Blog

Mkude na Ajib hawatamani tunachokitamani!

Sambaza kwa marafiki....

Viungo bora, hodari na wenye vipaji vya kipekee. Unaweza kuchagua neno lolote lile utakalolipenda ili kuonesha umahiri wa hawa watu na ukawa sahihi kabisa.

Watu ambao wamefanikiwa kujipenyeza kwenye mioyo ya waliowengi kwa sababu tu ya vipaji vyao walivyo navyo kwenye miguu yao.

Miguu yao imebarikiwa, akili zao zimetunukiwa zikiwa ndani ya uwanja lakini zikiwa nje ya uwanja zimekuwa katika kiwango cha chini tofauti na akili za ndani ya uwanja.

Ni mara ngapi umesikia Jonas Mkude na Ibrahim Ajib wamekuwa watovu wa nidhamu?, nadhani ni wimbo ambao umedumu sana tena kwa kipindi kirefu.

Mkude

Ni wimbo ambao umezoeleka sana kwenye masikio yetu. Limekuwa jambo la kawaida sana masikio yetu kusikia kuwa Ibrahim Ajib na Jonas Mkude ni watovu wa nidhamu.

Na hiki ndicho kisa kikubwa cha Jonas Mkude kuvuliwa kitambaa cha unahodha ndani ya Simba. Wakati niko Mwanza nishawahi kukutana na Jonas Mkude kwenye kumbi moja ya starehe mida ya usiku wa manane wakati ambao alitakiwa kucheza mechi kesho yake.

Usiku wa manane ametoroka kambi, na anatakiwa apate muda mwingi wa kupumzika kwa ajili ya mechi ya kesho yake lakini muda huo ndiyo kwanza alikuwa kwenye kumbi moja kubwa ya starehe tena usiku wa manane.

Ndipo hapo unapoanza kufikiria aina ya mchezaji kama huyu anafikiria nini ?, anawaza nini kuhusu kipaji chake?. Kuna siku ashawahi kuwaza kufika mbali kupitia kipaji chake ?

Utaanzaje kufika mbali wakati nidhamu haiko karibu na wewe ? Ni kitu ambacho ni kigumu sana na ndicho kitu ambacho huwa kinawafanya makocha wengi kuwaadhibu hawa.

Ajib

Na kipindi ambacho wanaadhibiwa ndicho kipindi ambacho mashabiki wengi hupaza sauti zao kwa kuwatetea na kuwalalamimia makocha bila kufahamu tatizo ambalo liko nyuma yake.

Leo hii tunaweza kumlaumu sana kocha Emmanuel Amunike kwa kuwaacha hawa wachezaji wawili, lakini hatuwezi kufikiria tatizo lililo nyuma ya hiki kitu.

Tukumbukeni ameacha wachezaji ambao makocha wengi wamewahi kulalamikia nidhamu yao. Siyo mara ya kwanza kwa wachezaji hawa kufanya makosa ya kinidhamu na wakaadhibiwa.

Stars wakiwa Misri

Tumekuwa tukitamani sana kuwaona Ibrahim Ajib na Jonas Mkude wakifanikiwa kwenye mpira wa miguu lakini wao hawaoni kama wanatakiwa kufanikiwa.

Wanaenda kinyuma na matarajio yetu. Ndiyo maana mara nyingi hutenda matendo ambayo huwasababishia wao kurudi nyuma kwenye hatua ya mafanikio.

Kwenye michuano ya Afcon walitakiwa kwenda kujiuza. Hawakuona fursa iliyopo kwenye hii michuano ya Afcon. Na inawezekana kabisa hawaumii kuachwa kwao kwenye kikosi.

Hapa ndipo umuhimu wa kuwa na wasimamizi bora wa vipaji vya wachezaji unapohitajika. Wanahitajika watu ambao wanaweza kuwasimamia wachezaji hawa ili kufikia mafanikio ambayo wengi huyatamani.

Tafadhali tumia viungo vya mitandao ya jamii kusambaza.