Sambaza....

NILIKUWA na imani kubwa kwa Lesotho kupata ushindi dhidi ya Tanzania katika mchezo wa tano wa kundi la mwisho kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za kombe la Mataifa ya Afrika 2019 (michuano itakayo nchini Cameroon)

MIPANGO

Kwa sababu za kimpira, mechi ya Jumapili huko Maseru ilikuwa ngumu tangu Oktoba 18 wakati Taifa Stars walipoichapa 2-0 Cape Verde Islands jijini Dar es Salaam.

Kama ilivyo sasa, Stars ikiomba Cape Verde waifunge Lesotho katika mchezo wa mwisho wa kundi L huko Prahia mwezi Machi mwaka ujao, Lesotho nao walikuwa bize mwezi uliopita kuwaombea Stars ushindi au matokeo ya sare vs Cape Verde.

Ni hesabu ambazo tayari zimetoa matokeo chanya upande wa Lesotho kwa maana Stars iliifunga Cape Verde- jambo ambalo kimkakati lilikuwa muhimu sana kwa Lesotho.

Hesabu za Stars zitaleta faida? Baada ya kuifunga Cape Verde mwezi uliopita na Lesotho kuchapwa nyumbani 2-0 na Uganda, Stars ilifanikiwa kupanda hadi nafasi ya pili katika kundi- pointi tano nyuma ya viongozi Crannes waliokuwa na alama kumi baada ya kila timu kucheza michezo minne.

Maombi ya Lesotho kwa Stars mwezi uliopita yalikuwa na mikakati. Kinadhalia, baada ya kuchapwa 3-0 Kampala, Oktoba 12, Lesotho waliona ugumu wa kupata walau alama moja katika game zao mbili na Crannes.

Wakahitaji game ya Tanzania na Cape Verde imalizike kwa sare ama Stars kushinda ili kuizuia Cape Verde isiwaondoe katika mbio za kufuzu.

Kumbuka michezo ya mzunguko wa tatu katika kundi ilimalizika kwa Cape Verde 3-0 Tanzania, Uganda 3-0 Lesotho. Hivyo kama Cape Verde wangeshinda Dar es Salaam wangefikisha pointi saba- alama moja zaidi ya Lesotho kama wangeshinda michezo yote miwili ya mwisho- Lesotho v Tanzania, Cape Verde v Lesotho.

Matokeo ya mzunguko wa nne katika kundi yalimaanisha Crannes walikuwa na zaidi ya 90% za kufuzu. Na timu za Tanzania ( pointi tano), Cape Verde ( pointi nne) na Lesotho (pointi mbili) zote zina nafasi ya kumaliza nafasi ya pili.

Mpango wa Lesotho ulikuwa ni kuimaliza Tanzania jana na matokeo ya ´wenyewe kwa wenyewe´ yatawafanya wawe juu ya Stars katika msimamo.

Wakati huo huo walikuwa wakiombea mabaya Cape Verde pale Kampala siku moja kabla ya kuivaa Stars. Wamefanikiwa: Stars iliichapa Cape Verde, Oktoba, Crannes wakashinda 1-0 Cape Verde juzi Jumamosi, na wao wakaichapa Stars jana Jumapili.

Vumelo Khutlang akikosa goli mojawapo la wazi wakati wa mechi.

Hesabu zao ziliambatana na mikakati. Walijitazama na kuona baada ya sare ya 1-1 nyumbani vs Cape Verde, Oktoba 13, na kipigo cha 2-0 nyumbani kutoka kwa Crannes mwezi uliopita, waliamini wanaweza kuifunga Tanzania mwezi huu kama watajituma na kupunguza makosa yao katika ngome.

Hesabu za mpira hutimia pale timu inapokuwa na nia itakayoambatana na mbinu, ufundi, utimamu wa mwili na kiakili- bila kusahau hamasa ya wachezaji ndani ya mchezo.

Tanzania ilikwenda Lesotho na kauli mbiu ´Ni zamu yetu Afcon´. Ni uongo, Stars bado ina safari ndufu kufikia kufuzu kwa CAN ya kwanza baada ya miaka zaidi ya 38 walipofuzu kwa fainali za Nigeria mwaka 1980 (kabla ya kuzaliwa kwangu)

Uganda

Stars inalazimishwa kupita njia ya mkato kufuzu Mataifa ya Afrika. Nadhani tunapaswa kuendelea kusubiri kwanza ili wenye dhamana ya kuongoza, kuendesha na kusimamia mchezo huu wajifunze. Cape Verde ama Lesotho wanastahili kuungana na Uganda kwa safari ya Cameroon mwakani.

Nitaelezea wakati ujao panapo majaliwa kwanini timu hizo mbili zinastahili kufuzu badala ya Stars ambao hata hesabu za soka zinawashinda! Kulikuwa na sababu gani ya kulazimisha ushindi Maseru? Hesabu za mpira zilihitaji sare pale. Ingetosha mno.

Na wakati Tanzania ikiomba Cape Verde ashinde vs Lesotho Machi mwakani, ni lazima ikumbukwe kipa na nahodha wa Uganda, Dennis Onyango ndiye nyanda pekee asiyeruhusu nyavu zake kufikiwa na mpira baada ya makundi yote 12 kukamilisha mzunguko wa tano katika kampeni hii ya kwenda Cameroon.

Kama soka ni hesabu, Stars itaenda Cameroon kwa mgongo wa Cape Verde, lakini kimpira ni Lesotho au Cape Verde watakaoungana na Uganda kwa sababu si rahisi kumfunga ´Captain Onyango´ ambaye amewaongoza wenzake kushinda michezo yao yote miwili ya ugenini ( Cape Verde 0-1 Uganda, Lesotho 0-2 Uganda)

Sambaza....