Blog

Niliwahi kumuona “GUARDIOLA” Kwenye mwili wa “DJUMA”.

Sambaza....

Historia iliwahi kuniaminisha kuwa Joseph Omong atafanya vizuri katika klabu ya Azam Fc. Nilikuwa na imani kubwa sana juu ya hili. Kwanini niliamini hivi ?, Azam Fc ilimchukua kocha ambaye aliwahi kushinda kombe la shirikisho barani Africa akiwa na AF Leopards.

Niliamini kupitia mafanikio haya, niliamini Azam FC wamemchukua kocha ambaye ni mshindi, kocha ambaye ana uzoefu mkubwa na mpira wa Afrika. Na kwa kuzingatia kuwa Azam Fc walikuwa wameweka uwekezaji mkubwa ndani ya timu yao, imani yangu ilizidi kuimarika kuwa huyu atafanya vyema.

Timu ambayo huwezi kusikia malalamiko ya wachezaji kucheleweshewa mishahara, timu ambayo ilikuwa na miundombinu mizuri ya kumfanya kocha na wachezaji wake wafanye vizuri.

Kwa kifupi Joseph Omong aliletwa sehemu ambayo ni tulivu sana!, sehemu ambayo ingemhakikishia yeye kufanya vyema na timu ya Azam FC.

Lakini mwisho wa siku haikuwa vile kama nilivyokuwa nategemea!, Joseph Omong alishindwa kuifanya Azam FC kufanya vyema kwenye michuano ya kimataifa. Hakukaa muda mrefu sana akawa amefukuzwa pale Chamazi!, akili yangu haikutaka kukubaliana na uhalisia kuwa Joseph Omong ameshindwa kufanya vyema pale Azam FC.

Macho yaliiambia akili yangu kuwa Joseph Omong ameshindwa!, akili yangu ilipingana sana na taarifa ile ambayo macho yangu yalikuwa yanaifikisha!.

Nilijipa sababu nyingi sana za kumtetea Joseph Omong, nilijiaminisha kuwa labda hakupewa muda wa kutosha wa kusoma mazingira ya mpira wetu.

Hakupewa muda wa kutosha wa kutengeneza timu yake ya ushindi pale Azam FC!, huu ndiyo ulikuwa utetezi wangu mkubwa kwa Joseph Omong kwa sababu nilikuwa naamini sana kupitia uwezo wake.

Niliamini alikuwa na uwezo wa kufanya makubwa kama aliyoyafanya pale AFC Leopards, majonzi yaliuvaa moyo wangu baada ya kuona Joseph Omong anaondoka kwenye ramani ya soka la Tanzania.

Soka ambalo lilikuwa linamwihitaji sana kwa mujibu wa mtazamo wangu. Nilibaki nikiwa nimenyong’onyea sana!, muda mwingi nilikuwa na uhuzuni kubwa moyoni mwangu kutokana na kufukuzwa kwa Joseph Omong kana kwamba alikuwa ndugu yangu wa damu!.

Kumbe tuliunganishwa na damu moja tu, damu ya mpira, damu ambayo imebeba ndugu kote duniani. Damu ambayo inatoka katika ukoo mkubwa kuzidi ukoo wowote duniani, ukoo ambao unafuatiliwa sana kwa karibu na watu wote.

Ndiyo ukoo ambao umeifanya Simba Sc kuwa moja ya wanafamilia wa mpira wa miguu, ndiyo ukoo ambao ulisababisha Simba Sc kumrudisha tena Joseph Omong katika ardhi ya Tanzania.

Ardhi ambayo nilikuwa naona kabisa inahitaji uwepo wa Joseph Omong. Huzuni yangu ya awali ilifutika ghafla !, kwa ghafla furaha likawa vazi rasmi la kwenye mwili wangu.

