Blog

Ni sahihi kushangilia suluhu ya Stars Kampala, ..wakati Dar ni ‘nyanya’ na utendaji mbovu?

Sambaza....

NI sahihi kufurahia suluhu-tasa dhidi ya Uganda jijini Kampala, lakini kama hatutabadili kwa dhati mtazamo wetu wa ndani- matumizi ya uwanja wa nyumbani hakuna ambacho kitapatikana upande wa Taifa Stars.

Si vizuri kuzungumzia kuhusu wachezaji walio nje ya timu, lakini kwa kiwango cha uchezaji wa Shiza Kichuya, Erasto Nyoni , Jonas Mkude, Shomari Kapombe na John Bocco vingeweza kuzalisha kitu cha ziada kwa Stars pale Namboole lakini mtu mmmoja ndani ya Shirikisho la Soka alisababisha timu kukosa mchango wa wachezaji hao.

Licha ya kujituma mno katika kipindi cha pili, lakini kwa kipindi chote cha kwanza Thomas Ulimwengu alikuwa hana msaada katika timu, Frank Domayo alifanya Mudhari Yahya kukosa umakini zaidi na hivyo kuifanya Uganda kutawala eneo hilo kutokana na uwezo mdogo wa viungo hao katika kupiga pasi timilifu na kupandisha mashambulizi.

Tom, aliwapa uhuru mkubwa walinzi wa kati wa Cranes kwa sababu alishindwa kubaki katika eneo lake kama mshambulizi wa kwanza wa kati. Domayo hakuwa akionekana katika kuzuia mipira na pasi za Uganda, mara nyingi alionekana pale alipopoteza mpira jambo ambalo lilimchosha haraka Mudathir huku likimfanya Gadiel Michael ambaye kimsingi alipaswa kubaki pembeni zaidi akiingia eneo lisilo lake mara kadhaa na kupelekea ;pia pasi za Abdi Banda kutokwenda katika muelekeo sahihi.

Ilikuwa ni mechi ya kwanza ya Amunike akiisimamia Stars na jambo zuri nililojifunza kwake ni kwamba anaweza kuwapandisha kiwango wachezaji wake. Baada ya kurudi kipindi cha pili, Tom alikuwa imara zaidi na kipa Denis Onyango ambaye hakuwa amechufuka kwa saa nzima aliyoitumia katika uwanja uliojaa maji, akaanza kuona hatari na mara mbili au tatu Tom alikuwa karibu kumuadhibu.

Domayo ambaye alicheza kwa robo tatu ya mchezo alipandisha kiwango chake katika utulivu na muda wote wa zaidi ya dakika 20 za kipindi cha pili alikuwa bora katika upigasi pasi na sasa alionekana mara nyingi katika utibuaji wa mipira na pasi zenye madhara za Cranes. Hii ndiyo sababu ya kumjua kocha mwenye mwelekeo, na Amunike licha ya kuwakosa wachezaji ambao angeweza kunufaika nao ameonyesha ana kitu ambacho kinawezekana kuipa Stars nafasi ya kufuzu CAN 2019-Cameroon.

UTENDAJI MBOVU

Haihamasishi kuona mchezaji au wachezaji Fulani wanaoweza kuisaidia timu ya Taifa kwa wakati husika wakishindwa kufanya hivyo kwasababu tu kuna mtu/watu wanaosukumwa na kufanya hivyo kwa maslai yao binasfsi.

Vyovyote unavyoweza kusema kwa kiwango kile cha jana kilichoonyeshwa na Cranes, Bocco, Kichuya, Kapombe, Nyoni na Mkude wangekuwa msaada mkubwa zaidi kwa Stars lakini utendaji kazi mbovu ndani ya Shirikisho kumewaangusha.

John Bocco

KUTUMIA VIZURI UWANJA WA NYUMBANI….

KUTOA SARE DHIDI YA Uganda tena nyumbani kwao ni jambo la kufurahisha na kama ni malengo basi timu inabaki katika mtazamo uleule wa kufuzu. Faida ya suluhu hii ni kwamba Uganda na Tanzania zimebaki zikipisha kwa alama mbili. Cranes wana pointi nne na Stars wana pointi mbili kila timu imecheza game mbili.

Matokeo yoyote ya mchezo mwingine wa kundi hilo L utakaochezwa Lesotho kwa kuwakaribisha Cape Verde hayataiathiri sana Stars labda kama wangepoteza Kampala. Lesotho wakishinda watafikisha alama nne sawa na Uganda kwa sababu walifanikiwa kupata sare ya 1-1 jijini Dar es Salaam katikla mchezo wa kwanza dhidi ya Stars.

Cape Verde ambao ni wapinzani wajao wa Stars ( Oktoba 10) wakishinda watafikisha alama tatu kwani ndiyo timu pekee katika kundi iliyopoteza nyumbani tena wakichapwa 1-0 na Uganda juni mwaka uliopita.

Sare ( Lesotho vs Cape Verde leo Jumapili) itakuwa matokeo sahihi zaidi kwa Stars, lakini je, kuna uwezekano wa kupata alama zote sita vs Cape Verde ( Oktoba 13) na Cranes Machi 22, 2019 katika ardhi ya nyumbani? Zikipatikanma inamaanisha Stars itafikisha alama nane kwa mwenendo wa kundi jinsi ulivyo timu yenye poitni nane –kumi inaweza kufuzu kutoka katika kundi hili.

Uganda wanaweza kufikisha alama kumi kama watashinda michezo yao miwili ya nyumbani ( vs Lesotho, Oktoba 10, na Cape Verde, Novemba 16) hakika pointi tatu walizopita Cape Verde zinawabeba mno hata kama watapoteza Dar Es Salaam na Lesotho katika michezo mingine miwili ya ugenini. Wakati Stars ikiwasimamisha inamaana wameshindwa kufungua gape la pointi kufikia tano baada ya michezo miwili tu.

Cape Verde wanaweza kukusanya alama sita nyumbani, watakuja Dar na kwenda Kampala, kama hawatashinda wala kutoa sare ugenini Leo watakuwa hatarini kwasababu wana alama sita tu ambazo kama watacheza vizuri nyumbani kwao vs Stars na Lesotho zitawafanya waongeze alama sita tu. Stars inapaswa kuongeza umakini katika uwanja wa nyumbani kwasababu ndiyo mahali pekee panapokupa ongezeko kubwa la pointi.

Ni sahihi kushangilia sare vs Uganda pale Namboole? Hapa, tunapaswa kushinikiza matokeo katika michezo ya nyumbani na kuwaondoa watendaji wabobvu kama wale waliowadanganya kina Bocco, Kichuya, Shiza, Hassan Dilunga, Kapombe na Mkude muda waliotakiwa kuripoti kambini. Vinginevyo hakuna mafanikio zaidi muendelezo wa ‘homa ya vipindi’. Bado inakera, hata kama ni mafanikio kwa wengine.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x