Sambaza....

Chama cha soka mkoa wa Dar es Salaam kimeipongeza klabu ya soka ya Simba kwa kufanikiwa kutinga hatua ya makundi ya ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa jumla ya mabao 4-3 dhidi ya Nkana FC ya nchini Zambia.

Akitoa pongezi hizo kwa niaba ya DRFA katibu mkuu Msanifu Kondo amesema walichokifanya Simba mbali na kulitangaza Taifa lakini pia wameutangaza mkoa wa Dar es Salaam na kuwathibitishia umma kwa namna ambazo mkoa huo umezidi kujiimarisha katika kukuza soka.

“Napenda kutoa pongezi kwa uongozi Simba, viongozi, wanachama, wachezaji na Watanzania wote, Simba wamefanya tukio kubwa sana, maana mara mwisho ilikuwa ni mwaka 2003 kama chama tunasema tupo pamoja nao na tutazidi kushirikiana nao,” amesema.

Amesema jambo ambalo wamelifanya Simba pia si dogo kwani kwa miaka mingi Tanzania imeshindwa kufika hatua hiyo na amewaombea kufika mbali zaidi kama walivyowahi kufanya hivyo miaka ya nyuma walipocheza fainali za Afrika.

“Tutaendelea kuhakikisha kuwa katika hatua ya makundi wanazidi kufanya vizuri, kama uongozi tunajua kadiri wanavyozidi kusonga mbele ndivyo wanapoenda kukutana na timu ngumu, naamini hata uongozi wa Simba wanalijua hilo na watakuwa na mikakati mizuri ili kufika mbali pengine zaidi ya pale walipofika mwaka 2003,” Kondo amesema.

Simba walifanikiwa kuwaondoa  Nkana licha ya kupoteza kwa mabao 2-1 katika mchezo wa awali, kwani katika mchezo wa duru ya pili walifanikiwa kupata mabao matatu kupitia kwa Jonas Mkude, Meddie Kagere na Clatous Chama mabao ambayo yamewafanya kufudhu hatua ya Makundi.

Mara ya mwisho Simba kucheza hatua ya Makundi walipangwa kundi A pamoja na timu za Enyimba, Ismaily na ASEC Mimosas ambapo walishika nafasi ya tatu baada ya kukusanya alama saba, alama nne pungufu ya Yule aliyeshika nafasi ya pili ambapo kama wangeshika nafasi hiyo wangetinga hatua ya nusu fainali.

Hatua ya Makundi inatarajiwa kupangwa Disemba 28 mwaka huu na timu nyingine zilizofuzu hatua hiyo ni pamoja na Esperance Tunis, TP Mazembe, Orlando Pirates, Mamelodi Sundowns, CS Constantine, FC Platinum, Ismaily SC, Lobi Stars, Wydad AC, Al Ahly SC, AS Vita Club, JS Saoura, ASEC Mimosas, Horoya AC na Club Africain.

Sambaza....