Nikawa na furaha tena, tabasamu lilivaa uso wangu. Muda mwingi nikawa natabasamu, yote haya ni kwa sababu Joseph Omong alikuwa kwenye ardhi ambayo nilitaka awepo.

Ardhi ambayo inahitaji watu waliofanikiwa ili na sisi tufanikiwe zaidi. Ardhi ambayo mbegu ya mafanikio haikuwahi kufikirika kama ndiyo mbengu ambayo tunatakiwa kuipanda!. Ardhi ambayo kila mvua ya mafanikio ikinyesha hukuta ardhi ikiwa tupu haina mbegu yoyote ya mafanikio iliyopandwa, kwa sababu tu hatujawahi kupata mpandaji mzuri wa mbegu hizo.

Mpandaji mzuri niliyekuwa namtamani na nilimuona anafaa sana ni Joseph Omong. Msimbazi ndiko kukawa sehemu yake mpya ya kuweka makazi. Sehemu hii siyo tulivu sana kama palipokuwa kule Chamazi.

Nilianza kupata hofu kama ataweza kufanya vyema sehemu ambayo ina kelele kila kukicha!, nilijipa imani kuwa anaweza! Nikaamini kabisa anaweza. Lakini ilikuwa kinyume kabisa na mategemeo yangu ya awali.

Hakuweza kufanya vyema mpaka akawapendeza watu wa Msimbazi!, hakuwavutia, na hakuwahi kuwashawishi kuwavutia!. Hapo ndipo mlango wa kutokea ulipofunguliwa zaidi.

Akaondoka!, kwa mara ya pili akawa ameshindwa kufanya vyema akiwa Tanzania!. Iliniuma sana kwa sababu historia ilikuwa inambeba sana kufanya vyema lakini kwa wakati huo historia haikuwa upande wake tena!.

Aliondoka sehemu ambayo wengi hawakupendezwa naye, ndipo hapo alikuja mtu ambaye alikuja kupora mioyo ya walio wengi. Mioyo ambayo ilikuwa inatamani kuona timu bora na inayocheza vizuri.

Mioyo ya wengi ilitulia na kupiga goti kwa kumshujudia Masoud Djuma “Irambona”. Huyu akawa Mungu wa Msimbazi. Alipata wafuasi wake ambao walikuwa wanaamini kupitia yeye tu. Hawakuamini kupitia mwingine tena.

Hata walipoletewa Pierre Lechantre hawakuata kabisa kumuelewa. Huyu alishinda Afcon akiwa na Cameron lakini hakuaminiwa na kueleweka kabisa.

Kila jicho lilikiri uwezo wa Masoud Djuma ” Irambona”, kila goti lilipigwa chini kushujudia uwezo wa Masoud Djuma “Irambona” na kila kunywa kili kiri kuwa huyu ndiye Bwana wa mpira.

Alikuwa bwana wa mpira haswaaa!, alikuwa kijana mdogo ambaye alijua nini maana ya soka la kisasa. Kwa kifupi alijua kabisa mahitaji ya soka la kisasa.

Ndiyo maana ilikuwa mshangao wa wengi kwake yeye kuja na mfumo wa 3–5-2 na timu ikacheza vizuri na ikafanya vyema. Mfumo ambao ni mpya hapa kwetu. Lakini ni mfumo wa kisasa.

Hakuogopa kuwekeza kwenye hiki kitu kabisa!, uoga ulikuwa mbali sana na kiini cha moyo wake. Ujasiri ndilo vazi lililokuwa limefunika ngozi ya mwili wake. Na kwa ujasiri huo aliifanya timu icheze kwa kujiamini sana na kufanya vyema. Ndiyo maana kila nilipokuwà namtazama nilikuwa namuona Pep Guardiola kwenye mpira wetu!.

Sambaza....
Subscribe
Notify of

0 Maoni
Inline Feedbacks
Tazama Maoni Yote
0
Tungependa kupata maoni yako, tafadhali tuambiax
()
x