Sambaza....

Katibu mkuu wa klabu ya soka ya Stand United Kenny Nyangi amesema klabu haijaridhishwa na nafasi ambayo wameishika katika msimu wa ligi kuu soka Tanzania Bara uliofikia tamati Jumatatu ya Mei 28, 2018.

Nyangi amesema kama klabu ni lazima wajiulize kwanini wamemaliza katika nafasi ya chini kuliko timu za Lipuli na Singida United ambazo zimepanda daraja msimu hivyo wanapaswa kujitafakari na kuona kama wanastahili kuwepo katika nafasi kama hizo msimu ujao.

“Kwa kweli ni jambo la aibu kwetu Stand United ambao tunaenda msimu wa tano mfululizo katika ligi kuu, si jambo zuri kumaliza chini ya timu kama Lipuli na Singida United ambazo ni timu mpya, nafasi tuliyoipata msimu huu itakuwa changamoto kwetu ili kuona njia gani tunafanya kumaliza katika nafasi za juu zaidi, hata ya tano au ya nne msimu ujao,” Nyangi amesema.

Stand United yenye maskani yake mkoani Shinyanga ilipanda daraja msimu wa 2014/2015 na katika msimu huo wakanikiwa kushika nafasi ya 10 wakiwa na alama 31, msimu wa 2015/2016 walifikisha alama 40 katika nafasi ya saba huku 2016/2017 wakimaliza na alama 38 katika nafasi ya 6.

Stand United ambayo ilianza vibaya msimu huu kwa kucheza takribani michezo mitatu bila kupata ushindi wala sare yoyote wamefanikiwa kumaliza katika nafasi ya 11 wakiwa na alama 32 baada ya kushinda minane kati ya 30 ambayo wamecheza.

Sambaza....