Julia kwake kama msaidizi, Masoud Djuma ambaye alipewa Ufalme kabla ya ujio wa Patrick Aussems.

Djuma katika majukumu yake

Na ndiyo kocha ambaye Ufalme wake ulisimikwa kabla hata Pierre Lenchantre hajafika katika ardhi ya Dar es Salaam.

Masoud Djuma alijua jinsi ya kucheza na akili za watu wa Simba ndiyo maana atabaki kuwa kocha kipenzi kuzidi kocha mkuu.

Inawezekana Pierre Lenchantre na Patrick Aussems wana historia nzuri na bora ya ufundishaji kuzidi Masoud Djuma lakini kwa mashabiki wa Simba Masoud Djuma ni bora kuzidi hawa wawili.

Alishajiwekea Ufalme wake awali na anaaminika sana ila bado kitu kimoja tu.

Bado siku ambayo Ufalme wa Masoud Djuma utadhihirishwa rasmi, na hiki ndicho kitu ambacho Masoud Djuma anakisubiri.

Yuko pale Simba akisubiri siku ambayo atatangazwa kuwa Mfalme halali wa nchi ya msimbazi.

Nchi ambayo wananchi wake wanampenda na kumwamini sana kuliko Mfalme wa sasa

Sambaza....